Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi ya Kuepuka Kununua Vitu Kupita Kiasi

Jinsi ya Kuepuka Kununua Vitu Kupita Kiasi

Mbali na kushinikizwa na wauzaji bidhaa, hisia zetu pamoja na mazoea yetu yanaweza kutuchochea kununua vitu kupita kiasi. Yafuatayo ni madokezo sita yatakayokusaidia kudhibiti ununuzi wako.

  1. Epuka kununua vitu ambavyo hukupangia. Je, wewe hufurahia msisimuko unaotokana na kununua vitu, hasa vile vilivyopunguzwa bei? Ikiwa ndivyo, huenda ukawa na mwelekeo wa kununua vitu ambavyo hukupangia. Ili kuepuka tabia hiyo, tua na ufikirie matokeo ya kununua, kumiliki, na kudumisha kitu unachotaka kununua. Fikiria kuhusu vitu ulivyonunua bila kupangia na baadaye ukajuta kwamba ulivinunua. Chukua muda kufikiria kwa uzito kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

  2. Epuka kununua vitu ili tu ujihisi vizuri. Kununua vitu kunaweza kukutuliza kwa muda unapohisi kuwa umeshuka moyo. Lakini hisia zisizofaa zinaporudi, huenda ukahisi kwamba unahitaji kununua vitu vingine ili upate kitulizo. Badala ya kununua vitu ili ujihisi vizuri, zungumza na marafiki wanaoweza kukusaidia au jihusishe katika utendaji fulani kama vile kwenda matembezi.

  3.   Usifanye ununuzi wa vitu kuwa tafrija. Maduka makubwa ya kifahari yamefanya ununuzi wa vitu kuwa burudani. Ingawa huenda lengo lako la kwenda madukani au kutazama bidhaa kwenye Intaneti likawa ni kufurahisha macho tu, vitu unavyoona vimekusudiwa kuchochea tamaa yako ya kununua. Nenda madukani wakati tu unahitaji kununua kitu fulani hususa, na ununue kitu hicho tu.

  4. Uwe mwangalifu unapochagua marafiki. Mtindo wa maisha na mazungumzo ya marafiki wako yanaweza kuchochea tamaa yako. Ikiwa unanunua vitu vingi kupita kiasi ili tu ufanane na marafiki wako, basi chagua marafiki ambao hawakazii sana pesa au mali.

  5. Chukua mikopo kwa hekima. Ni rahisi kuchukua mikopo bila kufikiria matokeo. Iwe unatumia njia gani kuchukua mkopo, jaribu kulipa kiasi fulani cha mkopo huo kila mwezi. Jua ni kiasi gani cha riba utakachotozwa kwa mkopo unaochukua. Jihadhari na mashirika ya kifedha yanayotoa mkopo wa kiasi kikubwa cha pesa bila masharti mengi. Badala ya kuchukua mkopo au kununua vitu kwa mkopo, weka pesa akiba hadi utakapoweza kununua kitu unachohitaji kwa pesa taslimu.

  6. Fahamu hali yako ya kifedha. Ni rahisi kutumia pesa kupita kiasi kwa sababu hujui hali yako ya kifedha. Weka rekodi ya matumizi yako na ujue hali yako ya kifedha kwa ujumla. Panga bajeti ya matumizi ya kila mwezi ikitegemea mapato yako na matumizi ya wakati uliopita. Linganisha matumizi yako na bajeti uliyopanga. Mwombe rafiki unayemwamini akusaidie kuelewa mambo ya kifedha ambayo hujui.