Unayopaswa Kujua Kuhusu Malaria
Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba katika mwaka wa 2013, zaidi ya watu milioni 198, waliambukizwa malaria na imekadiriwa kuwa watu 584,000 walikufa kutokana na ugonjwa huo. Karibu watu 4 kati ya 5 waliokufa ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Ugonjwa huo unatishia mamia ya nchi na maeneo mbalimbali ulimwenguni, na watu bilioni 3.2 wanakabili hatari ya kuambukizwa.
1 MALARIA NI NINI?
Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea. Dalili zake hutia ndani homa, kuhisi baridi, kutokwa na jasho, maumivu ya kichwa na mwili, kichefuchefu, na kutapika. Dalili hizo zinaweza kuonekana baada ya saa 48 hadi 72, ikitegemea aina ya vimelea na muda ambao mtu amekuwa na ugonjwa.
2 MALARIA HUENEZWAJE?
-
Vimelea vya malaria vinavyoitwa Plasmodia, hungia katika mfumo wa damu kupitia kuumwa na mbu jike aitwaye Anopheles..
-
Vimelea hivyo huenda katika chembe za ini la mtu aliyeambukizwa, na huko vimelea huzaliana..
-
Wakati chembe za ini zinapopasuka, huruhusu vimelea, ambavyo hushambulia chembe nyekundu za damu ya mtu aliyeambukizwa. Huko, vimelea hivyo huzidi kuongezeka..
-
Wakati chembe nyekundu za damu zinapopasuka, huruhusu vimelea, ambavyo hushambulia kwa wingi zaidi chembe nyekundu za damu..
-
Mzunguko wa chembe nyekundu za damu unapovamiwa na mipasuko hiyo huendelea. Kisha mtu aliyeambukizwa huanza kuonyesha wazi dalili za malaria kila baada ya chembe nyekundu ya damu kupasuka.
3 UNAWEZA KUJIKINGA JINSI GANI?
Ikiwa unaishi katika nchi ambazo malaria imeenea . . .
-
Tumia chandarua. Chandarua hicho kinapaswa
-
kuwekwa dawa ya kuua mbu.
-
kisiwe na shimo au tundu.
-
kuchomekwa vizuri kwenye godoro.
-
-
Puliza dawa ya kuua wadudu nyumbani mwako.
-
Ikiwezekana, weka wavu wa kuzuia wadudu katika madirisha na milango, na utumie kiyoyozi na feni ili kufukuza mbu.
-
Vaa nguo zenye rangi nyangavu na zinazofunika mwili vizuri.
-
Inapowezekana, epuka kuwa katika maeneo yenye mbu wengi, mabwawa yenye mbu, na maji yaliyotuama, mahali ambapo mbu huzaliana.
-
Ikiwa umeanza kuugua tafuta matibabu haraka.
Ikiwa unapanga kutembelea nchi ambayo malaria imeenea . . .
-
Kabla ya kusafiri, pata habari za karibuni kuhusu ugonjwa huo. Kwani aina ya vimelea vya malaria wa eneo moja huenda vikatofautiana na vya eneo jingine, jambo hilo litakusaidia kuamua aina ya dawa inayofaa zaidi. Pia, litakuwa jambo la hekima kuwasiliana na daktari wako ili kujua mambo unayopaswa kuepuka kwa kuzingatia hali ya afya yako.
-
Unapokuwa katika nchi hiyo, fuata maelekezo yaliyo katika makala hii kwa ajili ya watu wanaoishi katika nchi zenye ugonjwa wa malaria.
-
Ikiwa umeambukizwa, tafuta matibabu haraka. Kumbuka kwamba huenda dalili hizo zikaonekana kati ya juma moja hadi majuma manne baada ya kuambukizwa.