Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 MSAADA KWA AJILI YA FAMILIA | NDOA

Jinsi ya Kudhibiti Matumizi

Jinsi ya Kudhibiti Matumizi

KIKWAZO

Unapotazama orodha yako ya mapato na matumizi unatambua kwamba pesa zinakuponyoka kama mchanga unavyopita katikati ya vidole. Muda mrefu haujapita tangu ulipofunga ndoa, na unashindwa kudhibiti matumizi. Je, utamlaumu mwenzi wako? Usikimbilie kufanya hivyo! Shirikiana naye kuchunguza mambo ambayo huenda yamewaingiza nyote wawili katika hali hiyo. *

KISABABISHI NI NINI?

Mabadiliko. Kama ulikuwa ukiishi nyumbani kabla ya kuolewa, huenda hukuzoea kulipa gharama za nyumbani na kuchangia malipo. Inawezekana pia kwamba wewe na mwenzi wako mna maoni yanayotofautiana kuhusu pesa. Kwa mfano, huenda mmoja wenu anapenda sana kutumia pesa na yule mwingine anapenda kuweka akiba. Inachukua muda kabla wenzi wa ndoa kufanya marekebisho na kukubaliana jinsi watakavyopangia matumizi ya pesa.

Kama magugu kwenye bustani, madeni yanayopuuzwa yatazidi kuongezeka

Kuahirisha mambo. Jim, ambaye sasa ni mwanabiashara mwenye mafanikio, anakiri kwamba mara tu baada ya kufunga ndoa, alisumbuka sana kwa kushindwa kudhibiti matumizi. Anasema: “Kwa vile nilichelewa kulipa gharama za nyumbani, mimi na mke wangu tulitumia pesa nyingi kulipia gharama zilizochelewa. Tuliishiwa na pesa!”

Mtego “usioonekana wa pesa.” Ni rahisi kutumia pesa kupita kiasi kama huoni zikitoka kwenye kibeti chako. Huenda ikawa hivyo ikiwa unatumia kadi ya benki kulipia gharama mbalimbali, au unanunua bidhaa kupitia Intaneti. Mtego wa kupata mkopo haraka unaweza pia kuwanasa wenzi wapya wa ndoa.

Vyovyote vile, matumizi ya pesa yanaweza kusababisha matatizo makubwa katika ndoa yako. “Watu wengi waliofunga ndoa husema kwamba pesa ndilo tatizo kubwa, bila kuzingatia kiasi walicho nacho,” kinasema kitabu Fighting for Your Marriage. “Pesa ndicho kisababishi kikuu cha mizozano.”

 UNACHOWEZA KUFANYA

Amueni kushirikiana. Badala ya kulaumiana, shirikianeni kudhibiti matumizi yenu ya pesa. Anzeni kwa kukubaliana kwamba hamtaruhusu matumizi ya pesa yawatenganishe.—Kanuni ya Biblia: Waefeso 4:32.

Pangeni bajeti. Andikeni gharama zenu zote kwa mwezi mmoja, kutia ndani gharama ndogondogo. Hilo litawasaidia kujua matumizi yenu ya pesa na kutambua matumizi yasiyofaa. “Lazima uache kumwaga pesa,” anasema Jim aliyetajwa mapema. “Yaani ujizuie kabisa.”

Andika orodha ya malipo muhimu, kutia ndani chakula, nguo, kodi au malipo ya nyumba, gharama za gari, na mambo kama hayo. Andika kiwango kinachohitajika kwenye kila sehemu, ili kuonyesha pesa mtakazotumia katika kipindi fulani, labda kwa mwezi.—Kanuni ya Biblia: Luka 14:28.

“Mkopaji ni mtumishi wa mtu anayemkopesha.”​—Methali 22:7

Tenga pesa kila mwezi kwa ajili ya kila matumizi (chakula, kodi, mafuta ya gari, na kadhalika). Watu fulani hufanya hivyo kwa kuweka pesa kwenye bahasha, kila bahasha kwa matumizi hususa. * Pesa zikiisha kwenye bahasha moja, wataacha kununua vitu vilivyotengewa bahasha hiyo au kuchukua pesa kutoka kwenye bahasha nyingine.

Fikiria upya maoni yako kuhusu vitu vya kimwili. Furaha haitegemei kuwa na vifaa vya kisasa. Yesu alisema: “Hata wakati mtu ana vitu vingi uzima wake hautokani na vitu alivyo navyo.” (Luka 12:15) Kwa kawaida matumizi yako ya pesa yanaonyesha kama unaamini maneno hayo.—Kanuni ya Biblia: 1 Timotheo 6:8.

Fanya marekebisho. “Ingawa huenda mambo kama kuwa na televisheni ya kisasa na kula hotelini yakaonekana yasiyogharimu mno, yanaweza kukuvuruga kifedha,” anasema Aaron, ambaye amekuwa katika ndoa kwa miaka miwili. “Tulilazimika kujinyima mambo fulani ili tuishi kulingana na mapato yetu.”

^ fu. 4 Ingawa makala hii inawalenga wale ambao wamefunga ndoa hivi karibuni, kanuni zinazotajwa zinawahusu wote waliofunga ndoa.

^ fu. 14 Kama unalipia vitu kwa kutumia kadi ya benki, weka orodha ya matumizi katika kila bahasha.