Unabii wa 3. Magonjwa
Unabii wa 3. Magonjwa
“Kutakuwa . . . na magonjwa ya kuambukiza.”—LUKA 21:11, Habari Njema kwa Watu Wote.
● Bonzali, ofisa wa afya katika nchi moja ya Afrika ambayo imekumbwa na vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe, anajitahidi anavyoweza kuwatibu wafanyakazi kwenye mgodi fulani katika mji wa kwao ambao wanakufa kwa ugonjwa wa Marburg. * Maombi yake ya kupata msaada kutoka kwa maofisa walioko jijini yanakosa kujibiwa. Miezi minne baadaye, msaada unafika, lakini Bonzali tayari amekufa. Aliambukizwa ugonjwa wa Marburg na wale wafanyakazi wa migodi aliokuwa anajaribu kuwaokoa.
MAMBO ya HAKIKA YANAONYESHA NINI? Magonjwa yanayoathiri mapafu (kama vile nimonia), magonjwa ya kuharisha, UKIMWI, kifua kikuu, na malaria ni kati ya magonjwa mabaya zaidi yanayomwathiri mwanadamu. Katika mwaka wa 2004 pekee, magonjwa hayo matano yalisababisha vifo vya watu wapatao milioni 10.7. Hilo linamaanisha kwamba magonjwa hayo yalisababisha kifo cha mtu mmoja baada ya kila sekunde tatu, katika mwaka wote mzima.
NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Idadi ya watu duniani inaendelea kuongezeka, hivyo lazima kuwe na visa vingi zaidi vya magonjwa. Kuna watu wengi zaidi wanaoweza kuambukizwa.
JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Idadi ya watu duniani imeongezeka sana. Vivyo hivyo, uwezo wa mwanadamu wa kupima, kudhibiti, na kutibu magonjwa umeongezeka. Hivyo basi, magonjwa na madhara yake kwa mwanadamu yanapaswa kuwa yamepungua. Lakini, mambo ni kinyume cha hayo.
UNA MAONI GANI? Je, watu wanapatwa na magonjwa mabaya kama Biblia ilivyotabiri?
Matetemeko ya nchi, njaa, na magonjwa yanaathiri mamilioni ya watu. Lakini, mamilioni ya wengine huteswa na wanadamu wenzao—wengi wakitendewa vibaya na wale ambao wanapaswa kuwalinda. Ona yale ambayo unabii wa Biblia unasema yangetokea.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Homa ya Kuvuja Damu ya Marburg inasababishwa na kirusi kinachohusianishwa na Ebola.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Ni jambo baya sana kuliwa na simba au mnyama mwingine, lakini ni jambo baya vilevile kuliwa kutoka ndani na ugonjwa fulani na kuona wengine pia wakiathiriwa.”—MTAALAMU WA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA, MICHAEL OSTERHOLM.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 6]
© William Daniels/Panos Pictures