Jina la Mungu, Yehova, KATIKA Hekalu la Misri
Jina la Mungu, Yehova, KATIKA Hekalu la Misri
ISIPOKUWA Biblia, ni maandishi gani mengine ya kale zaidi ambayo yana jina la Mungu, Yehova, au Yahweh? Wasomi fulani wanajibu kwa uhakika hivi: Ni maandishi ya karne ya 14 K.W.K. Kwa nini wanasema hivyo?
Kufikia mwaka wa 1370 K.W.K., Wamisri walikuwa wameshinda mataifa mengi. Mtawala wa Misri wa wakati huo, Farao Amenhotep (Amenophis) wa Tatu, alikuwa amejenga hekalu la kifahari huko Soleb, katika nchi ya Nubia, ambayo sasa inaitwa Sudan. Wataalamu wa vitu vya kale walipopata hekalu hilo, waliona maandishi ya michoro ya Wamisri ambayo yanaonyesha Tetragramatoni ya Kiebrania—YHWH, au Yehova. Maandishi hayo yaliandikwa miaka 500 kabla ya maandishi yanayojulikana sana ya Jiwe la Moabu, ambayo hapo mbeleni yalionwa kuwa maandishi ya kale zaidi yaliyo na jina la Mungu. Kwa nini jina la Mungu wa Biblia limeandikwa katika hekalu la Wamisri?
“Shasu Nchi ya Jahu”
Farao Amenhotep wa Tatu alikuwa ameweka wakfu hekalu alilokuwa amejenga kwa mungu Amun-Ra. Hekalu hilo lilikuwa na urefu wa mita 120 hivi na lilikuwa kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Nile. Maandishi ya michoro ambayo yalikuwa yamerembesha sehemu za chini za nguzo katika ukumbi mmoja wa hekalu hilo yanaorodhesha majina ya maeneo ambayo Amenhotep alidai kwamba alikuwa ameteka. Kila eneo linawakilishwa na mfungwa, ambaye mikono yake imefungiwa mgongoni akiwa na ngao ambayo imeandikwa jina la nchi yake au watu wa nchi yake. Kati ya majina yaliyo kwenye maandishi hayo ya michoro, ni jina la nchi za watu wanaoitwa Washasu, au Washosou. Watu wa Shasu walikuwa nani?
Shasu lilikuwa jina la ujumla ambalo Wamisri waliwapa Wabedui, makabila yaliyodharauliwa ya watu walioishi upande wa mashariki wa mpaka wa Misri. Nchi za Washasu zilitia ndani maeneo ya kusini mwa Palestina, kusini mwa Mto Yordani, na Sinai.
Wachunguzi fulani wanasema kwamba nchi zinazosemekana kuwa za Washasu zilienea upande wa kaskazini kufikia Lebanoni na Siria. Orodha iliyokuwa huko Soleb ya nchi zilizokuwa zimetekwa ilionyesha nchi ambayo wengine wamesema ilikuwa ikiitwa “Yahwe katika nchi ya Shosou,” “Shasu nchi ya Jahu,” au “Nchi ya Shasu-yhw.” Mchunguzi wa vitu vya kale vya Misri Jean Leclant anasema kwamba jina lililoandikwa kwenye ngao huko Soleb “linafanana na ‘tetragramu’ ya mungu wa Biblia, YHWH.”Wasomi wengi wanaamini kwamba lazima jina Jahu, Yahu, au Yahwe katika maandishi haya na katika maandishi mengine kama hayo liwe linamaanisha mahali au wilaya. Msomi Shmuel Ahituv anasema kwamba maandishi hayo yanaonyesha “eneo kubwa la jamii ya waabudu wa Yāhū, Mungu wa Israeli.” * Ikiwa maoni yake ni sahihi, jina la eneo hilo ni moja kati ya mifano mingi ya maneno ya kale ya Kiyahudi yanayotambulisha eneo na mungu wa eneo hilo. Mfano mwingine ni neno Assur, ambalo linatambulisha nchi ya Ashuru na mungu wake mkuu.
Kuhusu maandishi yaliyo katika hekalu huko Nubia, msomi wa Biblia na mtaalamu wa vitu vya kale Roland de Vaux anasema: “Katika eneo ambalo mababu wa Israeli walikuwa wameshirikiana nalo sana, kufikia katikati ya karne ya pili Kabla ya Kristo, kulikuwa na jina la eneo au jina la mtu ambalo lilifanana sana, au lilikuwa sawa kabisa na jina la Mungu wa Israeli.”
Jina Ambalo Bado Linaheshimiwa
Soleb si mahali pekee huko Nubia ambapo jina Yahwe linapatikana katika maandishi ya michoro ya Misri. Maandishi yanayofanana na orodha iliyo huko Soleb yanapatikana pia katika mahekalu ya Ramsesi wa Pili huko Amarah Magharibi na huko Aksha. Katika orodha iliyo huko Amarah, maandishi ya michoro yanayosema “Yahwe katika nchi ya Shosou” yanakaribia kufanana na yale ya maeneo mengine ya Shosou, yanayodhaniwa kuwa Seiri na Labani. Biblia inahusianisha maeneo hayo na sehemu za kusini mwa Palestina, Edomu, na Sinai. (Mwanzo 36:8; Kumbukumbu la Torati 1:1) Ni maeneo ambayo yalitembelewa sana na watu waliomjua na kumwabudu Yehova kabla na baada ya Waisraeli kwenda Misri.—Mwanzo 36:17, 18; Hesabu 13:26.
Tofauti na majina ya miungu mingine ambayo yanapatikana katika maandishi ya kale, jina la Mungu wa Biblia, Yehova, bado linatumiwa sana na kuheshimiwa. Kwa mfano, katika nchi zaidi ya 230, Mashahidi wa Yehova zaidi ya milioni saba wanatumia maisha yao kuwafundisha wengine jina hilo na pia kuwasaidia wamkaribie Mungu mwenye jina hilo la pekee.—Zaburi 83:18; Yakobo 4:8.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 7 Wasomi fulani wana mashaka kwamba maandishi hayo ya michoro yanamaanisha kwamba Washasu “walikuwa wafuasi wa mungu Yahweh.” Wanaamini kwamba huenda jina lisilojulikana la eneo hilo linafanana tu na jina la Mungu wa Israeli kwa njia fulani isiyo wazi.
[Blabu katika ukurasa wa 21]
Kwa nini Yehova, jina la Mungu wa Biblia, limeandikwa katika hekalu la kipagani la Wamisri?
[Ramani katika ukurasa wa 21]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MISRI
Hekalu huko Soleb
SUDAN
Mto Nile
[Picha katika ukurasa wa 21]
Mfano wa nguzo ya Hekalu
[Picha katika ukurasa wa 22]
Eneo la magofu ya hekalu la Amun-Ra, huko Soleb, Sudan
[Hisani]
Ed Scott/Pixtal/age fotostock
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]
Background: Asian and Middle Eastern Division/The New York Public Library/Astor, Lenox and Tilden Foundations