Kwa Nini Wavulana Hawanipendi?
Vijana Huuliza
Kwa Nini Wavulana Hawanipendi?
Anajua mimi ninajulikana sana, kwa kuwa nimemwambia wavulana wengine wananipenda. Alicheka nilipomwambia jinsi marafiki wangu wengine walivyo wajinga. Anajua kuwa mimi ni mwerevu kwa sababu hata nimemrekebisha mara kadhaa. Sijui ni lini ataniomba tuwe marafiki wa karibu.
Yeye ni mrembo, lakini anaonekana kuwa hana akili sana! Siwezi kupata nafasi ya kuongea ninapokuwa naye. Na ninapopata nafasi ya kuongea, yeye hunirekebisha! Ninapomwona, mimi hutaka tu kutoroka.
JE, WEWE huhisi kuwa wavulana hawapendezwi nawe? Wasichana wengi huhisi hivyo hata wale ambao huenda ungefikiri hawana tatizo hilo! Kwa mfano, mfikirie Joanne. Ni mrembo, mwenye akili, na mwenye ufasaha. Lakini, yeye husema: “Mara nyingi mimi huhisi kuwa wavulana hawanipendi. Wachache ambao niliwapenda, walionyesha kuwa wanapendezwa nami kwa muda fulani kisha wakaacha kuongea na mimi kabisa!”
Ni mambo gani yanayowafanya wavulana wavutiwe na wasichana? Ni mambo gani yasiyowavutia? Bila kujishushia heshima, ni mambo gani unayoweza kufanya ili umvutie mvulana mzuri?
Mambo ya Kufanya
● Fahamu akili na moyo wako. Huenda ulivutiwa na wavulana hata zaidi baada tu ya kuanza kubalehe. Huenda ulivutiwa na mvulana zaidi ya mmoja. Hilo ni kawaida. Lakini ikiwa mara moja ungeruhusu uwe na hisia za kimahaba na mvulana wa kwanza uliyevutiwa naye, huenda ingeathiri ukuzi wako wa kihisia na kiroho. Inachukua muda kukomaa, na ‘kufanya upya akili zako’ kuhusu mambo yaliyo ya muhimu, na kufikia baadhi ya miradi yako mwenyewe.—Waroma 12:2; 1 Wakorintho 7:36; Wakolosai 3:9, 10.
Ni kweli kuwa wavulana wengi huvutiwa na wasichana ambao bado hawana msimamo thabiti au ambao hawana uzoefu. Hata hivyo, Mathayo 19:6.
wavulana kama hao huvutiwa tu na mwili wa msichana huyo na si jinsi alivyo kwa ndani. Ukweli ni kwamba, mvulana aliye na usawaziko atatafuta msichana ambaye watafaana.—Kile ambacho wavulana husema: “Mimi huvutiwa na msichana ambaye anaweza kutoa maoni yenye akili, anayejiamini kabisa.”—James.
“Ninapendezwa na msichana ambaye anaweza kujieleza kwa unyoofu na kwa adabu, na hakubaliani tu na kila kitu ninachosema. Hata kama yeye ni mrembo, sijihisi nikiwa huru na msichana ambaye husema mambo yanayonipendeza tu. Hilo huniogopesha!”—Darren.
“Ninakubali kuwa mara nyingi ninapokutana na msichana mrembo kwa mara ya kwanza, mimi huvutiwa naye. Lakini mara moja mimi huacha kuvutiwa naye ikiwa msichana huyu hana miradi hususa na inayofaa. Kwa upande mwingine, ikiwa anajua ni nini anachotaka kufanya na maisha yake—hasa ikiwa amefikia baadhi ya miradi yake—hilo humfanya avutie sana.”—Damien.
● Jifunze kuwaheshimu wengine. Kama tu vile wewe unavyotaka kupendwa, wavulana unaowafahamu pia hutamani sana kuheshimiwa. Si jambo la kushangaza kuwa Biblia humwambia mwanamume ampende mke wake lakini mke anapaswa “kumheshimu sana” mume wake. (Waefeso 5:33) Kwa kupatana na habari hii, uchunguzi uliyofanyiwa mamia ya vijana wa kiume ulifunua kuwa asilimia 60 walisema wanathamini sana heshima kuliko upendo. Zaidi ya asilimia 70 ya wanaume waliofanyiwa uchunguzi huo walikubaliana na hilo.
Heshima haimaanishi kusalimu amri—kwamba hupaswi kuwa na maoni yako mwenyewe na kuyaeleza hata kama ni tofauti na yake. (Mwanzo 21:10-12) Lakini jinsi unavyoeleza maoni yako itaamua kama mvulana huyo atavutiwa nawe au la. Ikiwa wakati wote utamrekebisha au utapinga kile anachosema, huenda akahisi kuwa humheshimu sana. Lakini ikiwa utakubali maoni yake na usifu kile unachoona kinapaswa kusifiwa, huenda atakubali na kuthamini maoni yako. Bila shaka, mvulana aliye na utambuzi ataona ikiwa unawatendea watu wa familia yako na watu wengine kwa heshima. *
Kile ambacho wavulana husema: “Wavulana hupenda kufikiri kuwa kuna mtu anayeona kuwa maoni yao ni muhimu, hasa msichana wanayempenda.”—Anthony.
“Nafikiri heshima ndilo jambo muhimu zaidi mwanzoni mwa urafiki. Upendo unaweza kusitawi baadaye.”—Adrian.
“Ikiwa msichana anaweza kuniheshimu, bila shaka atanipenda.”—Mark.
● Valia kwa kiasi, na udumishe usafi. Jinsi unavyovalia hutangaza kile unachofikiria na huonyesha wazi mtazamo wako. Kabla hujaanza kuongea na mvulana yeyote, mavazi yako tayari yanasema mengi kukuhusu. Ikiwa mavazi yako ni yenye mpangilio mzuri na ya kiasi, basi yatasema mambo mazuri kukuhusu. (1 Timotheo 2:9) Ikiwa mavazi yako ni yenye kuwavutia watu kingono au ni ya kizembe, basi yatasema mambo mabaya kukuhusu!
Kile ambacho wavulana husema: “Jinsi msichana anavyovalia huonyesha mtazamo wake kuelekea maisha. Ikiwa anavalia kizembe au nguo zenye kuonyesha uchi wake, hilo hunieleza wazi kuwa anataka sana kuwavutia watu wa jinsia tofauti.”—Adrian.
“Mimi huvutiwa sana na msichana anayetunza nywele zake, anayenukia vizuri, na aliye na sauti inayopendeza. Nilivutiwa na msichana mmoja mrembo, lakini kwa kuwa hakuwa safi niliachana naye.”—Ryan.
“Mimi huvutiwa na msichana ambaye hahisi anahitaji kutumia vipodozi vingi na nguo zenye kubana sana au zenye kuonyesha uchi wake ili awavutie watu wa jinsia tofauti.”—Ethan.
“Ikiwa msichana atavalia kwa njia yenye kuwavutia watu kingono, watu watavutiwa naye mara moja. Lakini singependa kuanzisha uhusiano na msichana wa aina hiyo.”—Nicholas.
Mambo ya Kuepuka
● Usiwachezee wengine kimapenzi. Wanawake wana uwezo mkubwa sana wa kuwavutia wanaume. Uwezo huo unaweza kutumiwa vibaya au vizuri. (Mwanzo 29:17, 18; Methali 7:6-23) Ikiwa utamjaribu kila mvulana unayekutana naye, mwishowe itasemekana kwamba wewe huwachezea wengine kimapenzi.
Kile ambacho wavulana husema: “Kukaa tu kando ya msichana anayevutia na kugusana naye mabega kunaweza kukusisimua na hata kuamsha hisia. Hivyo nafikiri msichana anayekugusagusa mnapoongea anachezea hisia zako.”—Nicholas.
“Ikiwa msichana anatafuta njia ya kugusagusa mkono wa kila mvulana anayekutana naye au anamtazama kila mvulana anayepita kwa mahaba, nafikiri anapenda kuwachezea wengine kimapenzi, na msichana wa aina hiyo hanivutii.”—José.
“Ninaweza kumfafanua msichana anayewachezea wengine kimapenzi kuwa msichana anayemgusa kila mvulana anayekutana naye na mara moja anamgeukia mvulana mwingine ambaye anamwonyesha upendezi.”—Ethan.
● Mpe nafasi ya kupumua. Biblia inasema kwamba watu wawili wanapooana wanakuwa “mwili mmoja.” (Mwanzo 2:24) Wakati huo ndipo mume na mke huachilia uhuru waliokuwa nao walipokuwa waseja; wanaanza kuwajibika kwa mmoja na mwenzake. (1 Wakorintho 7:32-34) Hata hivyo, ikiwa umeanza tu kuwa na uhusiano na mvulana fulani, usitazamie awajibike kwako kwa kadiri hiyo, naye hapaswi kutazamia hivyo kutoka kwako. Ukimharakisha akukazie fikira, huenda ukafanya urafiki wenu uvunjike. *
Kile ambacho wavulana husema: “Nafikiri msichana hanipi nafasi ya kupumua ikiwa anataka kujua kila kitu ninachofanya na hawezi kuwa na maisha ya kawaida au hata hapendezwi na mambo mengine isipokuwa mimi.”—Darren.
“Ikiwa msichana niliyekutana naye hivi karibuni ananitumia ujumbe mfupi kwa simu kila wakati na anataka kujua niko na nani, hasa majina ya wasichana katika kikundi changu, basi nafikiri hiyo ni ishara mbaya.”—Ryan.
“Ukiona msichana hakuruhusu ufanye mambo na marafiki wako wa kiume na anakasirika usipomwalika awe pamoja nawe kila wakati basi huyo ni kama kupe.”—Adrian.
Jione Kuwa Mtu wa Maana
Bila shaka unawajua wasichana ambao wanaweza kufanya chochote ili waonekane na wampendeze mvulana. Wengine huenda wanaweza kushusha viwango vyao ili tu wapate rafiki wa kiume au hata mume. Hata hivyo, kanuni ya ‘unavuna unachopanda’ inatumika. (Wagalatia 6:7-9) Ikiwa huthamini jinsi ulivyo na viwango unavyoishi kulingana navyo, basi utawavutia wavulana ambao hawakuthamini wewe au viwango vyako.
Ukweli ni kuwa si wavulana wote watakaovutiwa na wewe na hilo ni jambo zuri! Lakini ikiwa unajali sana urembo wako wa ndani na wa nje pia, ‘utakuwa na thamani kubwa machoni pa Mungu’—na utamvutia mvulana anayekufaa.—1 Petro 3:4.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 14 Ona sura ya 3 ya kitabu Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
^ fu. 28 Bila shaka, ikiwa wenzi wanachumbiana, wanapaswa kuwajibika kwa wachumba wao.
MAMBO YA KUFIKIRIA
● Unaweza kuonyeshaje kuwa unaheshimu maoni na hisia za mvulana?
● Unaweza kuonyeshaje kuwa unajiona kuwa wa maana?
[Picha katika ukurasa wa 27]
Upendo na heshima ni kama magurudumu mawili ya baiskeli—yote ni muhimu