Je, Wajua?
Je, Wajua?
Madhabahu ya “Mungu Asiyejulikana” ambayo mtume Paulo aliona huko Athene ilikuwa nini?—Matendo 17:23.
▪ Waandishi kadhaa wa Ugiriki ya kale walitaja madhabahu kama hizo. Kwa mfano, mwanahistoria na mwanajiografia Pausanias wa karne ya pili W.K., alisema kwamba huko Olimpia, kulikuwa na “madhabahu ya miungu Isiyojulikana.” Naye Philostratus, mwanafalsafa na msemaji mwenye ufasaha, alisema kwamba huko Athene “kulikuwa na madhabahu za kutukuza miungu isiyojulikana.”
Diogenes Laertius, mwandikaji wa karne ya tatu W.K., anasimulia kuhusu mapokeo fulani yanayofafanua chanzo cha “madhabahu zisizo na jina.” Hadithi hiyo ya karne ya sita au saba K.W.K., inataja jinsi mtu fulani anayeitwa Epimenides alivyotakasa jiji la Athene kutokana na ugonjwa fulani. Diogenes anaandika: “[Epimenides] alichukua kondoo . . . na kuwapeleka Areopago; na hapo akawaachilia waende popote walipotaka na kuwaagiza wale waliowafuata kondoo hao watie alama mahali ambapo kila kondoo alilala chini, kisha watoe dhabihu kwa mungu wa eneo hilo. Inasemekana kwamba kwa kufanya hivyo, ugonjwa huo ulikomeshwa. Hivyo, hata leo madhabahu zisizo na jina zinaweza kupatikana katika maeneo tofauti-tofauti ya Attica.”
Labda sababu nyingine iliyochochea watu wajenge madhabahu kwa miungu isiyojulikana, inasema kamusi The Anchor Bible Dictionary, ni kwamba “waliogopa kuivunjia heshima miungu fulani isiyojulikana na hivyo kukosa msaada wa miungu hiyo au kuifanya ikasirike.”
Kwa nini Wayahudi wa karne ya kwanza waliwadharau wakusanya-kodi?
▪ Wakusanya-kodi hawapendwi na watu. Hata hivyo, katika karne ya kwanza wakusanya-kodi walionekana kuwa kati ya watu wafisadi na wenye kudharauliwa zaidi nchini Israeli.
Watawala Waroma walitoza watu kodi ya juu sana. Maofisa Waroma walikusanya kodi ya ardhi kutoka kwa watu binafsi, lakini kazi ya kukusanya kodi ya bidhaa zilizouzwa nje ya nchi na zile zilizoingia nchini, kutia ndani bidhaa zilizosafirishwa kupitia nchini, ilipewa mtu ambaye alikuwa tayari kuwapa Waroma pesa nyingi zaidi. Kwa hiyo, wafanyabiashara wenyeji walinunua haki ya kukusanya kodi katika maeneo fulani. Kwa vile watu hao walikuwa tayari kutumiwa na Waroma waliochukiwa, Wayahudi wenzao waliwachukia sana, na waliwaona kuwa “wasaliti na waasi imani, waliochafuliwa kwa kuchangamana mara nyingi na wapagani,” kinasema kitabu Cyclopædia cha M’Clintock na Strong.
Wakusanya-kodi hawakuwa wanyoofu hata kidogo, na walijitajirisha kwa pesa walizokusanya kutoka kwa Wayahudi wenzao. Baadhi ya wakusanya-kodi walikadiria kupita kiasi thamani ya bidhaa zilizotozwa kodi na kisha kuiba pesa za ziada walizopata, huku wengine wakitumia mashtaka ya uwongo ili kuwanyang’anya maskini pesa. (Luka 3:13; 19:8) Kwa hiyo, Wayahudi waliwaona wakusanya-kodi kuwa sawa na watenda dhambi na, kitabu The Jewish Encyclopedia kinasema kwamba “hawakustahili kuwa mahakimu au hata mashahidi.”—Mathayo 9:10, 11.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Madhabahu ya mungu asiyejulikana, mabomoko ya Pergamamu, Uturuki
[Picha katika ukurasa wa 18]
Mchongo wa Waroma unaoonyesha mkusanya-kodi, karne ya pili au ya tatu W.K.
[Hisani]
Erich Lessing/Art Resource, NY