HABARI KUU | KUDUMISHA AMANI NYUMBANI
Jinsi ya Kukomesha Mizozo Nyumbani
UFANYE nini ikiwa inaonekana kwamba mizozo katika familia yako haiishi? Huenda mizozo hiyo imekuwa mibaya zaidi na inatukia mara nyingi zaidi. Labda hata hujui chanzo cha ugomvi huo. Lakini bado mnapendana na hamtaki kuumizana.
Ni muhimu kukumbuka kwamba kwa kuwa tu mna maoni yanayotofautiana, haimaanishi kwamba familia yenu inasambaratika. Kinachoamua ikiwa nyumba yenu itakuwa na amani au la, si ugomvi wenyewe bali ni jinsi mnavyoushughulikia. Fikiria hatua zifuatazo zinazoweza kuwasaidia kukomesha mizozo.
1. ACHA KULIPIZA KISASI.
Ili kuwe na mabishano, lazima kuwe na watu wawili wanaozungumza. Lakini mmoja anaponyamaza na kusikiliza badala ya kuzungumza, mabishano huisha. Kwa hiyo, epuka kumjibu mwenzako unapokasirishwa. Dumisha heshima yako kwa kujizuia. Kumbuka, kuwa na amani katika familia ni muhimu zaidi kuliko kushinda mabishano.
“Pasipo na kuni moto huzimika, na pasipo na mchongezi ugomvi hutulia.”
—Methali 26:20.
2. ELEWA HISIA ZA WENGINE KATIKA FAMILIA.
Kumsikiliza mwenzako kwanza kwa makini ukiwa na hisia-mwenzi bila kumkatiza au kumhukumu kunaweza kutuliza hasira na kudumisha amani. Badala ya kumshuku mwenzako, tambua hisia zake. Usifikiri ana nia mbaya wakati amekosea tu kwa sababu ya kutokamilika. Huenda akasema maneno yenye kuudhi bila kufikiri au kwa sababu ameumizwa hisia na si kwa sababu ana kinyongo au analipiza kisasi.
“Jivikeni upendo mwororo wenye huruma, fadhili, unyenyekevu wa akili, upole, na ustahimilivu.”
—Wakolosai 3:12.
3. JIPATIE NAFASI YA KUTULIA.
Ukikasirika, huenda ikafaa uondoke kwa busara ili utulie kidogo. Unaweza kwenda kwenye chumba kingine au ukatembee hadi utakapokuwa sawa. Kufanya hivyo si sawa na kumnyamazia mwenzako. Badala yake, huenda ni nafasi nzuri ya kusali ili Mungu akupe subira, ufahamu, na uelewaji.
“Kabla mabishano hayajalipuka, jiondokee.”
—Methali 17:14.
4. FIKIRIA KWA MAKINI NI NINI KINACHOHITAJI KUSEMWA NA JINSI YA KUKISEMA.
Hakuna faida ya kutafuta maneno ya kujibizana na mwenzako. Badala yake, jaribu kusema jambo litakalotuliza hisia zilizoumizwa za mpendwa wako. Na badala ya kumwamulia mwenzako hisia zake, mwombe ajieleze na umshukuru kwa kukusaidia kuelewa hisia zake.
“Kuna mtu anayesema bila kufikiri kama kwa upanga unaochoma, lakini ulimi wa mwenye hekima huponya.”—Methali 12:18.
5. ZUNGUMZA KWA SAUTI YA CHINI NA KWA NJIA INAYOONYESHA UNATAFUTA MAPATANO.
Mtu mmoja katika familia anapokosa subira anaweza kuamsha hasira ya mwenzake. Epuka kejeli, matusi, au kuzungumza kwa sauti ya juu, hata ikiwa unahisi umekosewa. Epuka kuwalaumu wengine kwa kusema mambo kama vile “Wewe hunijali” au “Wewe hunisikilizi kamwe.” Badala yake, mweleze mwenzi wako kwa utulivu jinsi ambavyo mwenendo wake ulivyokuathiri (“Ninaumia unapo . . . ”). Hupaswi kamwe kumsukuma mwenzako, kumpiga kofi, teke, au kumtendea kwa jeuri ya aina nyingine. Pia, hupaswi kumtukana, kumdhihaki, au kumtisha mwenzi wako.
“Uchungu wote wenye uovu na hasira na ghadhabu na kupiga kelele na matukano na viondolewe mbali kutoka kwenu pamoja na ubaya wote.”—Waefeso 4:31.
6. OMBA MSAMAHA UPESI NA UELEZE UTAKACHOFANYA ILI KUREKEBISHA HALI.
Usiache hisia zisizofaa zikufanye usahau kwamba lengo lako kuu ni kufanya amani. Kumbuka kwamba hamfaidiki mkilumbana. Lakini mkifanya amani, nyote wawili mnafaidika. Kwa hiyo, kubali kosa lako. Hata ikiwa unasadiki kwamba hujakosea, unaweza kuomba msamaha kwa sababu ya kukasirika, kwa kutenda kwa njia isiyofaa, au kwa kumkasirisha mwenzako bila kukusudia. Kudumisha amani kati yenu ni muhimu kuliko kushinda bishano. Na ukiombwa msamaha, uwe tayari kusamehe.
“Nenda ujinyenyekeze na kumsihi sana mwenzako.”—Methali 6:3.
Bishano linapokwisha, unaweza kufanya nini ili kuchangia amani ya familia? Jambo hilo litazungumziwa katika makala inayofuata.