Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Asilimia 17 hivi ya watoto wanaoenda shuleni nchini Brazili walio na umri wa miaka 10 hadi 13 wanawadhulumu wengine au wao ndio wanaodhulumiwa.—O ESTADO DE SÃO PAULO, BRAZILI.
Watoto walio na umri wa chini ya miaka 12 wanapatikana wakiwa na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu, kiwango cha juu cha kolesteroli, vijiwe vya figo, na matatizo ya ini. Visababishi vikuu ni nini? Hawafanyi mazoezi, wanakula chakula kingi kisicho na lishe, na ni wanene kupita kiasi.—ABC, HISPANIA.
Kulingana na makadirio ya serikali ya Marekani, gharama za kumlea mtoto aliyezaliwa mnamo 2008 katika familia yenye mapato ya kadiri, hadi atakapotimia umri wa miaka 18 ni “karibu dola 221,190 (au dola 291,570 unapokadiria kulingana na kuongezeka kwa gharama).”—WIZARA YA KILIMO, MAREKANI.
Kusahau Jinsi ya Kucheza
Kulingana na uchunguzi uliofanywa hivi karibuni, asilimia 20 ya wazazi nchini Uingereza wanasema kwamba wamesahau “jinsi ya kucheza na watoto wao.” Asilimia 33 wanasema kwamba kucheza kunawachosha, huku wengine wakisema kwamba hawana wakati wa kucheza wala hawajui ni mchezo gani watacheza na watoto. Professor Tanya Byron, ambaye ni mwanasaikolojia anasema hivi kuhusu matokeo ya uchunguzi huo: “Ili mzazi na mtoto wafurahie wakati ambao wanatumia kucheza, mambo manne ni muhimu: wakati huo unapaswa kuwa wenye kuelimisha, wenye kuchochea, wenye kumsaidia mtoto na mzazi wachangamane, na kuwasiliana.” Ingawa mzazi 1 kati ya 3 alipendelea kucheza michezo ya kompyuta pamoja na watoto wake, idadi kubwa ya watoto hupenda kucheza michezo hiyo peke yao. Michezo ambayo watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 15 hupendelea zaidi kucheza na wazazi wao ni ile ya nje ya nyumba au inayochezwa juu ya ubao.
Kusoma Hadithi Kabla ya Kulala
Huduma fulani ya Intaneti inasema kwamba inaweza kuwasaidia akina baba ambao hawana wakati wa kuwasomea watoto wao hadithi kabla ya kulala. “Programu za hali ya juu hurekodi sauti ya baba akisoma hadithi, inaongeza muziki na madoido mengine, kisha inamtumia mtoto hadithi hiyo katika barua-pepe,” linaeleza gazeti Daily Telegraph la Sydney. Hata hivyo, wataalamu wa mahusiano hawakubaliani kabisa na mbinu hiyo. “Kumsomea mtoto kunasaidia sana kujenga uhusiano pamoja naye,” anasema Dakt. Richard Fletcher ambaye anahusika katika uchunguzi fulani kuhusu familia katika Chuo Kikuu cha Newcastle, Australia. Akina baba wanapowasomea watoto wao, wanapata nafasi ya kuchangamana nao, kuwakumbatia, na kucheka pamoja. Hakuna barua-pepe inayoweza kumfaidi mtoto kama vile baba anavyoweza kumfaidi anapoketi chini na kumsomea, anasema Fletcher.