Samaki Aina ya pono —Mashine ya kutengeneza Mchanga
Mchanga hutoka wapi? Kuna vyanzo vingi mbalimbali. Lakini huenda ukashangazwa na moja ya chanzo kinachoelezwa katika makala hii. Ni samaki anayesaga tumbawe na kuwa mchanga laini—samaki aina ya pono!
Pono (parrot fish) wanaishi katika maji ya kitropiki ulimwenguni pote. Baada ya kumeza kipande cha tumbawe, wanatafuta chembechembe za chakula na kutema mabaki, ambayo ni mchanga. Ili kufanya kazi yake, samaki huyo anatumia taya za midomo yake imara na meno yake magumu. Baadhi jamii za samaki hao wanaweza kuishi miaka 20 bila meno yake kupukutika.
Katika maeneo yenye matumbawe yaliyokufa, samaki huyo hutafuna kwa urahisi na kutokeza mchanga kwa wingi kuliko chanzo kingine chochote cha asili. Watafiti fulani wanakadiria kwamba samaki huyo huzalisha mamia ya kilogramu za mchanga kwa mwaka.
Pono hufanya kazi nyingine muhimu. Anapokula matumbawe yaliyokufa, miani iliyo kwenye tumbawe na majani, jambo hilo hudumisha usafi wa tumbawe. Tumbawe ni chakula muhimu kwa pono, na hii ndiyo sababu huyatunza matumbawe. Sehemu ambazo hakuna pono na viumbe wengine wanaofanya hivyo, matumbawe huharibiwa na miani na magugu-maji. “Wengine hudai kwamba matumbawe yaliyopo sasa yasingekuwa katika hali hiyo ikiwa kusingekuwa na viumbe kama hao,” kinaeleza kitabu Reef Life.
Kutokana na shughuli zote hizo za mchana, pono wanahitaji kupumzika vizuri wakati wa usiku, pindi hiyo pono hufanya jambo lisilo la kawaida. Wakati wa usiku ni hatari kuwa katika matumbawe, kwa sababu kuna viumbe wengi wanaowinda. Kwa kawaida pono hulala mafichoni chini ya mwamba, lakini sehemu hiyo iliyofichika haiwezi kuwalinda wakati wote kutokana na papa mwenye njaa.
Ili kuwa salama zaidi, baadhi ya samaki hao hujifunika wakati wa usiku. Wao hutoa ute wenye utelezi ambao hufunika kabisa miili yao, na kuwa kama gauni jangavu la usiku. Wanasayansi wa viumbe vya majini wanaamini kwamba harufu mbaya inayotoka kwenye ute huo huwalinda kutoka kwa viumbe wanaowawinda.
Pono ni miongoni mwa samaki wanaovutia na wale wanaoonekana kwa urahisi kwenye matumbawe. Mara nyingi pono jike na dume huwa na rangi zinazong’aa, ambazo hubadilika kwa kadiri wanavyoendelea kukua. Lakini jambo zuri hata zaidi ni kwamba pono hupatikana kwa wingi katika maeneo ambayo hawavuliwi kupita kiasi. Hivyo, ni samaki wanaoonekana kwa urahisi.
Unapomtazama kwa karibu pono na kumsikiliza anapotafuna juu ya tumbawe, ni baadhi ya mambo ambayo watafiti wa miamba ya matumbawe hawawezi kusahau. Pia, pono wanapofanya kazi yao, huboresha mazingira kwa viumbe wengine katika matumbawe na ili kufurahisha wanadamu.