Je, Wajua?
Mafundi wa meli wa zamani walifanyaje ili vyombo vya baharini visiingie maji?
Lionel Casson, mtaalamu wa meli za zamani, anaelezea jinsi watengeneza meli nyakati za Waroma walivyofanya ili kuzuia maji yasiingie ndani ya meli. Kwa kawaida “walipaka lami kwenye nafasi kati ya mbao au hata upande wote wa nje, na pia upande wa ndani wa mashua au meli.” Miaka mingi kabla ya Waroma, Wakaldayo na Wababiloni walipaka lami kwenye mashua na meli zao ili kuzuia maji.
Maandiko ya Kiebrania yanataja mbinu hiyohiyo kwenye andiko la Mwanzo 6:14. Neno la Kiebrania linalotafsiriwa “lami” linamaanisha mojawapo ya bidhaa iliyopatikana kutokana na petroli.
Lami asilia hupatikana katika hali mbili
Lami ilipatikana kwa wingi nyakati za Biblia. Nchi Tambarare ya Sidimu, iliyokuwa kwenye Bahari ya Chumvi, “ilikuwa imejaa mashimo ya lami.”
Ni njia gani zilizotumiwa kuhifadhi samaki zamani?
Kwa muda mrefu, samaki wamekuwa chakula muhimu. Kabla ya kuanza kusafiri na Yesu, baadhi ya mitume wake walikuwa wavuvi kwenye Bahari ya Galilaya. (Mathayo 4:18-22) Angalau baadhi ya samaki waliovua humo walitayarishwa kwenye “viwanda” vilivyokuwa karibu.
Mbinu ya kuhifadhi samaki ambayo huenda ilitumiwa zamani huko Galilaya bado inatumiwa katika maeneo fulani. Kwanza, samaki hutolewa matumbo na kuoshwa kwa maji. Kitabu Studies in Ancient Technology kinaelezea hatua zinazofuata: “Chumvi hupakwa kwenye mapezi, mdomo na magamba. Samaki waliotiwa chumvi kwa wingi hufunikwa kwa jamvi. Baada ya kuachwa kwa siku 3-5 rundo hilo hugeuzwa na kukaa tena kwa kipindi kama hicho. Wanapokaushwa kwa njia hiyo, umajimaji wa mwili hukauka na chumvi huingia ndani ya samaki. Baada ya kukauka, wanakuwa wagumu.”
Haijulikani samaki wangehifadhiwa kwa muda gani kupitia njia hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa Wamisri wa kale waliuza samaki waliokaushwa huko Siria, hilo linaonyesha kwamba njia hizo zilifaulu.