Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Mnamo 2007, China ilikuwa na “watu 106 waliokuwa na dola zaidi ya bilioni moja ikilinganishwa na watu 15 [katika mwaka wa 2006] na hakukuwa na yeyote katika mwaka wa 2002.”—CHINA DAILY, CHINA.
▪ “Wahindi wanaowapuuza wazazi wao wanaozeeka wanaweza kufungwa chini ya sheria mpya inayoonyesha mahangaiko kwamba maendeleo ya haraka . . . yanafanya watu wasahau utamaduni ambao umekuwapo kwa karne nyingi wa kuwatunza watu wa familia.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, INDIA.
▪ “Leo, nchini Uingereza idadi ya Waislamu na Waanglikana inalingana.”—THE ECONOMIST, BRITAIN.
Miti ya Siberia “Inachimba” Madini
Katika misitu ya Siberia “unaweza kupata dhahabu kwenye visiki vinavyooza vya miti,” linaripoti gazeti la Urusi Vokrug Sveta. Wanasayansi kutoka Ulan-Ude, Irkutsk, na Novosibirsk wametambua kwamba miti ya kijani kibichi inayokua juu ya maeneo ya madini mengi huko Siberia hufyonza madini yaliyoyeyuka kutoka kwenye udongo wakati wote wa mwaka. Miti hiyo inapokufa na kuoza, madini hayo yanapatikana kwenye mabaki ya miti. Kutoka kwa mabaki ya tani moja ya miti hiyo iliyooza, wanasayansi Wasiberia walipata gramu tano za platinamu, karibu miligramu 200 za dhahabu, na kilo tatu za fedha.
Huduma ya Kwanza Kwenye Mazishi
Wachimba-kaburi wamepewa kifaa cha kufanya moyo upige tena katika makaburi fulani huko Australia. Kwa kusudi gani? Ili kuwafanya waombolezaji wenye huzuni wanaopata mshtuko wa moyo waamke na kuanza kupumua tena, linaripoti gazeti la Sydney Sun-Herald. “Mazishi ni maeneo hatari kwa watu kupata mshtuko wa moyo,” anaeleza Sisenanda Santos, msemaji wa huduma za St. John Ambulance, ambayo inasimamia mipango hiyo. “Watu wako katika vikundi vikubwa, wana huzuni, na mara nyingi wamevaa nguo nyingi kupita kiasi katika siku zenye joto.” Kifaa hicho kina maagizo yaliyorekodiwa ya kumwongoza mtu anayekitumia na kinatoa umeme unaofanya moyo wa mtu upige ikiwa kitatambua dalili zozote za mshtuko wa moyo.
Talaka Zinadhuru Mazingira
Idadi inayoongezeka ya talaka ulimwenguni pote inadhuru mazingira kwa sababu inafanya watu watumie vitu zaidi. Watu wanapotalikiana wanakuwa na nyumba nyingi zaidi, kunakuwa na watu wachache zaidi wanaoishi katika nyumba, na kila mtu anatumia vitu vingi zaidi, unasema uchunguzi uliochapishwa katika jarida Proceedings of the National Academy of Sciences. “Mnamo 2005 pekee watu waliotalikiana nchini [Marekani] hawangetumia vyumba zaidi ya milioni 38, umeme kwa saa bilioni 73, na lita trilioni 2.4 hivi za maji ikiwa wangetumia kiasi kinacholingana na kile cha watu waliooana.” Katika 2000, kulikuwa na familia milioni 6.1 kama hizo ‘zisizotumia mali vizuri’ nchini Marekani.
Biblia Ndogo Zaidi Kuwahi Kuchapishwa
Wanasayansi Waisraeli wa tekinolojia ya nano wamefaulu kuchapisha “Agano la Kale” lote katika Kiebrania kwenye kipande cha silikoni “kidogo kuliko kichwa cha pini,” kinaripoti chanzo cha habari cha Intaneti Science Daily. Jambo hilo liliwezekana kwa kuelekeza vipande vidogo sana vya gallium ili kuyaandika maandishi hayo kwenye sehemu iliyofunikwa na dhahabu. “Mradi wa kutengeneza Biblia ya nano unaonyesha uwezo wetu wa kupunguza ukubwa,” anaeleza profesa Uri Sivan wa Taasisi ya Tekinolojia ya Technion-Israeli. Hilo linafungua njia ya “kuhifadhi habari nyingi kwenye sehemu ndogo.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]
AP Photo/Ariel Schalit