Kwarara wa Kaskazini Aliyezuiwa Kuhamahama
Kwarara wa Kaskazini Aliyezuiwa Kuhamahama
FAMILIA ya washiriki watano iko tayari kuanza safari ndefu na marafiki wamekuja kuwaaga. Familia hiyo inatazama kwa mara ya mwisho eneo ambalo limekuwa makao yao kwa muda mrefu kisha wanaondoka. Marafiki wanawatazama hadi wanapotokomea.
Tumefika katika Kituo cha Kuzaliana cha Kwarara huko Birecik, mji ulio karibu na Mto Frati, Uturuki. Familia ambayo imeondoka ni ya kwarara wa kaskazini ambao wako katika hatari ya kutoweka. Kila ndege amefungiwa kifaa cha setilaiti kwenye mguu wake. Wafanyakazi na wageni walio na wasiwasi ikiwa ndege hao watarudi nyumbani, wanawatazama wakipaa na kuelekea katika eneo lisilojulikana.
Kwarara wa kaskazini ni ndege wa aina gani? Anapohama, yeye huelekea wapi? Na kwa nini tuchunguze kuhusu safari yake ya kuhama?
Jifunze Zaidi Kumhusu Ndege Huyu
Kwarara wa kaskazini anapoanguliwa huwa na manyoya kichwani. Hata hivyo, anapoendelea kukua manyoya hayo hung’oka. Sehemu nyingine ya mwili wake imefunikwa kwa manyoya meusi ambayo yanapopigwa na jua yanaonekana kuwa na rangi mbalimbali zinazometameta. Ngozi na mdomo wake ni wa rangi nyekundu isipokuwa kwenye sehemu ya juu ya kichwa chake. Pia kwarara huyu ana manyoya marefu nyuma ya shingo yake.
Kwarara hukomaa baada ya miaka mitatu au minne. Kwa kawaida kwarara huishi kati ya miaka 25 na 30. Anakula wadudu, mijusi, na wanyama wadogo. Kwarara wa kike anaweza kutaga yai moja au matatu kwa mwaka na kuyalalia kwa majuma manne hivi. Jambo lenye kushangaza kuhusu ndege hawa ni kwamba wao huishi na mwenzi mmoja maisha yao yote. Mmoja anapokufa, mwenzake huomboleza kifo hicho. Imeonekana mara nyingi kwamba mwenzi huyo anayeomboleza
huacha kula hadi afe au hata anajitupa chini kwenye mwamba.Wenyeji wa Birecik husema kuwa kufikia karne ya 20 watu wamekuwa wakisherehekea kurudi kwa kwarara baada ya safari yao ya kuhama. Waliamini kuwa ni ishara ya kukaribia kwa majira ya kuchipua. Wakati wa sherehe hiyo iliyofanywa Februari, mashua zilivutwa kwenye nchi kavu kutoka kwenye Mto Frati na kufuatiwa na kupigwa kwa ngoma na shamrashamra.
Wakati huo kulikuwa na makundi mengi ya kwarara hadi wangeonekana kama wingu kubwa jeusi lililo angani. Hata hivyo, katika karne iliyopita, na hasa katika miaka 50 iliyopita, idadi hiyo imepungua sana. Wakati mmoja kulikuwa na wenzi 500 au 600 huko Birecik, lakini katika miaka ya 1950 idadi hiyo ilipungua sana kwa sababu ya matumizi ya dawa za kuua wadudu. Leo kuna kwarara wachache tu ulimwenguni.
Juhudi za Kuwalinda Nchini Uturuki
Kituo cha Kuzaliana cha Kwarara kilianzishwa huko Birecik mnamo 1977. Ndege hao waliruhusiwa kuhamahama kila mwaka hadi mwaka wa 1990 wakati ambapo ni ndege mmoja tu alirudi. Kuanzia wakati huo, ndege hao walizuiwa wasihame. Katika mwezi wa Julai (Mwezi wa 7) na Agosti (Mwezi wa 8) wakati ambapo ndege hao wangeanza kuhama, wafanyakazi waliwafungia ndani ya vyumba vidogo. Walifungiwa humo hadi Februari au Machi (Mwezi wa 3) mwaka uliofuata, wakati ambapo wangetazamiwa kurudi.
Mnamo 1997 iliamuliwa kwamba ndege hao waruhusiwe kuhama. Jambo la kusikitisha ni kwamba kati ya ndege 25 walioachiliwa hakuna aliyerudi. Kuanzia mwaka wa 1998 na kuendelea, ndege wote waliendelea kuzuiwa wasihame. Lakini bado ndege hao wanaendelea kuongezeka. Kwa sasa kuna ndege 100 hivi katika kituo hicho.
Wakati Ujao wa Kwarara wa Kaskazini
Kwa kusikitisha, ni ndege wawili tu kati ya wale watano waliotajwa mwanzoni mwa habari hii waliorudi. Kisha, mnamo 2008 kikundi kingine cha ndege kiliruhusiwa kuhama. Wao pia hawakufaulu kurudi nyumbani. Wenye mamlaka waliripoti kuwa ndege hao walisafiri hadi kusini na kufika nchi ya Jordan lakini wakafa kutokana na sumu. Hivyo, licha ya kwamba idadi ya ndege hao inaongezeka katika kituo cha kuzaliana na wanasayansi na wenye mamlaka serikalini wanajitahidi sana kuwasaidia, bado wakati ujao wa ndege hao umo hatarini.
Jitihada za hivi karibuni zinaonyesha kwamba licha ya ndege hao kuzuiwa kuhama ili waweze kulindwa, bado hawajapoteza hisia yao ya kisilika inayowachochea kuhama. Jambo hilo linathibitisha maneno ya Biblia katika Yeremia 8:7: “Hata korongo juu mbinguni—anajua vema nyakati zake zilizowekwa; na njiwa-tetere na barawai na teleka—huangalia vema wakati wa kila mmoja wao kuingia.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]
Left: Richard Bartz; right: © PREAU Louis-Marie/age fotostock