Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtu Aliyechora Ramani ya Dunia

Mtu Aliyechora Ramani ya Dunia

Mtu Aliyechora Ramani ya Dunia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UBELGIJI

Mwanzoni mwa mwaka wa 1544, Gerardus Mercator alijikuta katika seli ya gereza iliyokuwa na baridi na giza. Alikuwa na uhakika kwamba angeuawa. Kwa nini jambo hilo lilimpata mchoraji ramani huyo mkuu wa karne ya 16? Ili tupate jibu, acheni tuchunguze maisha yake na kipindi alichoishi.

MERCATOR alizaliwa mwaka wa 1512 huko Rupelmonde, bandari ndogo karibu na Antwerp, Ubelgiji. Alisomea katika chuo kikuu cha Louvain. Baada ya kuhitimu, alisomea mafundisho ya Aristoto lakini baada ya muda mfupi akaanza kutatanika kwa sababu hakuona upatano kati ya mafundisho ya Aristoto na Biblia. Mercator aliandika hivi: “Nilipoona kwamba simulizi la Musa la mwanzo wa dunia halikupatana na maoni ya Aristoto na wanafalsafa wengine, nilianza kuwashuku wanafalsafa wote nami nikaanza kuchunguza uumbaji.”

Kwa kuwa hakutaka kuwa mwanafalsafa, Mercator aliacha masomo katika chuo kikuu. Hata hivyo, katika maisha yake yote alijaribu kuthibitisha kwamba simulizi la Biblia la uumbaji ni sahihi.

Anageukia Jiografia

Mnamo 1534, Mercator alianza kujifunza hisabati, astronomia, na jiografia chini ya mwanahisabati Gemma Frisius. Isitoshe, huenda Mercator alijifunza uchoraji kutoka kwa Gaspar Van der Heyden, aliyekuwa mchoraji na mtengenezaji wa ramani zenye umbo la duara. Mwanzoni mwa karne ya 16, wachoraji ramani walitumia herufi nzito zinazoitwa Gothic zilizochukua nafasi nyingi kwenye ramani. Hata hivyo, Mercator alitumia mwandiko mpya uliobuniwa huko Italia unaoitwa italiki ambao unaandikwa kwa herufi zilizolazwa na kuunganishwa. Mwandiko huo ulisaidia sana kutengeneza ramani zenye umbo la duara.

Katika mwaka wa 1536 Mercator alifanya kazi ya kuchora na kutengeneza ramani yenye umbo la duara akishirikiana na Frisius na Van der Heyden. Mwandiko maridadi wa Mercator wenye herufi zilizounganishwa ulisaidia sana kufanikiwa kwa mradi huo. Nicholas Crane, mwandishi wa kisasa wa maisha ya Mercator, anaandika kwamba ingawa mchoraji ramani mwingine “alifaulu kuandika maeneo hamsini ya Amerika kwenye ramani ya ukutani iliyokuwa na upana unaolingana na kimo cha mwanadamu, Mercator aliandika maeneo sitini katika duara yenye upana unaotoshana na viganja viwili vya mkono”!

Kutokea kwa Mchoraji wa Ramani

Kufikia 1537, Mercator alitokeza mchoro wake wa kwanza bila msaada wa watu wengine. Ilikuwa ramani ya ile Nchi Takatifu, ambayo aliichora ili kuwasaidia watu “waelewe vizuri zaidi [Agano la Kale na Agano Jipya].” Katika karne ya 16, ramani za hiyo Nchi Takatifu hazikuwa sahihi hata kidogo, baadhi yake zikiwa na majina ya maeneo yasiyozidi 30 na mengi kati ya majina hayo yakiwa mahali pasipofaa. Hata hivyo, ramani ya Mercator ilionyesha zaidi ya maeneo 400! Isitoshe, ilionyesha njia ambayo Waisraeli walipitia walipokuwa wakisafiri jangwani baada ya kutoka Misri. Kwa sababu ya usahihi wake, ramani hiyo ilipendwa sana na watu walioishi kipindi kimoja na Mercator.

Akichochewa na mafanikio yake, Mercator alitokeza ramani ya ulimwengu mnamo 1538. Kabla ya wakati huo, wachoraji wa ramani hawakujua mengi kuhusu Amerika Kaskazini na waliiita Nchi ya Mbali Isiyojulikana. Ingawa tayari kulikuwa na jina la kijiografia “Amerika,” Mercator ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia jina hilo kurejelea Amerika Kaskazini na Kusini.

Mercator aliishi wakati ambapo watu walikuwa wakisafiri kwenye bahari za ulimwengu na maeneo mengi mapya yalikuwa yakivumbuliwa. Mabaharia walitoa habari zenye kupingana zilizofanya iwe vigumu kuchora ramani na hivyo wachoraji wa ramani walihitaji kukisia habari ambazo hawakupewa. Hata hivyo, mnamo 1541, Mercator alifaulu kuchora “ramani kamili zaidi ya dunia ambayo imewahi kutolewa.”

Ashtakiwa kwa Kueneza Uvumi

Huko Louvain, ambako Mercator aliishi, kulikuwa na Walutheri wengi. Kufikia mwaka wa 1536, Mercator alipendelea imani ya Walutheri, na inaonekana kuwa baadaye mke wake alikuwa Mlutheri. Mnamo Februari (Mwezi wa 2) 1544, Mercator alikamatwa pamoja na raia wengine 42 wa Louvain kwa mashtaka ya kuandika “barua zenye kutiliwa shaka.” Hata hivyo, huenda pia ikawa alikamatwa kwa sababu ramani yake ya ile Nchi Takatifu ilitiliwa shaka na Tapper na Latomus, wanatheolojia wawili kutoka chuo kikuu cha Louvain. Wanaume hao wawili walikuwa wamesimamia kesi ya mtafsiri wa Biblia William Tyndale, ambaye aliuawa huko Antwerp mnamo 1536. Huenda Tapper na Latomus walikuwa na wasiwasi kwamba ramani ya Nchi Takatifu iliyochorwa na Mercator ingewachochea watu kusoma Biblia, kama tu ile tafsiri ya Biblia ya Tyndale. Vyovyote vile, Mercator alifungwa katika kasri la Rupelmonde, mji aliozaliwa.

Antoinette Van Roesmaels, mmoja wa watu waliokuwa wameshtakiwa, alitoa ushahidi kwamba Mercator hakuwa amewahi kujiunga na kikundi cha Waprotestanti waliokuwa wakisoma Biblia kisiri. Hata hivyo, kwa kuwa Antoinette alikuwa amejiunga na kikundi hicho, alizikwa akiwa hai na akafa kwa kukosa hewa. Mercator aliachiliwa baada ya kufungwa kwa miezi saba, lakini mali yake yote ilitwaliwa. Mnamo 1552, Mercator alihamia Duisburg, Ujerumani ambako watu hawakuwa na ubaguzi wa kidini.

Atlasi ya Kwanza

Mercator aliendelea kutetea simulizi la Biblia la uumbaji. Alitumia wakati mwingi kuandika muhtasari wa simulizi lote la uumbaji “wa mbingu na dunia, kuanzia mwanzo wa nyakati hadi sasa,” kama alivyosema. Muhtasari wake ulitia ndani habari kuhusu mfuatano wa matukio na jiografia.

Mnamo 1569, Mercator alichapisha orodha ya matukio muhimu zaidi ya kihistoria kuanzia uumbaji na kuendelea, ambayo ilikuwa sehemu ya kwanza ya muhtasari wake, ulioitwa Chronologia. Kusudi lake lilikuwa kuwasaidia wasomaji wake kutambua kipindi walichoishi kwa kulinganishwa na historia. Hata hivyo, kwa kuwa katika kitabu chake Mercator alikuwa ametia ndani malalamishi ya Luther kuhusu malipo ya kupata msamaha yaliyoandikwa mwaka wa 1517, kitabu Chronologia kilitiwa katika fahirisi ya Kanisa Katoliki ya vitabu vilivyopigwa marufuku.

Katika miaka iliyofuata, Mercator alitumia wakati wake mwingi akichora na kuchonga mabamba ya kuchapishia kwa ajili ya uchapishaji wa ramani zake mpya. Mnamo 1590, Mercator alipatwa na ugonjwa wa kiharusi ambao ulimfanya asiweze kuzungumza na kumfanya apooze upande wa kushoto. Hilo lilifanya iwe vigumu kwake kuendelea kufanya kazi yake. Hata hivyo, aliazimia kumaliza kazi yake, na akaendelea hadi alipokufa mnamo 1594 akiwa na umri wa miaka 82. Rumold, mwana wa Mercator, alimaliza kuchora ramani tano za baba yake. Ramani zote za Mercator zilichapishwa mnamo 1595. Huo ndio uliokuwa mkusanyo wa kwanza wa ramani kuitwa atlasi.

Atlasi ya Mercator ilikuwa na maelezo ya sura ya kwanza ya Mwanzo, ambayo yalitetea uasilia wa Neno la Mungu licha ya upinzani kutoka kwa wanafalsafa. Mercator aliyaita maelezo hayo “lengo la kazi zangu zote.”

“Mwanajiografia Mkuu wa Siku Zetu”

Toleo lililoongezwa ukubwa la Atlasi, iliyochapishwa na Jodocus Hondius mnamo 1606 lilichapishwa katika lugha nyingi na nakala nyingi sana zikauzwa. Abraham Ortelius, mchoraji wa ramani wa karne ya 16 alimsifu Mercator kuwa “mwanajiografia mkuu wa siku zetu.” Hivi karibuni, mwandishi Nicholas Crane alimfafanua Mercator kuwa “mtu aliyechora ramani ya kwanza ya dunia.”

Bado tunafaidika kutokana na kazi za Mercator kila siku. Kwa mfano, wakati wowote tunapoangalia atlasi au kutumia Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Satelaiti (GPS), tunafaidika kutokana na kazi za Mercator, mwanamume mwenye kutokeza ambaye maisha yake yote alijitahidi kujua mahali pake katika uumbaji wa Mungu.

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

MERCATOR—MWANAFUNZI WA BIBLIA MWENYE BIDII

Mercator aliamini kwamba dunia ingekuwa mahali penye uadilifu, amani, na ufanisi. Aliandika muhtasari ambao haukuchapishwa wa Waroma sura ya 1-11 ambamo alikanusha fundisho la Calvin kwamba kila kitu kimeamuliwa mapema. Kwa kushangaza, alimpinga Martin Luther na kusema kwamba matendo yalihitajika ili mtu aokolewe si imani tu. Katika barua moja, Mercator aliandika kwamba dhambi “haitoki kwenye sayari [unajimu] wala haitoki kwa mwelekeo wa viumbe vya Mungu, lakini inatokana na uhuru wa kuchagua wa mwanadamu.” Katika barua yake alipinga fundisho la Kikatoliki kwamba mkate na divai hugeuka na kuwa mwili na damu halisi ya Kristo, na akasema kwamba maneno ya Yesu “huu ni mwili wangu” hayapaswi kuchukuliwa kihalisi, badala yake yanapaswa kuchukuliwa kwa njia ya mfano.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]

MISTARI YA MERCATOR

Je, umewahi kujaribu kunyoosha ganda la chungwa? Bila shaka, huwezi kufanya hivyo bila kuharibu umbo lake. Mfano huo unaonyesha tatizo linalowakabili wachoraji wa ramani wanapojaribu kuchora umbo la duara la dunia kwenye ramani iliyo tambarare. Mercator alitatua tatizo hilo kwa kuanzisha mfumo unaoitwa mistari ya Mercator. Katika mbinu hiyo, mistari inayotambulisha digrii za latitudo kutoka kwenye ikweta hadi kwenye vizio imeachana kwa nafasi zinazotoshana. Ingawa mbinu hiyo haionyeshi kwa usahihi umbali na ukubwa (hasa kuelekea kaskazini na kusini), ilikuwa hatua kubwa katika uchoraji wa ramani. Ramani ya ukutani ya Mercator ya mwaka wa 1569 iliyoonyesha dunia yote ilikuwa ndiyo uchoraji wake bora zaidi na ilichangia sana katika kumfanya awe mchoraji mashuhuri wa ramani. Kwa kweli, mistari ya Mercator bado inatumiwa katika ramani za bahari na katika Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Satelaiti wa kisasa.

[Picha]

Mistari ya Mercator inaweza kulinganishwa na pipa lililokatwa na kufunguliwa ambapo dunia imenyooshwa

[Picha katika ukurasa wa 20]

Ramani ya Mercator ya Nchi Takatifu aliyochora 1537, ilionyesha zaidi ya maeneo 400

[Picha katika ukurasa wa 20, 21]

Ramani ya dunia ya Mercator, 1538

Ona neno “AMERI CAE” katika mabara yote mawili ya Amerika

[Picha katika ukurasa wa 19]

Antwerpen, Stedelijk Prentenkabinet

[Picha katika ukurasa wa 20]

Both maps: From the American Geographical Society Library, University of Wisconsin-Milwaukee Libraries