Walienda Kutafuta Dhahabu, Wakapata Makao
Walienda Kutafuta Dhahabu, Wakapata Makao
KATIKA majiji mengi ulimwenguni, mtu anaposikia kuhusu mji wa Wachina, anafikiria kuhusu maduka, mikahawa, sherehe, na dansi za dragoni za Wachina. Hata hivyo, kila mji wa Wachina una historia yake. Miji iliyo huko Australia leo ilianzishwa na wahamiaji Wachina walioenda huko, wakitarajia kupata utajiri katika machimbo ya dhahabu yaliyokuwa yamegunduliwa.
Mlima Mpya wa Dhahabu
Dhahabu ilipogunduliwa huko Australia katika mwaka wa 1851 Wachina walimiminika kwa wingi sana katika eneo hilo. Maelfu ya wanaume walifunga safari yenye magumu baharini kutoka delta ya Mto Pearl, iliyo katika Mkoa wa Guangdong, China kuelekea upande wa kusini wa dunia. Hapo awali dhahabu ilikuwa imegunduliwa huko California, Marekani, na Wachina waliozungumza Kikantoni waliyaita machimbo hayo ya dhahabu Mlima wa Dhahabu. Kwa hiyo, machimbo yaliyogunduliwa huko Australia yakaitwa Mlima Mpya wa Dhahabu.
Lakini wanaume hao hawakuhama ili tu wakatafute dhahabu. China ilikuwa imepatwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, misiba ya asili, na umaskini, na mambo hayo yalifanya hali iwe ngumu.
Kwa kuhuzunisha, baadhi ya Wachina wa kwanza kufunga safari kuelekea Australia hawakufanikiwa kuona fuo zake. Walikufa kwa sababu ya magonjwa yaliyoenea haraka katika meli zilizokuwa zimesongamana watu. Wale waliofaulu kufika nchi hiyo mpya waligundua kwamba maisha yalikuwa magumu sana kuliko walivyotarajia.
Kazi Ngumu Katika Machimbo ya Dhahabu
Wanaume hao walikuwa wapweke sana kwa kuwa kulingana na desturi, wanawake na watoto walibaki China ili kulinda mahali pao katika nasaba ya familia. Katika mwaka wa 1861, wanaume
Wachina zaidi ya 38,000 waliishi Australia, lakini kulikuwa na wanawake 11 tu Wachina. Hata hivyo, ni wachache tu waliokuwa wamepangia kuishi huko. Wengi wao walikuwa wameazimia kurudi nyumbani kwa familia zao wakiwa na utajiri na umashuhuri.Tamaa hiyo iliwafanya watafute dhahabu kwa bidii. Wachimbaji hao waliishi katika mahema na walifanya kazi ngumu kwa saa nyingi chini ya jua kali. Mwanzoni, baadhi yao waliogopa kuchimba migodi iliyokuwa chini ya ardhi kwa sababu ya ushirikina. Hivyo walianza kuchimba juu ya ardhi na kusafisha mchanga uliokuwa na dhahabu wakitumia milizamu ya mbao. Jitihada zao zilifanikiwa. Rekodi zinaonyesha kwamba kati ya mwaka wa 1854 na 1862, kilogramu 18,662 hivi za dhahabu zilizopatikana katika jimbo la Victoria zilipelekwa China.
Kwa kusikitisha, baadhi ya utajiri huo ulifujwa kwa kucheza kamari na uraibu wa kasumba—mazoea ambayo watu wapweke walijihusisha nayo. Mara nyingi matokeo yalikuwa kuharibika kwa afya na kupoteza mapato na tarajio la kurudi nyumbani. Baadhi ya watu hao walisaidiwa na mashirika ya Kichina na watu mmojammoja, lakini wengine walikufa wakiwa maskini na wapweke.
Wachina hao pia walikabili uhasama kutoka kwa wachimbaji wengine waliowaonea wivu na
kuwashuku kwa sababu Wachina walishirikiana kwa ukaribu na kufanikiwa katika uchimbaji wa dhahabu. Uhasama huo ulitokeza vurugu na mashambulizi dhidi ya Wachina. Dhahabu yao iliporwa, na mahema na mali yao kuteketezwa. Mwishowe uhasama huo ulipungua. Hata hivyo, miaka 50 hivi baada ya dhahabu kugunduliwa, Sheria ya Kuwazuia Wahamiaji ya 1901 iliwazuia wahamiaji kutoka Asia kuhamia Australia. Sheria hiyo ilifutiliwa mbali mwaka wa 1973.Dhahabu Ilipoisha
Migodi ilipoacha kutokeza dhahabu, Wachina fulani waliamua kubaki Australia. Kwa hiyo, Wachina walianzisha biashara za dobi, mikahawa, na mashamba madogo ya kukuza bidhaa za kuuzwa kwenye miji iliyokuwa na machimbo ya dhahabu. Wachina pia walijulikana kuwa watengenezaji bora wa fanicha na wauzaji matunda na mboga. Kwa sababu hiyo, kufikia mwisho wa karne ya 19, kulikuwa na jamii au miji ya Wachina katika majiji mengi ya Australia, kutia ndani Atherton, Brisbane, Broome, Cairns, Darwin, Melbourne, Sydney, na Townsville.
Kwa sababu kulikuwa na wanawake wachache sana Wachina huko Australia, wanaume wengi walibaki wakiwa waseja. Hata hivyo, wengine wao walioa wanawake Waaustralia ingawa wenyeji wengi hawakupenda ndoa za aina hiyo. Baada ya muda, wazao wa ndoa hizo za watu wa mataifa mawili wakawa sehemu ya jamii ya watu wa Australia.
Leo kuna wahamiaji wengi Wachina nchini Australia kuliko hapo awali. Wengi wao huja kwa sababu ya masomo ya juu na biashara. Isitoshe, wahamiaji hao wanatia ndani wanawake wengi. Kinyume na ilivyokuwa hapo awali, kwa sababu ya kubadilika kwa uchumi ulimwenguni, wanaume wengi Wachina huhamishia familia zao Australia, kisha wao hurudi bara Asia na kufanya kazi huko China, Hong Kong, Singapore, au Taiwan.
Kweli mambo yamebadilika. Lakini kwa wahamiaji ulimwenguni pote, malengo ni yaleyale, yaani, kupata usalama na mafanikio katika nchi ya kigeni.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]
MBALI KULIKO WALIVYOFIKIRI
Ili kuepuka kulipa ada au kodi ya kutua, abiria Wachina walishuka kutoka kwenye meli kabla haijafika kwenye bandari kubwa zilizo kwenye pwani ya Australia na mamia ya kilomita kutoka machimbo ya dhahabu. Mji wa Robe, Kusini mwa Australia, ulikuwa moja kati ya miji waliyotua. Robe ulikuwa na wakazi kati ya 100 na 200, na katika muda wa miezi mitano katika mwaka wa 1857, Wachina 12,000 hivi walipitia mji huo.
Katika tendo lenye kushangaza lilionyesha uvumilivu na ushirikiano, vikundi vya mamia ya wanaume vilipitia sehemu za ndani za nchi ambayo haikuwa na watu wengi vikielekea kwenye machimbo ya dhahabu. Hata hivyo, ilikuwa mbali kuliko walivyofikiri, na safari hiyo ilichukua majuma matano hivi. Walipokuwa njiani, wahamiaji hao walichuma majani ya baharini na kula kangaruu na wombati. Pia walichimba visima na kutengeneza njia ambayo wengine wangefuata.
Wakiwa wamefunga nywele zao nyuma na kuvalia kofia, wanaume hao walikimbia polepole kwenye mstari mmoja huku wakiimba. Sarafu za Kichina zimepatikana kwenye njia hiyo. Wahamiaji hao walitupa pesa zao walipogundua kwamba hazikuwa na thamani yoyote nchini Australia.
[Hisani]
Image H17071, State Library of Victoria
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]
KITU CHENYE THAMANI ZAIDI KULIKO DHAHABU
Wayne Qu alikuwa mwanasayansi wa mazingira katika Shirika la Kisayansi huko China. Ili apandishwe cheo, Wayne na mke wake Sue walienda Ulaya katika miaka ya 1990 kwa ajili ya masomo ya juu. Wakiwa huko, walikutana na Mashahidi wa Yehova na wakaanza kujifunza Biblia pamoja nao. Katika mwaka wa 2000, Wayne na Sue walihamia Australia, na wote wawili waliendelea na masomo yao ya juu—Sue akisomea biolojia ya molekuli. Pia waliendelea kujifunza Biblia.
Wayne anaeleza: “Tulikuwa tumetumia miaka mingi ili kupata digrii za juu zaidi katika chuo kikuu. Hata hivyo, nilijiuliza: ‘Mwishowe, sisi sote tutazeeka, tuwe wagonjwa, na tufe. Je, hilo ndilo kusudi la uhai?’ Mambo hayo yote yalionekana kuwa ubatili. Hata hivyo, Biblia ilinipa mimi na Sue majibu yenye kuridhisha, yanayopatana na akili kuhusu maswali muhimu maishani.
“Pia, kujifunza Biblia kulituwezesha kuchunguza wazo ambalo hatukuwa tumewahi kulifikiria, yaani, kuwapo kwa Muumba. Nilisoma kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? kilichochapishwa na Mashahidi na wakati uleule, nilisoma kitabu kuhusu mageuzi kilichoandikwa na Charles Darwin. Vitabu hivyo, pamoja na utafiti wa kisayansi niliofanya, ulinisadikisha kwamba kuna Muumba. Sue pia alisadikishwa.
“Jambo lingine lililotusadikisha kwamba kuna Mungu ni kwamba Biblia ina nguvu ya kuboresha maisha. Kwa kweli, kitabu hicho kizuri sana kimetupatia tumaini la wakati ujao, marafiki wa kweli, na pia kimeimarisha ndoa yetu. Mimi na Sue tulibatizwa mwaka wa 2005, na tunafurahi kwamba tumepata kitu chenye thamani zaidi kuliko elimu ya juu na ‘dhahabu ambayo huharibika.’”—1 Petro 1:7.
[Picha katika ukurasa wa 19]
Mchimbaji wa dhahabu Mchina, miaka ya 1860
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]
Sydney Chinatown: © ARCO/G Müller/age fotostock; gold miner: John Oxley Library, Image 60526, State Library of Queensland