Je, Unahisi Umefadhaika?
Je, Unahisi Umefadhaika?
ULIMWENGUNI pote, mgongano kati ya kazi na maisha ya familia ni suala kuu. Kama vile ripoti moja inavyoonyesha, ‘biashara ya kimataifa, teknolojia mpya, na mkazo wa kufanya kazi saa 24 siku 7 kwa juma, umefanya iwe vigumu kwa watu siku hizi kutofautisha wakati wa kuwa nyumbani na wa kuwa kazini.’ Mabadiliko hayo yameleta utajiri usio na kifani. Lakini mafanikio hayo yameleta pia madhara. Mwandishi mmoja anasema: “Wengi wetu tunafanya kazi kupita kiasi, tuna shughuli nyingi sana za kibinafsi, na tumelewa kabisa. Tumefadhaika sana.”
Kuongezea hayo, fikiria jinsi watu wameathiriwa na kuzorota upesi kwa uchumi ambako kumetokea hivi karibuni. Wafanyakazi ulimwenguni pote, iwe wanafanya kazi ofisini au kazi za mikono wamepoteza kazi na nyumba zao. Huenda wanatamani wangekuwa na kazi.
Hebu tuone matatizo hayo yameenea kadiri gani:
▶ Wafanyakazi 6 kati ya 10 huko Ulaya wana mfadhaiko unaosababishwa na kazi.
▶ Mfanyakazi 1 kati ya 3 huko Marekani anahisi kwamba anafanya kazi kupita kiasi.
▶ Zaidi ya wafanyakazi 2 kati ya 3 huko Kanada wanaona ni vigumu kusawazisha maisha ya familia na kazi.
▶ Inakadiriwa kwamba zaidi ya wafanyakazi milioni 600, au asilimia 22 ya wafanyakazi wote ulimwenguni, huwa kazini kwa zaidi ya saa 48 kwa juma.
Takwimu hizo zinaonyesha tatizo kubwa sana ambalo wanadamu wanakabili. Uchunguzi fulani unasema kwamba kufanya kazi kwa muda mrefu kwa saa zisizo za kawaida husababisha afya mbaya, kuvunjika kwa mahusiano, kuwa mzazi mbaya, kutengana, na talaka.
Vipi wewe? Je, unafanya kazi kupita kiasi? Au wewe ni miongoni mwa mamilioni ambao hawana kazi kwa sasa? Je, unatamani kuwa na usawaziko mzuri kuhusu kazi na maisha ya familia? Ikiwa ndivyo, utafanyaje hivyo?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 3]
KAZI YA PILI
“Ninaporudi nyumbani,” anasema mwanamke mmoja ambaye ameajiriwa, “lazima nipike chakula cha jioni, nisafishe nyumba, nioshe nguo, niwachukue watoto, niwasaidie na kazi zao za shuleni, niwaoshe, na nihakikishe kwamba wamelala. Ninapomaliza hayo yote, huwa nimechoka sana.” Mamilioni ya wanawake bilioni 1.2 hivi walioajiriwa huwa na kibarua hicho kigumu kama tu wanaume wengi. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kwamba mara nyingi wanaume hukataa kufanya kazi za nyumbani. Wanawake ndio hufanya kazi hiyo nyingi iwe wameajiriwa au la.