Je, Wajua?
Je, Wajua?
Desturi ya kukusanya masalio ilikuwa nini na ni nani waliofaidika?
▪ Sheria ya Musa iliwakataza wakulima wasivune mazao yote katika mashamba yao. Hivyo, wale waliovuna nafaka hawakupaswa kuvuna kila kitu kwenye ukingo wa mashamba yao. Wale waliokusanya zabibu hawakupaswa kukusanya zilizotawanyika au kurudi kuvuna zile ambazo hazikuwa zimekomaa walipovuna mara ya kwanza. Na wale waliochuma zeituni walipaswa kuacha zile ambazo hazikuanguka chini. (Mambo ya Walawi 19:9, 10; Kumbukumbu la Torati 24:19-21) Kisha maskini, mayatima, wajane, na wakazi wageni wangekusanya au kuokota kilichokuwa kimebaki baada ya mavuno.
Sheria hii iliyohusu kukusanya masalio iliwanufaisha Waisraeli wote. Ilimtia moyo mwenye shamba kuwa mkarimu, kuepuka ubinafsi, na kutegemea baraka za Mungu. Pia iliwasaidia wale waliokusanya masalio wafanye kazi kwa bidii kwa sababu kukusanya masalio haikuwa kazi rahisi. (Ruthu 2:2-17) Kukusanya masalio kulisaidia watu maskini wasikose chakula au kuwa mzigo kwa jamii. Pia iliwasaidia wasijihisi kuwa wanadharauliwa kwa sababu ya kuomba-omba au kutegemea misaada.
Kwa nini Sulemani aliagiza mbao kutoka Lebanoni kwa ajili ya ujenzi wa hekalu huko Yerusalemu?
▪ Simulizi katika kitabu cha 1 Wafalme 5:1-10 linaeleza kuhusu mapatano yaliyofanywa kati ya Sulemani na Hiramu, mfalme wa Tiro. Kulingana na mapatano hayo, vyelezo vya mierezi na magogo ya mberoshi yangepaswa kupelekwa Israeli kutoka Lebanoni kupitia baharini ili kutumiwa katika ujenzi wa hekalu.
Mbao za mierezi zilikuwa bidhaa muhimu katika biashara iliyofanywa katika eneo la kale la Mashariki ya Kati. Nchini Misri na Mesopotamia, aina hii ya mbao ilitumiwa kwa ukawaida kutengeneza nguzo na pia mbao zilizotumika kufunikia kuta za mahekalu na nyumba za Wafalme. Hifadhi za nyaraka za kifalme, vitabu na maandishi ya kale yanathibitisha kuwa mbao za mierezi ziliendelea kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ya majiji yenye kujitawala yaliyokuwa kusini mwa Mesopotamia, nyakati nyingine zikiwa kama nyara au malipo ya kodi. Nchini Misri zilitumika katika ujenzi wa mashua za kifalme, majeneza, na vifaa vingine vilivyotumika katika mazishi.
Mbao za mierezi zilizotoka Lebanoni zilikuwa maarufu hasa kwa sababu zilidumu kwa muda mrefu, zilikuwa na harufu nzuri, zilipendeza, na hazikushambuliwa na wadudu. Hivyo, Sulemani alitumia bidhaa bora kabisa katika ujenzi wa hekalu. Leo, kuna misitu michache iliyotawanyika na iliyo midogo ikilinganishwa na misitu mikubwa ambayo zamani ilifunika milima ya Lebanoni.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Usafirishaji wa mierezi ya Lebanoni, mchongo kutoka katika nyumba ya Mfalme Sargoni wa Ashuru
[Hisani]
Erich Lessing/Art Resource, NY