Kutafuta Wachawi Huko Ulaya
KARNE kadhaa zilizopita huko Ulaya, wachawi walianza kutafutwa na kuuawa. Shughuli hiyo ilifanyika huko Ufaransa, Ujerumani, Italia kaskazini, Uswisi, Ubelgiji, Luxembourg, na Uholanzi. “Maelfu na maelfu ya watu waliuawa huko Ulaya na katika koloni za Ulaya,” na “wengine wengi wakateswa, kukamatwa, kuhojiwa, kuchukiwa, kushutumiwa, na kutishwa,” kinasema kitabu kinachoitwa Witch Hunts in the Western World. * Shughuli hiyo inayotisha ilianzaje? Ni nini kilichoichochea?
Baraza la Kuhukumu na Nyundo ya Wachawi
Baraza la Kuwahukumu Wazushi lilihusika sana katika shughuli hiyo. Liliundwa na Kanisa Katoliki katika karne ya 13 “ili kuwabadili waasi imani na kuzuia wengine kuasi,” kinaeleza kitabu Der Hexenwahn (Kufichua Wachawi). Baraza la Kuwahukumu Wazushi lilikuwa kama kikosi cha polisi cha kanisa Katoliki.
Mnamo Desemba 5, 1484, Papa Innocent wa Nane alitoa hati iliyoshutumu uchawi. Pia, aliagiza washiriki wawili wa Baraza la Kuhukumu Wazushi, Jakob Sprenger na Heinrich Kramer (aliyejulikana pia kwa jina la Kilatini, Henricus Institoris)—wakabiliane na tatizo hilo. Wanaume hao wawili walichapisha kitabu kinachoitwa Malleus Maleficarum, yaani, Nyundo ya Wachawi. Wakatoliki na Waprotestanti walikubaliana na kitabu hicho. Kilikuwa na hadithi za kutungwa kuhusu wachawi zilizotegemea hekaya, na pia hoja za kidini na kisheria zilizopinga uchawi, vilevile mwongozo wa kuwatambua na kuwamaliza wachawi. Kitabu Malleus Maleficarum (Nyundo ya Wachawi) kimefafanuliwa kuwa “kitabu hatari zaidi . . . na chenye madhara zaidi kati ya maandishi yote ulimwenguni.”
Kitabu Malleus Maleficarum (Nyundo ya Wachawi) kimefafanuliwa kuwa “kitabu hatari zaidi . . . na chenye madhara zaidi kati ya maandishi yote ulimwenguni”
Mashtaka ya uchawi hayakuhitaji kuthibitishwa. Kitabu Hexen und Hexenprozesse (Wachawi na Kesi za Wachawi) kinasema kwamba mashtaka “yalikusudiwa kumfanya mshtakiwa akiri makosa yake kupitia kushawishiwa, kulazimishwa, au kwa nguvu.” Mateso yalikuwa jambo la kawaida.
Kufuatia kuchapishwa kwa kitabu Nyundo ya Wachawi na agizo la Papa Innocent wa Nane, jitihada kubwa ya kuwasaka wachawi ilianza huko Ulaya. Isitoshe, shughuli hiyo ilichochewa na teknolojia mpya ya kuchapisha ambayo ilisaidia kusambaza ujumbe huo uliovuka bahari ya Atlantiki na kufika Amerika.
Ni Nani Walioshtakiwa?
Zaidi ya asilimia 70 ya wale walioshtakiwa walikuwa wanawake, hasa wajane ambao kwa kawaida hawakuwa na mtu wa kuwatetea. Washtakiwa walitia ndani maskini, wazee, na wanawake waliouza madawa ya kienyeji—hasa kama hayakufanya kazi. Kila mtu alikabili hatari, awe tajiri au maskini, mwanamume au mwanamke, watu wa kawaida au mashuhuri.
Watu waliodhaniwa kuwa wachawi walilaumiwa kwa sababu ya maovu yote. Inadaiwa kwamba “walisababisha baridi kali na walileta konokono na jongoo ili kuharibu mbegu na matunda duniani,” linasema gazeti Damals la Ujerumani. Kama mvua ingeharibu mimea, kama ng’ombe angekosa kutoa maziwa, ikiwa mwanamume hakuwa na uwezo wa kuzalisha au mwanamke alikuwa tasa, wachawi ndio waliolaumiwa!
Wachawi walitambuliwaje? Washukiwa fulani walifungwa na kutiwa ndani ya maji baridi “yaliyobarikiwa.” Ikiwa wangezama walionwa kuwa wasio na hatia na walitolewa ndani ya maji. Kama wangeelea, walionwa kuwa wachawi na waliuawa mara moja au kufunguliwa mashtaka. Washukiwa wengine walipimwa uzani, kwa kuwa ilidhaniwa kwamba wachawi walikuwa na uzani mdogo.
Jaribio lingine lilihusisha kutafuta “alama ya Ibilisi,” ambayo ilikuwa “alama iliyoachwa na Ibilisi ili kuonyesha kwamba ana uhusiano na mchawi,” kinasema kitabu Witch Hunts in the Western World. Maofisa wangetafuta alama hiyo “kwa kunyoa nywele zote za mshukiwa na kuchunguza kila sehemu ya mwili wake”—hadharani! Kisha wangedunga kwa sindano alama yoyote iwe ni alama aliyozaliwa nayo au kovu. Ikiwa hakuhisi uchungu au kutoa damu alipodungwa, hiyo ilionwa kuwa alama ya Shetani.
Serikali za Wakatoliki na Waprotestanti ziliunga mkono shughuli ya kuwatafuta wachawi, na watawala fulani Waprotestanti walikuwa wakatili kuliko Wakatoliki. Hata hivyo, baada ya muda watu walibadili maoni yao. Kwa mfano, mnamo 1631, Friedrich Spee, kasisi Myesuiti aliyeandamana na “watu waliodhaniwa kuwa wachawi” wengi wakielekea kuchomwa mtini wakiwa hai, aliandika kwamba kulingana na maoni yake, hawakuwa na hatia. Na akaonya kwamba kama zoea la kutafuta wachawi halingekomeshwa, nchi ingebaki tupu! Wakati huohuo, madaktari walianza kutambua kwamba ugonjwa kama vile kifafa ulihusiana na afya bali si kuingiwa na mashetani. Katika karne ya 17, mashtaka dhidi ya wachawi yalipungua sana, na kufikia mwishoni mwa karne hiyo yakakoma kabisa.
Kipindi hicho kinachotisha kinatufundisha nini? Jambo moja muhimu ni hili: Wakristo walipoanza kufundisha uwongo wa kidini na mambo ya kishirikina badala ya kufuata mafundisho ya Yesu Kristo, walisababisha uovu mwingi! Ikitabiri kuhusu aibu ambayo Ukristo wa kweli ungepata kutokana na wanaume hao wasio waaminifu, Biblia ilionya hivi: “Ile njia ya kweli [inge]tukanwa.”—2 Petro 2:1, 2.
^ fu. 2 Koloni za Ulaya zilitia ndani mabara ya Amerika.
Washukiwa walipimwa uzani kwa sababu ilidhaniwa kwamba wachawi walikuwa wepesi