JE, NI KAZI YA UBUNI?
Mguu wa Farasi
FARASI anaweza kukimbia kwa kasi ya mwendo wa kilometa 50 kwa saa. Ingawa hilo linahusisha misuli yenye uwezo wa pekee, yeye hutumia nguvu kidogo tu. Hilo linawezekanaje? Siri ni miguu yake.
Fikiria kinachotukia farasi anapokimbia. Misuli na kano hufyonza nishati mguu unapokanyaga chini, kisha huachilia mguu kwa ghafula kama springi na kumwezesha farasi kusonga mbele.
Isitoshe, farasi anapokimbia miguu yake hutikisika sana, jambo linaloweza kumuumiza kano. Hata hivyo, misuli yake ya miguu hupunguza mtikisiko. Watafiti wamesema muundo huo ni “ushirikiano wa kipekee kati ya misuli na kano” unaomwezesha farasi kuwa na kasi na pia nguvu.
Wahandisi wanajaribu kuiga muundo wa miguu ya farasi wanapotengeneza roboti zenye miguu minne. Hata hivyo kulingana na Maabara ya Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts, ni vigumu kuiga muundo huo tata hata kwa kutumia vifaa vya kisasa na ujuzi wa uhandisi uliopo.
Una maoni gani? Je, muundo wa mguu wa farasi ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?