Je, Wajua?
Maisha ya watumwa yalikuwaje katika Milki ya Roma?
Katika Milki ya Roma watu wengi walifanywa kuwa watumwa baada ya kushindwa vitani au kutekwa nyara. Mateka waliuzwa na kwa kawaida hawakurudi nyumbani kwao tena.
Watumwa wengi walikufa walipokuwa wakifanya kazi migodini, lakini maisha hayakuwa magumu sana kwa wale waliofanya kazi mashambani au nyumbani. Mtumwa angelazimishwa kuvaa chuma shingoni kilichokuwa na maandishi yaliyoonyesha zawadi ambayo mtu angepata kwa kumrudisha mtumwa huyo kama angetoroka. Wale waliojaribu kutoroka mara nyingi waliandikwa herufi F usoni kumaanisha fugitivus (mateka).
Kitabu cha Biblia cha Filemoni kinataja jinsi mtume Paulo alivyomrudisha mtumwa Onesimo aliyekuwa ametoroka kutoka kwa bwana wake, Filemoni. Ingawa Filemoni alikuwa na haki ya kisheria ya kumwadhibu Onesimo, Paulo alimwagiza Filemoni “[ampokee] kwa fadhili,” kwa msingi wa upendo na urafiki kati yake na Paulo.—Filemoni 10, 11, 15-18.
Kwa nini eneo la kale la Foinike lilijulikana kwa kutokeza rangi ya zambarau?
Eneo la Foinike ambalo inawezekana lilikuwa mahali ilipo Lebanon ya kisasa, lilijulikana kwa kutokeza zambarau ya Tiro, rangi iliyopata jina kutokana na jiji la Tiro. Mfalme Sulemani wa Israeli la kale alirembesha hekalu lake kwa “sufu iliyotiwa rangi ya zambarau” iliyotengenezwa na fundi kutoka Tiro.—2 Mambo ya Nyakati 2:13, 14.
Zambarau ya Tiro ilikuwa rangi yenye thamani zaidi wakati huo, hasa kwa sababu ya kazi iliyohusika kuitengeneza. Kwanza, wavuvi walikusanya baharini konokono wanaoitwa murex. * Konokono zaidi ya 12,000 walihitajiwa ili kutokeza rangi ya kutosha kutia kitambaa kimoja. Halafu konokono hao walitolewa kwenye magamba yao ili tezi zao zenye rangi zitolewe. Watengenezaji rangi walichanganya tezi hizo na chumvi na kuzianika juani kwa siku tatu. Kisha wakaweka mchanganyiko huo kwenye matangi yaliyofunikwa na kuuchemsha wakitumia maji ya bahari kwa siku kadhaa.
Kwa karne nyingi, kupitia biashara na mamlaka yao, Wafoinike waliendelea kutengeneza na kuuza zambarau ya Tiro. Mabaki ya kazi yao ya kutengeneza rangi yamepatikana karibu na Bahari ya Mediterania na hata maeneo ya mbali huko Cádiz,Hispania.
^ fu. 8 Magamba yao yana urefu wa kati ya sentimita 5 hadi 8.