Twatembelea Nyika Kubwa Nyeupe
Barua Kutoka Norway
Twatembelea Nyika Kubwa Nyeupe
NI ASUBUHI, mwanzoni mwa majira ya baridi. Tunachungulia dirishani kuona jinsi hali ya hewa ilivyo. Tunasisimka kama nini kuona anga jangavu la rangi ya bluu! Tunaenda kuhubiri kwa siku tatu kwenye eneo kubwa tambarare juu ya mlima wa Finnmarksvidda, ulio katika Mzingo wa Aktiki.
Nchini Norway, kunakuwa na baridi kali sana wakati wa majira ya baridi, kwa hiyo tunasitasita kwenda kwenye nyika ya kaskazini. Lakini tunafurahi kwamba tunasafiri pamoja na Mashahidi wa Yehova watatu ambao wanaishi katika eneo hilo. Wanajua hali zinavyokuwa na wametupa ushauri mzuri.
Barabara ni chache na njia iliyo bora ya kuwafikia watu wanaoishi katika maeneo ya mbali ni kutumia kigari kinachoendeshwa juu ya theluji. Tunapakia chakula, mafuta ya ziada ya gari, na mavazi kwenye magari yetu na kwenye kigari cha kukokotwa. Mbele yetu tunaona eneo kubwa tambarare juu ya kilele cha mlima Finnmarksvidda, ambalo limefunikwa kwa theluji. Theluji hiyo inang’aa kama almasi inapopigwa na miale ya jua. Mandhari hiyo ni maridadi sana!
Mlima wa Finnmarksvidda una wanyama kama vile mbawala, kongoni, simba-mangu, sungura, mbweha, mbwa-mwitu, na dubu wachache. Lakini tamaa yetu kubwa ni kuwafikia watu wanaoishi katika eneo hilo la mbali. Tunatamani sana kukutana na baadhi ya Wasami, ambao wanapata riziki yao kwa kuwinda mbawala na kufanya kazi kwenye mikahawa iliyo kwenye mlima huo.
Nje ya mkahawa wa kwanza, tunakutana na wanafunzi kadhaa vijana ambao wanashiriki katika mashindano ya kuteleza kwenye theluji. Wanasimama ili kuzungumza nasi na wanatuuliza tunachofanya. Tunafurahi kuwaeleza. Kisha tunapoondoka, mmoja wao anatuambia hivi: “Tunawatakia mema katika kazi yenu!” Tunapanda kwenye magari yetu tena, na kusafiri juu ya ardhi iliyofunikwa kwa theluji na maziwa yaliyoganda. Je, tutamwona mbawala?
Tunapokaribia nyumba fulani ndogo, mwanamume mmoja anatusalimu kwa tabasamu. Yeye ni mkaaji wa eneo hilo. Anapoona kwamba kigari chetu kimevunjika, anajitolea kwa fadhili kukirekebisha. Anafanya kazi hiyo polepole kwa kuwa watu hapa hawana haraka. Hivyo, anafanya tuhisi tumestarehe pia. Tunamshukuru anapomaliza kurekebisha kigari hicho na tunamweleza mambo
machache kutoka katika Biblia kuhusu sababu inayofanya Mungu aruhusu watu wateseke. Anasikiliza kwa makini na kabla hatujaondoka, anakubali kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? na magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Anatabasamu na kusema, “Asanteni kwa kunitembelea.”Baada ya kuwatembelea watu kadhaa, giza linaanza kuingia, na tunaanza safari ya kurudi kwenye nyumba yetu ndogo ambapo tutalala. Kwa ghafula tunamwona mbweha. Manyoya yake mekundu yanametameta anapotembea juu ya theluji nyeupe. Mnyama huyo anasimama kwa muda na kututazama kana kwamba anajiuliza hawa ni akina nani, kisha anaenda zake. Sasa theluji imeanza kuanguka, na inakuwa vigumu kuona vizuri. Hatimaye, tunafurahi kama nini tunapoona nyumba yetu! Tunawasha moto kwenye jiko na pole kwa pole nyumba inapata joto. Ingawa tumechoka kwa sababu ya kurushwa-rushwa na gari, tuna furaha.
Usiku unapita haraka sana. Tunapakia mizigo yetu kwenye gari na kuelekea eneo la chini. Tunafuata mto fulani, na kufika kwenye mkahawa mwingine wa mlimani. Hapa tunakutana na mwanamume kijana na tunazungumza naye kuhusu mambo kadhaa yenye kujenga kutoka katika Biblia. Kwa fadhili, anatuonyesha njia itakayotufikisha kwa urahisi kwenye njia kuu.
Siku ya mwisho ya ziara yetu inafika. Tunapoingia kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Stabbursdalen, tunaona mandhari nzuri sana. Tunaona pia milima yenye theluji inayometameta inapopigwa na miale ya jua. Kisha, mbele yetu tunaona kundi kubwa la mbawala! Wanalisha kwa utulivu, huku wakitumia kwato zao kubwa kuchimbua kuvu na kuvumwani zilizo chini ya theluji. Mbali kidogo, tunamwona Msami akiwa ameketi kwa utulivu juu ya kigari chake huku akichunga mbawala wake. Mbwa wake anahakikisha kwamba wanyama hao hawatawanyiki. Kwa muda mfupi, mbwa huyo anasimama na kunusa kuelekea upande wetu. Hata hivyo, anarudi mara moja na kuendelea na kazi yake. Tunamhubiria mchungaji huyo. Ni mwenye urafiki na anatusikiliza.
Tukiwa njiani kurudi nyumbani, tunafikiria watu wote tuliokutana nao katika safari yetu ya kilomita 300. Tunaona ni pendeleo kushiriki kwa kadiri ndogo tu kuwahubiria watu katika eneo hili kubwa lililofunikwa kwa theluji.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
© Norway Post