Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Uchunguzi wa kina kuhusu jamii za marijani zinazotengeneza matumbawe ulionyesha kwamba asilimia 32.8 ya jamii hizo “zinakabili hatari kubwa ya kutoweka” kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa au utendaji wa wanadamu.—SCIENCE, MAREKANI.
▪ Kati ya watoto 2,000 hivi walio na ma- tatizo ya kupumua waliochunguzwa katika kliniki ya watoto kwenye hospitali moja huko Athens, Ugiriki, “iligunduliwa kwamba asilimia 65 hivi walikuwa wameathiriwa na moshi wa sigara kutoka kwa mzazi mmoja au wote wawili.”—KATHIMERINI—TOLEO LA KIINGEREZA, UGIRIKI.
▪ “Kuongezeka kwa bei ya mafuta, kuongezeka kwa gharama za maisha, . . . tisho la kuporomoka kwa uchumi . . . , na misiba ya asili inayotokea mara nyingi inaonyesha kwamba uwezo wetu una mipaka: ni wazi kwamba hatuna suluhisho la muda mfupi au la kudumu la matatizo hayo makubwa.”—LLUÍS MARIA DE PUIG, MSIMAMIZI WA BARAZA LA BUNGE LA ULAYA.
▪ Iligunduliwa kwamba asilimia 17 ya wavulana na asilimia 18 ya wasichana nchini Poland wametumia dawa za kulevya kufikia wakati wanapokuwa na umri wa miaka 15.—ŻYCIE WARSZAWY, POLAND.
Pambano Kati ya Simba na Wanadamu
Kadiri idadi ya watu barani Afrika inavyozidi kuongezeka, mazingira ya wanyama-mwitu yanapungua, na kusababisha “mashambulizi ya mara kwa mara,” linasema jarida Africa Geographic la Cape Town. “Inaonekana kwamba [simba hasa] wanawawinda wanadamu.” Kwa mfano, nchini Tanzania, simba wamewaua angalau watu 70 kila mwaka tangu 1990. Jarida hilo linasema kwamba katika visa fulani makundi ya simba “yamevamia wanadamu, yakiwakamata mbele ya nyumba zao za nyasi na kung’oa paa zilizoezekwa kwa nyasi na kuta za matope.”
Maghala ya Kale ya Wamisri Yafukuliwa
Wachimbuaji wa vitu vya kale wa Chuo Kikuu cha Chicago waliokuwa wakifanya kazi kusini mwa Misri wamefukua maghala saba ya nafaka, ambayo ndiyo makubwa zaidi kuwahi kufukuliwa katika nchi hiyo. Vitu vilivyochimbuliwa karibu na mahali hapo viliwawezesha wachimbuaji hao kukadiria kwamba maghala hayo yalijengwa kati ya mwaka wa 1630 na 1520 K.W.K. Ikiwa tarehe hizo ni sahihi, basi maghala hayo yalikuwepo siku za Musa. Maghala hayo ya mviringo yaliyojengwa kwa matofali, yaliyo na kipenyo cha mita 5.5 hadi 6.5 na kimo cha mita 7.5 hivi, yalikuwa vituo vya serikali vya kugawanya chakula. Ripoti hiyo ya chuo kikuu ilisema kwamba vituo hivyo “vilitumiwa na serikali kama maeneo ya kukusanya na kugawa vyakula vilivyokuzwa kwenye bonde la Mto Nile. Nafaka zilitumiwa kama pesa na hivyo kuwapa mafarao nguvu.” Ripoti hiyo iliendelea kusema kwamba “kwa sababu nafaka zilitumika kama pesa, maghala hayo yalitumika kama benki na pia hifadhi za chakula.”
Karatasi Ngumu Kama Chuma
Watafiti katika Taasisi ya Tekinolojia ya Royal huko Sweden wamebuni njia ya kutokeza karatasi kutokana na sukari ya mbao ambayo hudumisha ugumu wa nyuzinyuzi zake. Njia ya kawaida ya kutokeza karatasi kutoka kwa unga wa mbao huharibu nyuzinyuzi hizo na kuzifanya zisiwe na nguvu. Lakini watafiti hao kutoka Sweden walifaulu kutenganisha unga wa mbao kwa kutumia vimeng’enya na kisha wakatenganisha nyuzinyuzi hizo kwa kutumia maji. Maji yanapoondolewa kwenye nyuzinyuzi hizo, zinashikamana na kutokeza karatasi zinazoweza kutanuka kuliko kiunzi cha chuma na feleji.