Hewa Safi na Mwangaza wa Jua —Je, Ni ‘Dawa Asili Za Kuua Viini’?
KATIKATI ya karne ya 20 wanasayansi walipogundua kwa mara ya kwanza dawa ya kemikali ya kuua viini, madaktari walitumaini kwamba dawa hizo mpya zingeweza kuondoa baadhi ya magonjwa. Mwanzoni dawa hizo mpya zilionekana kwamba zinatimiza jambo hilo. Hata hiyo, baada ya matumizi ya dawa hizo kuongezeka, viini vinavyokinza dawa hizo vilitokea.
Katika jitihada zao za kutafuta silaha mpya ya kupambana na maambukizo, baadhi ya wanasayansi wameanza kuchunguza njia zilizotumiwa zamani kudhibiti magonjwa. Njia moja ni kuchunguza faida za afya zinazotokana na mwangaza wa jua na hewa safi.
Somo Kutokana na Njia Zilizotumiwa Zamani
Nchini Uingereza kulikuwa na watu wengi waliozungumzia faida zinazotokana na mwangaza wa jua na hewa safi. Daktari John Lettsom (1744-1815) aliwaandikia watoto waliougua kifua kikuu (TB), mwangaza wa jua na hewa kutoka baharini ikiwa sehemu ya matibabu. Katika mwaka wa 1840, daktari mpasuaji, George Bodington, alisema kwamba watu wengi waliofanya kazi nje, kama vile ukulima, uchungaji, hawakuugua kifua kikuu, lakini wale waliotumia wakati mwingi ndani ya nyumba walikabili hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo.
Florence Nightingale (1820-1910) alijulikana sana kutokana na uvumbuzi wake katika uuguzi alipokuwa akiwahudumia wanajeshi wa Uingereza waliojeruhiwa katika Vita vya Crimea. Aliuliza hivi: “Umewahi kuingia katika chumba cha mtu . . . usiku au asubuhi kabla hajafungua madirisha na kugundua kwamba hewa ni nzito na si safi?” Alipendekeza kwamba chumba cha mgonjwa kiwe wazi kwa kipindi fulani ili hewa safi ya nje iingie ndani bila kumsumbua mgonjwa. Akaongeza: “Kulingana na uzoefu niliopata katika kushughulikia wagonjwa, nimegundua kwamba wanahitaji mwangaza kama tu wanavyohitaji hewa safi . . . Si mwangaza tu bali mwangaza wa jua wa moja kwa moja.” Watu wengi wakati huo waliamini pia kwamba kuanika shuka na nguo nyingine
nje ili zipigwe na jua kulichangia afya bora.Ingawa sayansi imeendelea tangu miaka ya 1800, bado utafiti wa karibuni umefikia mkataa wa namna hiyo. Kwa mfano, utafiti uliofanywa nchini China katika mwaka wa 2011, ulionyesha kwamba mabweni ya chuo yaliyojaa watu na kukosa mfumo mzuri wa kupitisha hewa “yalitajwa kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya mfumo wa kupumua.”
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linakubali kwamba mfumo wa asili wa kupitisha hewa unaohusisha hewa kutoka nje kuingia na kutoka katika jengo, ni muhimu ili kupunguza maambukizo ya magonjwa. Hivyo, Shirika la Afya Ulimwenguni lilichapisha mwongozo katika mwaka wa 2009, uliopendekeza matumizi ya mfumo wa asili wa kupitisha hewa na kuutaja kuwa njia bora ya kupunguza hatari ya maambukizo katika vituo vya afya. *
Huenda ukasema, ‘Mambo hayo yanafaa. Lakini yanahusiana namna gani na sayansi? Mwangaza wa jua na hewa vinazuia namna gani maambukizo?’
Dawa za Asili za Kuua Viini
Utafiti uliofanywa katika eneo la Wizara ya Ulinzi ya Uingereza unatupatia baadhi ya majibu. Wanasayansi walikuwa wakijaribu kuona hewa ingeendelea kuwa hatari kwa kipindi gani cha wakati ikiwa silaha ya kibiolojia yenye bakteria hatari ingelipuliwa katika jiji la London. Ili kutambua ikiwa kuna virusi katika hewa, watafiti waliweka vijidudu vinavyoitwa E. coli katika nyuzi za hariri za buibui na kuziachilia katika hewa. Jaribio hilo lilifanywa usiku kwa kuwa mwangaza wa jua ungewaua bakteria hao. Matokeo yalikuwa nini?
Saa mbili baadaye, karibu bakteria wote walikuwa wamekufa. Hata hivyo, bakteria walipowekwa ndani ya sanduku lililofungwa katika eneo hilo, na kwa kiwango kilekile cha joto na unyevunyevu, bakteria wengi waliendelea kuwa hai hata baada ya saa mbili. Kwa nini? Kwa sababu ya hali fulani iliyo katika hewa safi inayoua viini. Hali hiyo haijajulikana kihususa. Hata hivyo, watafiti wanasema kwamba kuna mchanganyiko wa asili unaopatikana katika hewa “unaotenda kama kiua-viini wanaopatikana katika angahewa.”
Mwangaza wa jua pia una tabia za asili za kuua viini. Gazeti linaloitwa Journal of Hospital Infection linasema kwamba “idadi kubwa ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa yanayosambazwa kupitia hewa haviwezi kuendelea kuwa hai ikiwa kuna mwangaza wa jua.”
Utafaidikaje na hewa safi na mwangaza wa jua? Unaweza kutembea kwa ukawaida nje na kutumia kipindi fulani kufurahia hewa safi na mwangaza wa jua. Huenda ukanufaika sana kwa kufanya hivyo.
^ fu. 8 Huenda hali fulani zikafanya isifae kuacha madirisha wazi. Hali hizo zinatia ndani ubora wa hali ya hewa, kelele, sheria zinazohusu moto, na usalama.