Awamu ya 1 ya Picha za Ujenzi Nchini Filipino (Februari 2014 Hadi Mei 2015)
Mashahidi wa Yehova wanajenga majengo mapya na kurekebisha majengo ya zamani ya ofisi ya tawi ya nchini Filipino iliyopo Quezon City. Kwa kuwa sasa machapisho kwa ajili ya Filipino huchapishwa katika ofisi ya tawi ya Japani, jengo lililotumiwa zamani kwa kazi ya uchapishaji nchini Filipino limebadilishwa na kuwa ofisi za Idara za Utafsiri, Kompyuta, Usanifu-Majengo na Ujenzi, Udumishaji, na Usafirishaji. Picha hizi zinaonyesha ujenzi na ukarabati mbalimbali uliofanywa katika jengo hilo na majengo mengine kuanzia Februari 2014 hadi Mei 2015. Mradi huo umekusudiwa kukamilika Oktoba 2016.
Februari 28, 2014—Jengo la 7
Wafanyakazi wa muda wakiweka vitunza joto vipya kwenye mifuko ili visipate unyevu. Wamevaa mavazi maalumu yanayolinda ngozi yao.
Aprili 2, 2014—Jengo la 7
Wafanyakazi wakimalizia ujezi wa paa la studio ya kurekodi Lugha ya Ishara ya Filipino. Matundu ya mraba yaliyo katika paa hilo yatatumika kupachika mashine za mfumo wa hewa (HVAC), zitakazokuwa zikiingiza hewa katika studio hiyo.
Oktoba 21, 2014—Eneo la ujenzi la Quezon City
Kuchimba ili kutengeneza mfumo wa kupooza hewa unaotumia maji baridi. Mfumo huo mpya utatumika katika majengo yote ya ofisi ya tawi.
Desemba 19, 2014—Madaraja yanayounganisha Jengo la 1, la 5, na la 7
Madaraja hayo yataunganisha majengo yote makubwa kutia ndani, Jengo la 1, ambapo kuna chumba cha kulia. Njia hizo zitatumiwa hasa na watu zaidi ya 300 wanaofanya kazi katika Jengo la 7.
Januari 15, 2015—Jengo la 5
Kreni yenye uwezo wa kubeba tani 50 ikinyanyua mabati kwa ajili ya paa. Kreni mbalimbali zilikodiwa kutoka kwenye makampuni ya watu binafsi.
Januari 15, 2015—Jengo la 5A
Jengo lenye safu mbili na ukubwa wa mita za mraba 125 lina vyoo viwili, lifti, na ngazi. Kujenga vyoo na ngazi katika jengo hilo imewezekana kupata eneo kubwa zaidi katika Jengo la 5. Pia, kuweka lifti katika jengo hilo, badala ya kuiweka kwenye Jengo la 5, kutazuia rekodi za sauti zisiathiriwe na sauti ya lifti hiyo.
Januari 15, 2015—Jengo la 5A
Wajenzi wakiunganisha vyuma kabla ya kumimina zege wakiwa chini ya mwavuli unaozuia jua. Wastani wa kiwango cha joto wakati wa mchana huwa nyuzi 29 Selsiasi katika mwezi wa Januari na hufika nyuzi 34 Selsiasi katika mwezi wa Aprili.
Machi 5, 2015—Jengo la 5
Wajenzi wakitengeneza boriti za kuezekea mabati kwa kutumia mbao. Karibu vipande 800 hivi vya mbao vilitumika katika ujenzi wa Jengo la 5.
Machi 17, 2015—Jengo la 5
Kuchanganya zege kwa kutumia mikono kwa ajili ya ujenzi mdogo. Wajitoleaji wanaosaidia katika mradi huu wa ujenzi wanatia ndani wafanyakazi zaidi ya 100 kutoka nchi za Australia, Hispania, Japani, Kanada, Korea ya Kusini, Marekani, New Zealand, Ufaransa, na nchi nyingine.
Machi 25, 2015—Jengo la 5
Kuezeka mabati kwenye Jengo la 5, ambalo awali lilikuwa na Idara ya Utafsiri. Jengo hilo linakarabatiwa ili litumiwe na Idara ya Kurekodi Sauti na Idara ya Utumishi.
Mei 13, 2015—Jengo la 5
Fundi akikata kwa kutumia mashine ya umeme vyuma vitakavyotumika kutengenezea kuta za ofisi.