Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Harpy—Tai Mwindaji Katika Msitu wa Mvua

Harpy—Tai Mwindaji Katika Msitu wa Mvua

Harpy—Tai Mwindaji Katika Msitu wa Mvua

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI EKUADO

▪ Wavumbuzi wa kale huko Amerika Kusini walishtuka walipomwona ndege huyo mkubwa. Walistaajabishwa sana na ndege huyo hivi kwamba wakamwita harpy, jina la jitu lenye kuogopesha lililokuwa nusu ndege na nusu mwanamke linalotajwa katika hekaya za Wagiriki.

Leo, ndege huyo mkubwa bado anawastaajabisha watu. Akiwa na kimo cha sentimita 91 na mabawa yenye upana wa mita 2 kutoka ncha moja hadi nyingine, ndege huyo anayepatikana katika misitu ya mvua ya Amerika ya Kati na Kusini ni mmoja kati ya tai wakubwa na wenye nguvu zaidi ulimwenguni. Ndege wa kike ndio wakubwa zaidi na wanaweza kuwa na uzito wa kilogramu 9.

Tai huyo mkubwa ana kucha zinazoweza kukua na kufikia urefu wa sentimita 13 hivi, urefu maradufu wa kucha za tai anayeitwa bald-eagle. Isitoshe, kulingana na gazeti National Geographic Today, kucha za tai huyo zina nguvu sana hivi kwamba zinaweza kuvunja “mifupa ya aina fulani ya nyani, kima, na wanyama wengine ambao tai huyo huwawinda katika msitu wa mvua, na mara nyingi huua wanyama hao mara moja.” Hata hivyo, licha ya ukubwa wake na kucha zake ndefu, tai huyo huruka akiwa kimya hivi kwamba huenda usimwone anapopita juu angani.

Ndege Aliye Hatarini

Ingawa wanadamu hawaogopeshwi na tai huyo, yeye ana sababu za kuwaogopa wanadamu. Kwa sababu ya uwindaji haramu na kuharibiwa kwa misitu, ndege huyo amewekwa kwenye orodha ya wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka, na ni vigumu sana kumwona mwituni. Katika jitihada za kumwokoa tai huyo, serikali ya Panama ilimtangaza kuwa ndege wa kitaifa na wawindaji haramu hupewa adhabu kali.

Nchini Ekuado, pia jitihada zimeanzishwa za kumwokoa tai huyo. Akizungumza na mwandishi wa Amkeni! daktari wa wanyama Dakt. Yara Pesantes wa Mbuga ya Wanyama ya Guayaquil alieleza kwamba tai harpy huanza kutaga mayai wanapofikia umri wa miaka minne au mitano. Hata wanapofikia umri huo, wao hutaga yai moja au mawili baada ya kipindi cha miaka miwili. Kwa sababu wao huzaana baada ya kipindi kirefu, inakuwa vigumu kuwahifadhi. Lakini programu ya kuwazalisha wakiwa kwenye hifadhi tayari imetokeza kifaranga mwenye afya, akasema Dakt. Pesantes.

Hata hivyo, hivi karibuni hakutakuwa na uhitaji wa kuwaweka tai hao katika hifadhi. Kwa sababu gani? Muumba, Yehova Mungu, atatawala kila kitu duniani na kuthibitisha kabisa kwamba hakuiumba dunia na viumbe wote waliomo bila sababu.—Zaburi 104:5; Isaya 45:18.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kutayarisha kumweka tai kitambulisho

[Hisani]

Pete Oxford/Minden Pictures

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Tui De Roy/Roving Tortoise Photos