Wasomaji Wetu Wanauliza . . .
Desturi za Krismasi Zina Ubaya Gani?
Kwa muda mrefu Krismasi imejulikana kuwa sherehe ya Wakristo ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu. Kuna desturi nyingi zinazohusiana na sherehe hiyo. Hata hivyo, kuna utata kuhusu jinsi desturi hizo zinavyohusiana na kuzaliwa kwa Yesu.
Jambo moja linalozusha utata huo ni hadithi za hekaya kuhusu Baba Krismasi. Chanzo cha Baba Krismasi mwenye ndevu nyeupe, rangi ya waridi mashavuni na aliyevaa nguo nyekundu, kimetokana na tangazo la biashara la Krismasi lililobuniwa na kampuni ya vinywaji huko Amerika ya Kaskazini katika mwaka wa 1931. Katika miaka ya 1950, baadhi ya watu huko Brazili walijaribu kubadili cheo cha Baba Krismasi na kumpa mtu wa taifa lao waliyemwita—Babu wa India. Matokeo yalikuwaje? Baba Krismasi hakumshinda tu Babu wa India bali pia “alimshinda mtoto Yesu na kuwa mwakilishi mkuu wa sherehe hiyo ya Desemba 25,” anasema Profesa Carlos E. Fantinati. Lakini je, sherehe ya Krismasi haifai tu kwa sababu ya hekaya kuhusu Baba Krismasi? Ili kupata jibu, acheni tuchunguze kuhusu Ukristo wa mapema.
“Katika karne mbili za kwanza za tangu Ukristo ulipoanza, watu wengi hawakusherehekea sikukuu za kuzaliwa za wafia imani au hata Yesu mwenyewe,” kinasema Encyclopedia Britannica. Kwa nini? Wakristo waliona kusherehekea siku ya kuzaliwa kuwa ni zoea la kipagani linalopaswa kuepukwa. Kwa kweli, Biblia haitaji tarehe ya siku aliyozaliwa Yesu.
Licha ya msimamo wa Wakristo wa mapema wa kupinga mazoea ya kusherehekea siku ya kuzaliwa, Kanisa Katoliki lilianza kusherehekea Krismasi katika karne ya nne W.K. Kanisa hilo lilitaka kujiimarisha kwa kupunguza umaarufu wa dini za kipagani za Roma na sherehe za msimu wa baridi, jua linapokuwa upande wa Kaskazini wa dunia. Kila mwaka, kuanzia Desemba 17 mpaka Januari 1, “Waroma wengi walisherehekea pamoja, walicheza, walishiriki katika matamasha, gwaride, na sherehe nyingine walipokuwa wakiabudu miungu yao,” kinasema kitabu Christmas in America, kilichoandikwa na Penne L. Restad. Ilipofika Desemba 25, Waroma walisherehekea kuzaliwa kwa Jua Lisiloweza Kushindwa. Ili kuanzisha Krismasi siku hiyo, kanisa liliwashawishi Waroma wengi kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu badala ya kuzaliwa kwa jua. Waroma “bado waliweza kufurahia vitu vyote vilivyohusiana na sherehe hizo za msimu wa baridi,” kinasema kitabu Santa Claus, a Biography, kilichoandikwa na Gerry Bowler. Kwa hakika, “waliendelea kusherehekea sikukuu hiyo mpya kama tu walivyozoea kufanya zamani.”
Ni wazi kwamba sherehe za Krismasi hazifai kwa sababu ya chanzo chake kibaya. Katika kitabu chake The Battle for Christmas, Stephen Nissenbaum, anaitaja Krismasi kuwa “sherehe ya kipagani yenye sura ya Ukristo.” Kwa hiyo, Krismasi inamvunjia heshima Mungu na Mwana wake, Yesu Kristo. Je, hilo ni jambo dogo tu? Biblia inauliza hivi: “Kuna ushirika gani kati ya uadilifu na uasi-sheria? Au nuru ina ushirika gani na giza?” (2 Wakorintho 6:14) Krismasi ni kama tawi la mti lililopinda ambalo “haliwezi kunyooshwa.”—Mhubiri 1:15.