Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
“Kabla kompyuta hazijabuniwa, ilikuwa vigumu sana [kwa wataalamu wa mimea] kufanya utafiti kamili katika vitabu vyao kabla ya kupatia mimea mipya majina, kwa hiyo walianza kuipatia majina yanayofanana.” Sasa, imegunduliwa kwamba kati ya majina milioni moja hivi yaliyoorodheshwa, angalau majina 477,601 ni visawe tu.—SCIENCE, MAREKANI.
“Ni asilimia 6 pekee ya Wachina wanaosema kwamba wana furaha.” Asilimia 39 hivi ya wale waliohojiwa katika utafiti huo wanaamini kwamba “tatizo kubwa linalofanya watu wakose furaha” ni “utajiri.”—CHINA DAILY, CHINA.
“Uchunguzi uliofanywa . . . kuhusiana na takwimu za uhalifu nchini Urusi ulionyesha kwamba nchini kote kuna ‘udanganyifu wa hali ya juu’ kuhusiana na takwimu hizo.” Mashirika ya kutekeleza sheria yana hatia ya “kuficha ukweli wa mambo kuhusu uhalifu” na kutoa takwimu za uwongo zinazoonyesha kwamba wamekabiliana vilivyo na uhalifu na kumbe jambo hilo si kweli.—RIA NOVOSTI, URUSI.
“Mwanafunzi mmoja kati ya watatu kwenye vyuo vikuu katika mji mkuu wa Ujerumani [Berlin] anaweza kujihusisha na umalaya [kazi inayotia ndani ukahaba na kucheza dansi zinazoamsha nyege] kama njia ya kujipatia pesa ili alipe karo.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, UJERUMANI.
Kujipodoa kwa Ajili ya Kujifungua
Vituo vya mawasiliano vinaathiri jinsi akina mama wanavyotangaza kuwa wamejifungua. Ingawa zamani akina mama walituma telegramu, “sasa akina mama waliojifungua hutangaza habari hiyo ya furaha kupitia kwa Intaneti,” inasema ripoti moja ya kituo cha televisheni cha ABC cha Marekani. Tangazo hilo mara nyingi linatia ndani picha ya mama na mtoto mara tu anapozaliwa. Akina mama wachanga wa siku hizi, ambao huhangaikia sana umbo lao, wanapodolewa muda mfupi tu kabla ya kujifungua. “Wengine wao hufanya mipango ili waandamane na mpambaji hadi hospitalini,” inasema ripoti hiyo. Kwa nini? Wangependa kumetameta wanapojifungua, anaeleza Toni Golen, msimamizi wa kitengo cha kujifungua katika Kituo cha Afya cha Beth Israel Deaconess huko Boston.
Utendaji Humsaidia Mtu Kuwa na Afya Nzuri
Watafiti wanasema kwamba kukaa kitako kwa muda mrefu kazini, shuleni, au ukitazama televisheni bila kufanya mazoezi kunahusiana moja kwa moja na magonjwa ya kudumu. “Unapoketi, utendaji wa kimeng’enya kinachofanya misuli ifyonze mafuta kutoka kwenye damu na kuyachoma hupungua sana,” linasema gazeti Vancouver Sun. Kulingana na gazeti hilo, ili tuwe na afya nzuri ‘tunahitaji kufanya mengi zaidi ya mazoezi ya mara kwa mara yanayoufanya moyo upigepige kwa kasi. Tunahitaji kujihusisha katika utendaji mwepesi au wa kadiri, na tufanye hivyo kwa ukawaida na kwa kuendelea, ili mfumo wetu wa kumeng’enya uendelee kufanya kazi vizuri.’