Upweke Unasababishwa na Nini?
Upweke Unasababishwa na Nini?
KUNA tofauti kati ya upweke na kuwa peke yako. Upweke ni kuwa peke yako huku ukitamani kuwa na watu wa kushirikiana nao. Lakini mtu aliye peke yake ametengwa au kujitenga na watu wengine.
Ni vizuri kutaka kuwa peke yako nyakati nyingine. Mara nyingi watu hutafuta wakati wa kuwa peke yao ili wasali au kutafakari kama Yesu Kristo alivyofanya. (Mathayo 14:13; Luka 4:42; 5:16; 6:12) Kwa upande mwingine, upweke ni hisia inayoleta maumivu. Ni nini humfanya mtu ajihisi mpweke?
● Kujitenga Katika Majiji Yaliyojaa Watu
Katika majiji makubwa, maelfu au hata mamilioni ya watu huishi karibu-karibu. Hata hivyo, inashangaza kwamba msongamano huo wa watu huchangia upweke. Pilkapilka za maisha ya jijini hufanya watu wasiwafahamu vizuri majirani wao. Hilo huwafanya watu wanaoishi jijini wachangamane na watu wasiowajua. Hali ya watu kuwashuku watu wasiowajua na kutaka kulinda faragha yao, kumechangia pakubwa upweke katika majiji makubwa.
● Wafanyakazi Kutendewa Kinyama
Wasimamizi katika biashara na viwanda vikubwa wamefanya wafanyakazi wote wajihisi upweke na wasiofaa kitu. Mara nyingi, wafanyakazi hushinikizwa na kupata mkazo usiokoma.
Isitoshe, kuhamishwa-hamishwa kwa wafanyakazi katika makampuni makubwa huwafanya wahisi kwamba kazi yao iko hatarini, wametengwa, na ni wapweke. Likizungumzia idadi kubwa ya visa vya kujiua kati ya wafanyakazi wa makampuni fulani huko Ufaransa, gazeti International Herald Tribune lilisema kwamba “kwa sababu ya mabadiliko ya kiuchumi,” wafanyakazi wengi huko Ufaransa wanahisi kwamba “wanashinikizwa kupita uwezo wao.”
● Mawasiliano Yasiyo na Hisia
Nchini Japani, Profesa Tetsuro Saito alisema: “Simu za mkononi na vifaa vingine vinapunguza uwezo wetu wa kuwasiliana na wengine kwa hisia.” Huko Australia, gazeti The Sunday Telegraph liliripoti hivi: “Teknolojia . . . inawafanya watu wajitenge kihisia. Watu . . . hutumiana ujumbe mfupi au barua-pepe badala ya kuzungumza moja kwa moja.”
Akieleza ni kwa nini anajihisi mpweke, Rachel, mwenye umri wa miaka 21, anayeishi Ufaransa alilalamika hivi: “Watu hawajitahidi kukutembelea, kwa kuwa wanafikiri kwamba kukutumia ujumbe mfupi, barua-pepe, na kutumia vituo vya maongezi kunatosha. Lakini hilo hunifanya nijihisi mpweke hata zaidi.”
● Mazingira Mapya
Kuzorota kwa uchumi kumewalazimisha watu kuhamia maeneo mengine ili wadumishe kazi zao au watafute kazi. Kuhama hufanya watu waache majirani, marafiki, shule, na nyakati nyingine familia zao. Wale wanaohama ni kama mmea uliong’olewa na kupandwa mahali pengine lakini mizizi yake ikabaki mahali ulipong’olewa.
Francis, anakumbuka siku aliyowasili Ufaransa kutoka Ghana. Anaeleza, “Kwa kuwa sikuelewa lugha, sikuwa na marafiki, na kulikuwa na baridi sana, nilijihisi mpweke sana.”
Akikumbuka wakati alipowasili Uingereza akiwa mhamiaji, Behjat anasema: “Ilikuwa vigumu sana kuzoea desturi za huko. Niliwafahamu watu fulani lakini sikuwa na marafiki wa karibu au watu wa familia ambao ningeweza kuzungumza nao na kuwaeleza hisia zangu.”
● Kifo cha Mtu Unayempenda
Kifo cha mwenzi wa ndoa huacha pengo kubwa. Inakuwa hivyo hasa ikiwa mtu alimtunza mwenzi huyo kwa kipindi kirefu. Mtu huhisi maisha yake yakiwa matupu kabisa.
Fernande, mjane anayeishi Paris anaeleza, “Jambo linaloniumiza sana ni kwamba siwezi tena kumweleza rafiki yangu mkubwa, yaani, mume wangu mambo yaliyo moyoni.” Anny anasema kwamba anamkosa sana mume wake
“hasa wakati nina maamuzi muhimu ya kufanya kuhusu afya au mambo mengine.”● Talaka, Kutengana, Kuwa Mseja Bila Kutaka
Talaka au kutengana humfanya mtu ajihisi mpweke na hafai. Tofauti na ilivyodhaniwa na wataalamu, watoto ndio wanaoathiriwa zaidi. Wataalamu fulani wanasema kwamba kuna uwezekano wa watoto kuwa wapweke wanapokuwa watu wazima kwa sababu wazazi wao walitalikiana.
Wale ambao hawajafunga ndoa kwa sababu hawawezi kupata mwenzi wa ndoa anayefaa huhisi upweke pindi fulani. Hisia hizo zinaweza kuongezeka watu wanaposema maneno yenye kuumiza kama, “Ungekuwa na furaha zaidi ikiwa ungekuwa umefunga ndoa.”
Wazazi wasio na mwenzi pia huwa wapweke. Kazi ya kulea watoto ina shangwe na matatizo pia, na inabidi wazazi wasio na mwenzi watatue matatizo hayo wakiwa peke yao.
● Uzee na Vijana Wasio na Hekima
Huenda wazee wakahisi upweke hata ingawa wanatunzwa na watu wa familia. Huenda watu wa ukoo au marafiki wakawatembelea mara kwa mara, lakini namna gani pindi ambazo hakuna mtu anayewatembelea, labda kwa siku au majuma kadhaa?
Si wazee tu ambao huhisi upweke. Vijana wengi hujihisi wakiwa wapweke pia. Wengi wao wamekuwa waraibu wa burudani zisizohusisha watu wengine kama vile kutazama televisheni, kucheza michezo ya video, au kutumia kompyuta kwa saa nyingi.
Je, kuna suluhisho kwa tatizo hili linalozidi kuenea? Ni nini kinachoweza kumsaidia mtu kukabiliana na upweke?
[Blabu katika ukurasa wa 5]
“Kwa kuwa sikuelewa lugha, sikuwa na marafiki, na kulikuwa na baridi sana, nilijihisi mpweke sana”