Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Albarracín—Mji Ulio Juu kama Kiota cha Tai

Albarracín—Mji Ulio Juu kama Kiota cha Tai

Albarracín—Mji Ulio Juu kama Kiota cha Tai

“Tembelea mojawapo ya miji maridadi zaidi nchini Hispania, tembelea Albarracín.”—José Martínez Ruiz, mwandishi Mhispania ambaye pia anaitwa Azorín, 1873-1967.

ALBARRACÍN ni mji wa pekee. Kwa nini? Kwanza ni kwa sababu ya mahali ulipo, historia yake, na mazingira yake yenye kupendeza. Kwa sababu hizo, mnamo 1961 serikali ya Hispania ilitangaza mji huo mdogo katika mkoa wa Teruel kuwa hifadhi ya kitaifa. Na mnamo 2005, kikundi cha wawakilishi wa watalii walichagua Albarracín kuwa “mji maridadi zaidi nchini Hispania.”

Mji wa Albarracín ulio kwenye milima ya Hispania ya kati, ni mji wa kale ulio na wakaaji 1,000 hivi. Mji huo umezungukwa na maeneo ya malisho yenye mito mingi na safu ya milima inayoitwa kwa jina la mji huo—Sierra de Albarracín.

Chanzo cha Chakula na Maji

Nyakati za kale wanyama wengi katika eneo hilo walifanya watu wahamie huko. Michoro iliyo kwenye mapango inaonyesha kwamba watu hao walikuwa wasanii stadi na walichunguza mazingira kwa makini. Walichora fahali wakubwa na wanyama wengine na wakawapaka rangi nyeupe inayoonekana tu katika eneo hilo. Wasomi wanafikiri kwamba mapango hayo ambayo yana michoro ya maisha ya kila siku yalitumiwa kufanyia mikutano ya kidini au ya umma.

Hata leo, mbawala, nguruwe-mwitu, na wanyama wengine wadogo wanapatikana kwa wingi katika hifadhi iliyo karibu ya Montes Universales. Na Mto Guadalaviar (neno la Kiarabu linalomaanisha “Mto Mweupe”) ni mojawapo ya mito ambamo trauti wanapatikana kwa wingi nchini Hispania.

Mnamo 133 K.W.K., Waroma walishinda makabila ya Waselti na Waiberia na wakajenga vijiji kadhaa katika eneo la Albarracín. Katika karne ya kwanza W.K., wahandisi Waroma walijenga mfereji (1) wenye urefu wa kilomita 18. Huo ulikuwa moja kati ya miradi migumu zaidi ya ujenzi uliofanywa na Milki ya Roma kwa ajili ya umma huko Hispania. Pia kuna uthibitisho wa kwamba watu walifuata dini ya Waroma. Mchongo kwenye jiwe la kaburi moja la Kiroma uliopatikana kwenye mji wa Albarracín ulionyesha kwamba watu waliabudu maliki.

Ufanisi Wakati wa Utawala wa Waislamu

Waarabu walikuwa wakitawala eneo hilo kufikia karne ya tisa, na inaaminiwa kwamba jina Albarracín limetokana na jina la Waislamu walioishi katika eneo hilo waliokuwa Waarabu wa ukoo wa Banu Razin. Katika Enzi za Kati, Waarabu, Wayahudi, na watu waliodai kuwa Wakristo waliishi pamoja wakiheshimiana na kwa amani. Kwa sababu hiyo, kipindi hicho ndicho kilichokuwa chenye ufanisi zaidi katika historia ya Albarracín.

Wasanii wa Albarracín walitengeneza vifaa maridadi, na pia inaonekana kwamba kulikuwa na matabibu wengi. Vifaa vya upasuaji vilivyochimbuliwa vinaonyesha kwamba madaktari hata walipasua watu waliokuwa na watoto wa jicho. Albarracín iliendelea kutawaliwa na Waislamu hadi mwisho wa karne ya 12 wakati ambapo mji huo ulianza kutawaliwa na Wakatoliki. Inaonekana kwamba katika historia yote ya Hispania huu tu ndio wakati ambapo mabadiliko kama hayo ya kisiasa yalifanyika kwa amani.

Mji wa Albarracín unaonekanaje leo? Bado mgeni anaweza kutembea katika barabara za mji huo wa kale, kwa kuwa hakuna jengo lolote la kisasa lililojengwa.

Jiji Lenye Kustaajabisha

Mwanafalsafa Mhispania José Ortega y Gasset (1883-1955) alisema kwamba Albarracín ni “jiji lenye kustaajabisha ambalo limening’inia mlimani.” Ufafanuzi huo unafaa, kwa kuwa mji huo umejengwa juu ya mwamba ulio mita 1,200 hivi juu ya usawa wa bahari na umezungukwa na korongo ndefu ambalo huwa kama handaki la maji lenye ulinzi. Ngome hii ya asili imelinda mji huo kwa karne nyingi na imefanya Albarracín iitwe Kiota cha Tai.

Mtu anapotembea kwenye barabara nyembamba za mji huo zilizojengwa kwa mawe, ataona majengo ya kale yenye kupendeza. Baadhi ya majengo hayo ni Corner Balcony, Blue House (2), na Julianeta House (3). Jengo la Julianeta linaonekana kana kwamba linaning’inia kati ya makutano ya barabara mbili.

Nyumba hizo za kale zimejengwa kwa mbao na lipu, vifaa ambavyo si vizito kama mawe. Matumizi ya vifaa hivyo ni muhimu unapofikiria kujenga juu ya mlima. Pia mgeni anaweza kuona madirisha yao madogo yenye pazia za lesi na vyuma (4). Pembe za paa zenye kupishana, veranda zenye matao ya mbao, vitu vya kubishia mlango visivyo vya kawaida ambavyo mara nyingi vinakuwa na maumbo ya wanyama, hufanya nyumba hizo ziwe za pekee.

Mtu yeyote ambaye hupatwa na kizunguzungu anapaswa kuwa mwangalifu asiangalie chini anapoingia kwenye nyumba hizo zinazoning’inia. Kwa kuwa mji huo umejengwa juu ya mwamba uliojitokeza, hakukuwa na nafasi ya kutosha kwa hiyo, wakaaji walijenga baadhi ya nyumba zao ukingoni kabisa mwa mwamba.

Kasri la Kiarabu limejengwa kwenye kilele cha mlima juu ya mji huo, mahali ambapo mji wa Albarracín ulianza kujengwa. Torre del Andador ni sehemu ya ukuta uliojengwa na Waarabu katika karne ya kumi. Majengo yaliyojengwa baadaye ni Kanisa la Kigothi, lililojengwa katika karne ya 16, na jumba la baraza la jiji lenye umbo la kiatu cha farasi ambalo lina veranda zenye matao.

Hazina za Asili

Kwa watu wanaopenda mazingira, Albarracín ina mambo mengi zaidi yenye kupendeza. Safu ya milima inayozunguka mji huo ina mimea na wanyama wengi. Chemchemi, vijito, na maporomoko ya maji hufanya milima hiyo yenye misitu ipendeze sana. Na watu ambao hupiga kambi huko hufurahia kuona nyota nyingi usiku.

Familia kadhaa za Mashahidi wa Yehova huishi katika eneo hilo. Mazingira yao maridadi huwakumbusha ahadi ya Biblia kwamba chini ya Ufalme wa Mungu wanadamu wataishi katika paradiso iliyoenea ulimwenguni pote. Wao hujitahidi kuwaambia jirani zao habari hizo njema.—Zaburi 98:7-9; Mathayo 24:14.

Kila mwaka watalii zaidi ya 100,000 hutembea katika barabara nyembamba za Albarracín. Ukitembelea Hispania, tembelea mji huo wa pekee ulio juu ya milima kama kiota cha tai.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

SANAA ZENYE THAMANI ZANGUNDULIWA ALBARRACÍN

Chupa ya fedha yenye mafuta. Mfalme Abdelmelic wa Waarabu aliagiza kwamba mke wake Zahr ambaye jina lake linamaanisha “Ua” katika Kiarabu, atengenezewe chupa hiyo. Maandishi yaliyoandikwa kwa dhahabu kwenye chupa hiyo yanasema hivi: “Baraka za kudumu . . . , msaada wa Mungu, na mwongozo wa kufanya yaliyo mema na haki.” Chupa hiyo inaonwa kuwa mojawapo ya hazina bora kabisa ya fedha kati ya sanaa za enzi za Wahispania na Waarabu.

Samaki aliyechongwa kwenye mwamba wa fuwele. Samaki huyo ana magamba, mdomo wa fedha, na mapezi ya dhahabu. Amerembeshwa kwa lulu na zabarijadi. Samaki huyo amechongwa kwa ustadi sana hivi kwamba wataalamu wanaamini haiwezekani kuwa mchongaji mmoja angemaliza kumchonga maishani mwake.

[Hisani]

Jar: Museo de Teruel. Foto Jorge Escudero; crystal: Sta. Ma de Albarracín Foundation

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

URENO

HISPANIA

MADRID

Albarracín

[Picha katika ukurasa wa 17]

1 Aqueduct

[Picha katika ukurasa wa 18]

2 Blue House

3 Julianeta House

4 Iron grille

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

© Ioseba Egibar/age fotostock