Vita Vimebadilika Siku Hizi
Vita Vimebadilika Siku Hizi
SIKUZOTE vita vimekuwa vikatili. Vimeharibu maisha ya askari wengi na vimefanya raia wengi wateseke. Lakini katika miaka ya hivi karibuni vita vimebadilika. Jinsi gani?
Leo, vita vingi ni vya wenyewe kwa wenyewe, yaani, vita kati ya vikundi vya raia wenye kupingana katika nchi ileile. Mara nyingi vita hivyo huendelea kwa muda mrefu, huathiri watu kihisia, na kuharibu nchi vibaya kuliko vita kati ya mataifa. Mwanahistoria Mhispania Julián Casanova anasema, “Vita vya wenyewe kwa wenyewe ni mapigano ya kikatili yenye umwagikaji wa damu ambayo husababisha vifo vya watu wengi, kulalwa kinguvu, watu kulazimika kuhama makwao, na katika visa vilivyo vibaya zaidi, jamii nzima-nzima huangamizwa.” Naam, majirani wanapofanyiana vitendo vya ukatili, madhara yanayotokea yanaweza kudumu muda mrefu.
Tangu Vita Baridi viishe, kumekuwa na vita vichache sana kati ya mataifa. “Vita vyote vikubwa vilivyopiganwa kati ya mwaka wa 1990 hadi 2000, isipokuwa vitatu tu, vilikuwa vya wenyewe kwa wenyewe,” yaripoti taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI).
Ni kweli kwamba huenda vita vya wenyewe kwa wenyewe visionekane kuwa vyenye kutisha sana na huenda vikapuuzwa sana na vyombo vya habari vya kimataifa. Hata hivyo, vita hivyo husababisha mateso na uharibifu. Watu wengi sana wamekufa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Katika miaka 20 iliyopita watu milioni tano hivi walikufa katika nchi tatu tu zilizokumbwa na vita—Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Sudan. Katika nchi za Balkan, vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe viliua watu 250,000 hivi, navyo vita vya kuvizia vinavyoendelea huko Kolombia vimeua watu 100,000.
Watoto ndio huathiriwa zaidi na ukatili wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi ilisema kwamba katika miaka 10 iliyopita, zaidi ya watoto milioni mbili walikufa katika vita hivyo. Wengine milioni sita walijeruhiwa. Idadi inayoongezeka ya watoto wanazoezwa kuwa askari. Mtoto mmoja ambaye ni askari anasema: “Walinizoeza. Wakanipa bunduki. Nikatumia dawa za kulevya na kuua raia wengi. Vilikuwa vita tu . . . Nilitii tu amri. Nilijua ni vibaya kuua. Si kupenda kwangu.”
Watoto wengi katika nchi ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa jambo la kawaida, wanakulia katika mazingira yasiyo na amani. Wanaishi katika mazingira ambako shule zimeharibiwa na ambako watu huzungumza kupitia mtutu wa bunduki. Dunja mwenye umri wa miaka 14 anasema: “Watu wengi sana wameuawa . . . Huwezi kuwasikia ndege wakiimba, unasikia tu sauti za watoto wakilia kwa kupoteza mama au baba, ndugu au dada.”
Ni Nini Husababisha Vita?
Ni nini huchochea vita hivyo vikatili vya wenyewe kwa wenyewe? Vita hivyo huchochewa hasa na chuki ya kikabila na kijamii, tofauti za kidini, ukosefu wa haki, na misukosuko ya kisiasa. Kisababishi kingine ni pupa ya kupata mamlaka na pesa. Viongozi wa kisiasa, ambao mara nyingi huchochewa na pupa, huchochea chuki ambayo hufanya vita viendelee au viwe vibaya zaidi. Ripoti ya SIPRI inasema kwamba wengi wanaopigana “huchochewa na faida za kibinafsi.” Ripoti hiyo inaongeza kusema: “Pupa huonyeshwa katika njia mbalimbali, kama vile biashara kubwa ya almasi inayofanywa na viongozi wa kijeshi na wa kisiasa na pia uporaji unaofanywa vijijini na vijana wenye bunduki.”
Kupatikana kwa urahisi kwa silaha hatari za bei ya chini huchangia kuenea kwa mauaji. Kila mwaka vifo vya watu wapatao 500,000, hasa wanawake na watoto, husababishwa na zile zinazoitwa silaha ndogo-ndogo. Katika nchi moja ya Afrika, bunduki aina ya AK-47 ina bei sawa na ya kuku. Inasikitisha kwamba katika sehemu fulani hesabu ya silaha ni karibu sawa na ya kuku. Sasa kuna silaha ndogo-ndogo na nyepesi zipatazo milioni 500 duniani—bunduki 1 kwa watu 12.
Je, vita vikatili vya wenyewe kwa wenyewe vitaitia alama karne ya 21? Je vita hivyo vinaweza kuzuiwa? Je, mwishowe watu wataacha kuua? Makala inayofuata itajibu maswali hayo.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Matokeo Yenye Kuhuzunisha ya Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe
Katika vita vikatili ambavyo havipiganwi kwa silaha za hali ya juu, asilimia 90 ya wanaoathiriwa ni raia wala si wapiganaji. “Ni wazi kwamba katika visa vingi, watoto, tofauti na watu wengine, huwa shabaha ya wapiganaji,” anasema Graça Machel, Mtaalamu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Madhara ya Vita juu ya Watoto.
Wanajeshi wamekuwa wakitumia mbinu ya kuwalala wanawake kinguvu. Katika maeneo fulani yaliyokumbwa na vita, waasi hulala kinguvu kila msichana wanayempata katika vijiji wanavyovamia. Kusudi lao ni kueneza hofu au kuharibu uhusiano wa familia.
Baada ya vita kunakuwa na njaa na magonjwa. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vinapotokea, mazao machache hupandwa na kuvunwa, hospitali chache sana huhudumia watu, msaada wa kimataifa huwafikia watu wachache sana wenye uhitaji. Uchunguzi mmoja kuhusu vita fulani vya wenyewe kwa wenyewe barani Afrika ulionyesha kwamba asilimia 20 ya walioathiriwa walikufa kwa sababu ya magonjwa na asilimia 78 kwa sababu ya njaa. Ni asilimia 2 tu waliouawa katika vita hivyo.
Kwa wastani, kila dakika 22 mtu fulani hupoteza kiungo au hufa kwa kukanyaga mabomu yaliyotegwa ardhini. Inakadiriwa kwamba kuna mabomu ya ardhini kati ya milioni 60 hadi 70 katika nchi zaidi ya 60.
Watu hulazimika kukimbia makwao. Leo duniani kuna wakimbizi milioni 50 wanaotia ndani watu waliolazimika kukimbia makao yao, na nusu ya idadi hiyo ni watoto.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
COVER: Boy: Photo by Chris Hondros/Getty Images
[Picha katika ukurasa wa 3]
Photo by Chris Hondros/Getty Images