Mahakama Ya Ulaya Yatetea Haki Ya Kutojiunga Na Jeshi Kwa Sababu Ya Dhamiri
MASHAHIDI WA YEHOVA ulimwenguni pote wanajulikana kwa msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote inapohusu siasa na vita katika nchi yoyote. Wanaamini kabisa kwamba lazima ‘wafue panga zao ziwe majembe’ na ‘wasijifunze vita tena.’ (Isaya 2:4) Hawamzuii mtu yeyote kujiunga na utumishi wa kijeshi. Lakini namna gani ikiwa dhamiri ya Shahidi haimruhusu kutumikia jeshini, ingawa nchi anayoishi inamlazimisha? Hiyo ndiyo hali ambayo kijana Vahan Bayatyan alikabiliana nayo.
Matukio Yaliyotangulia Kesi Kwenye Mahakama ya Ulaya
Vahan alizaliwa mnamo Aprili 1983 nchini Armenia. Mwaka wa 1996, yeye na watu wengine wa familia yake walianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, na akabatizwa akiwa na umri wa miaka 16. Kupitia mambo aliyojifunza katika Biblia Vahan alisitawisha heshima kubwa kuelekea mafundisho ya Yesu Kristo, kutia ndani mwongozo ambao Yesu aliwapa wafuasi wake kwamba wasichukue silaha na kupigana. (Mathayo 26:52) Kwa hiyo, muda mfupi baada ya kubatizwa Vahan alikabili uamuzi mzito katika maisha yake.
Nchini Armenia, sheria inawalazimu vijana wenye umri wa miaka 18 wajiunge na utumishi wa kijeshi. Kijana anayekataa kufanya utumishi huo, anaweza kuhukumiwa kufungwa jela kwa miaka mitatu. Vahan alitaka kuwatumikia wananchi wenzake. Vilevile, hakutaka kutenda kinyume na dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia. Hivyo, alifanya nini?
Mara tu alipofikisha umri wa kujiunga na utumishi wa kijeshi katika mwaka wa 2001, Vahan alianza kuwaandikia barua wenye mamlaka nchini Armenia. Katika barua zake, alisema utumishi huo ungemfanya atende kinyume na dhamiri yake na mambo aliyoamini. Wakati huohuo, aliwaambia kwamba alikuwa tayari kufanya kazi ya badala katika utumishi wa kiraia.
Zaidi ya mwaka mmoja ulipita, na bado Vahan aliendelea kuwaomba wenye mamlaka watambue msimamo wake wa kukataa kujiunga
na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Hata hivyo, Septemba 2002, Vahan alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kukataa kutii amri ya kujiunga na utumishi wa kijeshi. Alihukumiwa kifungo cha miezi 18. Hata hivyo, kiongozi wa mashtaka hakuridhika na adhabu hiyo. Mwezi mmoja tu baada ya hukumu hiyo kutolewa, kiongozi wa mashtaka aliwasilisha kesi hiyo katika mahakama ya rufaa, akitaka adhabu kali zaidi itolewe. Alidai kwamba msimamo wa Vahan wa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri “haukuwa na msingi wowote na ulikuwa hatari.” Mahakama ya rufaa ilikubali ombi hilo la kiongozi wa mashtaka na wakaongeza kifungo cha Vahan hadi miezi 30.Vahan alikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Armenia. Januari 2003, Mahakama hiyo iliunga mkono uamuzi wa mahakama ya rufaa. Mara moja, Vahan alipelekwa gerezani ili aanze kutumikia kifungo chake pamoja na wauaji, walanguzi wa madawa ya kulevya, na wabakaji.
Matukio Katika Mahakama ya Ulaya
Tangu mwaka wa 2001, Armenia imekuwa mwanachama wa Baraza la Ulaya. Kwa hiyo, raia wa Armenia wana haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ikiwa wamejaribu njia zote katika nchi yao bila kufanikiwa. Vahan alichagua kufanya hivyo. Katika rufaa yake, alisema hukumu aliyopewa kwa sababu ya kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi ilipingana na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu. Aliomba haki yake ya kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri ilindwe chini ya kifungu hicho—jambo ambalo hapo awali halikuwahi kufanikiwa.
Mnamo Oktoba 27, 2009, mahakama ya ECHR ilitoa uamuzi wake. Mahakama hiyo iliamua kwamba kwa kuunga mkono uamuzi ule wa awali, uhuru wa dhamiri kama inavyofafanuliwa na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya haulindi haki za kidhamiri za watu wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi.
Kufikia wakati huo, tayari Vahan alikuwa amemaliza kifungo chake, alikuwa na mke, na mvulana mdogo. Vahan alivunjwa moyo na hukumu hiyo. Kisha, alihitaji kufanya uamuzi wa kuachana na kesi hiyo au akate rufaa katika Baraza Kuu la ECHR. Aliamua kukata rufaa. Baraza Kuu hukubali kushughulikia kesi zisizo za kawaida, hivyo Vahan alifurahi baraza hilo lilipokubali kushughulikia kesi yake.
Mwishowe, mnamo Julai 7, 2011, huko Strasbourg, nchini Ufaransa, Baraza Kuu la ECHR lilitoa uamuzi wake. Mahakama hiyo ilifikia mkataa kwa ushindi mkubwa wakati kura 16 kati ya 17 zilipounga mkono kuwa nchi ya Armenia ilikiuka uhuru wa dhamiri wa Vahan
Bayatyan kwa kumfunga gerezani kwa sababu ya kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi chini ya msingi wa dhamiri. Hakimu aliyetoka Armenia ndiye tu aliyepinga uamuzi huo.Kwa nini uamuzi huo ulikuwa muhimu? Kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya ECHR kwa haki ya kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri kuonwa kuwa inalindwa kikamili chini ya Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya. Hivyo, mahakama hiyo inaona kuwa ni ukiukaji wa haki za kimsingi katika jamii ya kidemokrasia kumfunga mtu anayekataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.
Mahakama hiyo ilitoa maelezo yafuatayo kuhusu msimamo wa Mashahidi wa Yehova wa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri: “Kwa hiyo, Mahakama haina sababu ya kutilia shaka kwamba uamuzi wa mlalamikaji wa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi ulichochewa na imani yake ya kidini, ambayo anashikilia kwa unyoofu na ambayo inapingana kabisa na takwa la kujiunga na utumishi wa kijeshi.”
Jinsi Uamuzi Huo Ulivyopokewa
Kwa zaidi ya miaka 20, Mashahidi wa Yehova zaidi ya 450 ambao wamekataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya imani wamehukumiwa nchini Armenia. Makala hii ilipokuwa ikitayarishwa, kulikuwa na vijana 58 katika nchi hiyo ambao walikuwa gerezani kwa kuwa walikataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri yao ya kidini. Watano kati yao walihukumiwa baada ya ule uamuzi mkubwa wa kesi kati ya Bayatyan na serikali ya Armenia. * Katika mojawapo ya kesi hizo, kijana mmoja aliyekataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, alipowasilisha ombi la kuomba kiongozi wa mashtaka aondoe kesi yake, kiongozi huyo alikataa. Kiongozi huyo wa mashtaka alimjibu kwa barua iliyosema: “Uamuzi wa Mahakama ya Ulaya katika kesi kati ya Bayatyan na serikali ya Armenia, uliotolewa Julai 7, 2011, hautumiki katika kesi hii, kwa kuwa ni wazi kwamba hali zinazohusika katika kesi hizo mbili zinatofautiana kabisa.”
Kwa nini kiongozi wa mashtaka alihisi hivyo? Kwa sababu Vahan Bayatyan aliposhtakiwa hakukuwa na mpango wa badala wa utumishi wa kiraia. Serikali ya Armenia inadai kwamba tangu wakati huo kuna sheria ambayo inaruhusu mpango kama huo, kwa hiyo wale wasiotaka kujiunga na utumishi wa kijeshi wanaweza kujiunga na utumishi wa kiraia. Hata hivyo, utumishi huo uko chini ya usimamizi wa kijeshi na hivyo wengi wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri hawawezi kuukubali.
Vahan Bayatyan anafurahi kwa sababu ya uamuzi mkubwa uliofanywa ili kumwondolea hatia. Sasa kwa sababu ya uamuzi huo, serikali ya Armenia inalazimika kuacha kuwashtaki na kuwafunga watu ambao imani ya kidini waliyoshikilia sana haiwaruhusu kushiriki katika utumishi wa kijeshi.
Mashahidi wa Yehova hawakusudii kuleta mabadiliko katika mfumo wa kisheria wa nchi yoyote. Hata hivyo, kama tu kijana Vahan Bayatyan alivyofanya, wanajaribu kutetea haki zao za kisheria kwa kutumia sheria zinazofuatwa katika nchi wanazoishi. Kwa nini? Ili waendelee kuishi kwa amani na kutii kwa uhuru maagizo ya kiongozi wao Yesu Kristo.
^ fu. 17 Wawili kati yao walihukumiwa Julai 7, 2011, siku ileile ambayo uamuzi wa ECHR ulitolewa.