Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Baikal—Ziwa Kubwa Zaidi Ulimwenguni

Baikal—Ziwa Kubwa Zaidi Ulimwenguni

Baikal—Ziwa Kubwa Zaidi Ulimwenguni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI URUSI

TANGU zamani, makabila ya Wamongolia katika eneo la mbali ambalo leo linaitwa Siberia kusini yamelistahi sana ziwa hilo. Ingawa maziwa mengine ni mapana na marefu zaidi, ziwa hilo la maji baridi ndilo lenye kina kirefu zaidi ulimwenguni na lina maji mengi zaidi. Jina moja ambalo limetumiwa kwa muda mrefu zaidi ni Baikal, linalodhaniwa kumaanisha “Ziwa Tajiri” au “Bahari.” Kwa kweli, kwa sababu ziwa hilo ni “kubwa sana na huvukizwa kwa urahisi” mara nyingine mabaharia kandokando ya ziwa hilo huzungumzia kuhusu “kwenda baharini.”

Warusi wanajivunia sana Ziwa Baikal. Mwanasayansi mmoja huko Moscow aliliita “muziki mtamu ambao kila mtu alijifunza alipokuwa mtoto.” Kama tu muziki mtamu, ziwa hilo lina mambo mengi yenye kupendeza kama vile fuo maridadi sana, maji safi kabisa, na wanyama mbalimbali wasio wa kawaida ambao hawapatikani mahali pengine popote.

Kutoka angani, Ziwa Baikal ambalo lina urefu wa kilomita 636 na upana wa kilomita 80 huonekana kama jicho la bluu lililofunguliwa nusu. Asilimia 20 ya maji yote baridi duniani yako katika ziwa hilo. Hayo ni maji mengi zaidi kuliko yale yanayopatikana kwenye yale Maziwa matano Makubwa ya Amerika Kaskazini yakiwa pamoja! Ziwa Baikal lina kina cha zaidi ya mita 1,600. Ikiwa lingekaushwa ghafula, ingechukua mwaka mzima kwa mito yote ulimwenguni kulijaza tena!

Mgongano wa Mabara

Wataalamu wa kuchunguza mawe husema kwamba zamani, bara lililokuwa likisonga kuelekea upande wa kaskazini liligongana na bara la Asia. Mgongano huo ulikunja-kunja sehemu kubwa za miamba kana kwamba zilikuwa karatasi ngumu na kuzisukuma kwenye ardhi na kufanyiza milima ya Himalaya. Watu fulani wanaamini kwamba mgongano huo wa mabara hayo ulitokeza mabonde makubwa huko Siberia. Moja kati ya hayo linaitwa Bonde la Baikal. Baada ya muda, mchanga-tope kutoka kwenye milima inayozunguka ulimwagika katika bonde hilo kufikia kimo cha kilomita saba. Kisha maji yakajazia sehemu iliyobaki ya bonde hilo na kufanyiza Ziwa Baikal. Sasa, zaidi ya mito na vijito 300 humwaga maji yake kwenye ziwa hilo, lakini ni Mto Angara tu unaotoa maji.

Tofauti na maziwa mengi ya zamani, Ziwa Baikal halijajaa mchanga-tope au kugeuka kuwa kinamasi. Wanasayansi wanaamini hilo linasababishwa na miamba mikuu iliyo chini ya ziwa hilo ambayo bado inasonga na kupanua bonde hilo. Hivyo, badala ya kujaa kadiri muda unavyopita, kina cha ziwa hilo kinazidi kuongezeka mwaka baada ya mwaka! Miamba hiyo pia husababisha chemchemi za maji moto zitokee kwenye sakafu ya ziwa hilo.

Kuna Nini Ndani ya Ziwa Baikal?

Watu fulani huogopa kusafiri kuvuka Ziwa Baikal kwa mashua kwa kuwa unaweza kuona ndani kufikia kina cha mita 50 hivi kwani maji ni safi sana kana kwamba unatazama hewani! Jamii ya krasteshia wadogo wanaoitwa epischura huchuja na kuondoa mwani na bakteria ambazo huwa katika maziwa mengi. Kambamto huwasaidia katika kusafisha ziwa hilo kwa kula takataka ambazo zingeozea humo. Hivyo, maji hayo ni safi sana hivi kwamba miaka 20 hivi iliyopita maji ya ziwa hilo yaliyochunguzwa katika maabara yalichafuliwa na kontena ya glasi iliyoyabeba!

Mbali na maji yake yanayojulikana kuwa safi, maji ya Ziwa Baikal yana oksijeni nyingi sana isivyo kawaida. Maji ya maziwa mengine yenye kina kirefu, hayana oksijeni yanapofikia kina fulani na hivyo kufanya viumbe wa majini waishi sehemu zisizo na kina kirefu. Lakini katika Ziwa Baikal, mikondo kutoka upande wa mashariki na upande wa kaskazini hubeba oksijeni hadi chini kabisa kwenye ziwa hilo na kuchanganya maji yake kabisa. Kwa sababu hiyo, hata sehemu za chini zaidi za ziwa zina viumbe wengi sana.

Kuna msitu wa mimea chini ya ziwa hilo lenye maji safi yaliyo baridi sana. Sifongo wa kijani walio na matawi kama matumbawe huwa makao ya viumbe wengi wadogo. Viumbe wengi wanaopenda joto hukusanyika karibu na chemchemi za maji moto za ziwa hilo. Kati ya jamii ya viumbe 2,000 wanaopatikana katika ziwa hilo, jamii 1,500 hazipatikani mahali pengine ulimwenguni.

Ziwa Baikal linajulikana kwa sababu ya omul, samaki mweupe wa aktiki mwenye ladha zuri anayependwa na wavuvi. Ziwa hilo lina viumbe wengine wa kiajabu-ajabu. Kuna aina fulani ya mnyoo ambao unaweza kukua hadi kufikia sentimita 30, nao hula samaki. Hata kuna viumbe wenye chembe moja wanaoishi kati ya chembechembe za mchanga! Ziwa hilo linajulikana pia kwa sababu ya samaki anayeitwa golomyanka. Huenda huyo ndiye samaki asiye wa kawaida anayepatikana tu katika ziwa hilo.

Samaki huyo mdogo sana ambaye hupitisha mwanga ni mwenye kumeta-meta. Yeye huishi karibu na sakafu ya ziwa hili na huzaa. Asilimia 33 ya mwili wake ina mafuta na vitamini A kwa wingi. Anaweza kustahimili shinikizo la maji kufikia kina cha mita 200 hadi 450; hata hivyo, anapopigwa na jua, mwili wake huyeyuka na kubaki mifupa na mafuta. Golomyanka ni chakula kitamu cha mkazi maarufu wa Ziwa Baikal, yaani, nerpa, au sili wa Baikal. Huyo ndiye sili pekee anayeishi tu katika maji baridi.

Majira Yanayobadilika

Kwa miezi mitano hivi, Ziwa Baikal huwa limefunikwa na barafu. Kufikia mwishoni mwa Januari (Mwezi wa 1), barafu huwa na kina cha mita moja au zaidi. Barafu hiyo huwa na mistari kama ya michoro fulani nayo hung’aa inapopigwa na jua kama vioo vya madirisha. Barafu hiyo huonekana nyembamba kwani ni safi sana hivi kwamba watu wanaotembea juu yake wanaweza kuona miamba iliyo kwenye sakafu ya ziwa. Kwa kawaida, barafu hiyo huwa imara sana. Karne moja iliyopita, wakati wa majira ya baridi kali kulipokuwa na vita kati ya Warusi na Wajapani, jeshi la Warusi lilijenga reli kwenye barafu hiyo na kupitisha mabehewa 65 juu yake!

Kuanzia mwishoni mwa Aprili (Mwezi wa 4) hadi Juni (Mwezi wa 6), barafu hiyo hupasuka kwa kishindo kikubwa. Sauti hiyo kutoka kwenye ziwa, hutokeza “muziki wa barafu” unaojulikana sana na wenyeji. Mtaalamu wa mambo ya asili, Gerald Durrell, aliandika kwamba barafu hiyo “hutokeza sauti kama ya zeze ndogo [na] kutoa sauti kama ya paka wengi kwenye kikapu.” Punde si punde, hali ya hewa inapoanza kuwa na joto, upepo na mawimbi hutupa marundo ya barafu inayong’aa kwenye fuo.

Kadiri barafu inavyoyeyuka, ndivyo ndege wanavyoanza kurudi. Baadhi ya ndege wa Ziwa Baikal, kama vile ndege mpiga-mbizi, hukaa kwenye mdomo wa Mto Angara wakati wa majira ya baridi kali kwa kuwa sehemu hiyo haigandi. Kunapoanza kuwa na joto, ndege hao hukutana na ndege wengine wa majini kama vile bata, bata-bukini, bata-makelele, na korongo.

Watalii wanaotembelea ziwa hilo mwezi wa Juni huona dubu na watoto wao wakitembea kando ya maji wakila viluwiluwi vya inzi ambao huanguliwa kwa wingi juu ya miamba. Dubu hao hufurahia kula wadudu hao bila kujali kelele za inzi wanaowazunguka. Wanyama na ndege wengi huja kwenye ufuo wanapoona dubu hao wamekusanyika ili kula wadudu hao.

Kufikia msimu wa kiangazi, mwani huchipuka kwa wingi katika ziwa hilo na kutokeza chakula kwa ajili ya krasteshia wadogo na kufanya maji yawe na rangi ya kijani. Lakini kwa kawaida, unapokuwa kwenye fuo maji ya Ziwa Baikal huwa na rangi ya feruzi, na kwenye sehemu zenye kina kirefu maji yake yana rangi ya bluu nzito kama rangi ya bahari.

Fuo za ziwa hilo zina marundo ya mchanga na miamba mikubwa. Ghuba maridadi na rasi nyingi hutokeza mandhari nzuri ambayo mwandishi mmoja alisema inaonekana kama “mstari wa lulu zenye kung’aa,” ambayo hufanyiza mandhari yenye kubadilika-badilika ya maji na anga.

Mara nyingi ziwa hilo hupigwa na dhoruba baadaye katika mwaka. Upepo mkali hutokea wakati wa majira ya kupukutika kwa majani na nyakati nyingine unashuka juu ya ziwa hilo kwa nguvu kama ile ya kimbunga. Upepo huo unaweza kubadili maji matulivu ya ziwa hilo kuwa mawimbi yenye fujo yanayofikia kimo cha mita 4 hadi 6. Pia, inasemekana kwamba nyakati nyingine katika mwaka upepo umezamisha meli kubwa za abiria na mashua za kuvua.

Eneo Lenye Mandhari Mbalimbali

Hali mbaya ya hewa ya Siberia inaweza kufanya eneo la Ziwa Baikal lionekane kuwa sehemu kubwa, yenye upweke na baridi tu. Lakini kwa kweli, eneo hilo lina wanyama na mandhari mbalimbali zenye kuvutia. Safu nne za milima zinazozunguka ziwa hilo zina mbawala na pia mbuzi wa mlimani wa Siberia ambaye anakabili hatari ya kutoweka.

Kwenye nyanda za chini kuna nyika. Baadhi ya nyika hizo zinaweza kusemwa kuwa mashamba ya maua ya Siberia kwa kuwa zina maua mbalimbali ya pekee ya mwituni. Kati ya ndege wa pekee wanaopatikana katika nyika hizo ni korongo maridadi anayeitwa demoiselle na tandawala ambaye ndiye ndege mkubwa zaidi huko Asia.

Msitu muhimu sana kwa Ziwa Baikal ni ule wa taiga wenye miti ya misonobari. Ukubwa wa msitu huo unaozunguka ziwa hilo, ni mara mbili ya ukubwa wa msitu wa mvua wa Amazoni huko Brazili. Kama msitu huo, msitu wa taiga hutimiza fungu muhimu katika kudumisha mazingira na hali ya hewa ya ulimwengu. Jamii nyingi za ndege huishi humo kutia ndani capercaillie, aina fulani ya kwale wa Ulaya, mwenye mbwembwe nyingi na huimba wakati wa uchumba. Pia, bata-mdogo wa Baikal, anayeonyeshwa kwenye ukurasa wa 17, huja mara nyingi kwenye ziwa hilo.

Mnyama mmoja maarufu ni mbelele wa Barguzin. Idadi ya wanyama hao ambao wakati moja waliwindwa sana kwa sababu ya manyoya yao yenye kung’aa inaanza kuongezeka kwa sababu ya jitihada za wanamazingira. Jitihada za kuwalinda zilifanya Mbuga ya Kiasili ya Barguzin ianzishwe kwenye fuo za Ziwa Baikal mwaka wa 1916. Sasa kuna mbuga tatu za kiasili kwenye fuo za ziwa hilo, kutia ndani mbuga tatu za kitaifa kwa ajili ya umma.

Kutafakari Kina cha Hekima ya Uumbaji

Ziwa Baikal liko katika orodha ya UNESCO ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni na ni eneo linalopendwa sana na watalii. Kila mwaka, zaidi ya watalii 300,000 kutoka ulimwenguni pote hutembelea eneo hilo. Kitabu kimoja cha watalii kinasema kwamba “leo Baikal ni eneo lenye kuvutia kwa ajili ya watu wanaopenda mazingira na ni mahali pazuri pa kutalii. Kwa kuwa Baikal ina fuo maridadi, maeneo mazuri ya kutembea, ndege wenye kupendeza, na mahali pazuri pa kuendesha mashua, huenda itakuja kuwa sehemu bora zaidi ya kutalii barani Asia.”

Ziwa Baikal ni mahali panapofaa kutafakari kuhusu hekima ya hali ya juu ya Mungu na uzuri wa uumbaji wake. Ni nani mwingine isipokuwa Mungu ambaye angeweza kuumba ziwa maridadi kama hilo, likiwa na utendaji wake wa kiasili wa pekee unaotegemeza viumbe wengi walio ndani yake? Mtu akisimama kwenye fuo za Ziwa Baikal anaweza kurudia maneno ya mwandishi wa Biblia aliyesema hivi: “Lo! Jinsi kilivyo kina cha utajiri wa Mungu na hekima na ujuzi!”—Waroma 11:33.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

SILI PEKEE WA MAJI BARIDI ULIMWENGUNI

Ziwa Baikal ni makao ya makumi ya maelfu ya nerpa, au sili wa Baikal, ambao hula hasa samaki wa ziwa hilo. Hakuna anayejua jinsi nerpa hao walivyokuja kuwapo katikati ya Siberia na hawapatikani mahali pengine popote ulimwenguni. Sili wa jamii ya karibu zaidi ya nerpa anaishi umbali wa kilomita 3,220.

Kwenye uso wao bapa, nerpa wana macho makubwa sana yanayokaribiana, nao ndio sili wadogo zaidi ulimwenguni kwani wana urefu wa mita 1.4 hivi. Mara nyingi sili hao ambao si wakali huonekana wakiwa wamejianika juani kwenye miamba katika vikundi. Wao hawana tabia ya kawaida ya sili ya kuumana na kusukumana. Kwa kweli, huenda nerpa wakawa ndio sili watulivu zaidi duniani.

Wanabiolojia wanaochunguza sili wanasema kwamba nerpa “ni mtulivu zaidi kuliko sili wa Aktiki kwani [nerpa] anaweza kuguswa bila kuuma anaposhikwa kwenye nyavu ili afanyiwe uchunguzi wa kisayansi.” Ensaiklopidia moja inasema kwamba wapiga-mbizi fulani waliogelea na kuwafikia nerpa waliokuwa wamelala majini. Waliripoti kwamba hawakuamka hata walipoguswa au kugeuzwa.

[Hisani]

Dr. Konstantin Mikhailov/Naturfoto-Online

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

ENEO AMBALO WATU WALIHAMESHIWA

Kuanzia 1951 hadi 1965, wengi wa Mashahidi wa Yehova walipelekwa uhamishoni kwenye eneo la Ziwa Baikal kwa sababu walikataa kuvunja imani yao ya kidini. Mnamo 1951, Praskovya Volosyanko alipelekwa Olkhon, kisiwa kikubwa zaidi huko Baikal. Yeye pamoja na Mashahidi wengine waliokuwa uhamishoni walijiruzuku kwa kuvua samaki wakitumia nyavu. Hata hivyo, alitafuta njia za kushiriki katika aina nyingine ya “uvuvi” kwa kutumia Biblia yake kuwaambia wakazi wengi wa Olkhon habari njema ya Ufalme wa Mungu.

Mwaka wa 1953, Praskovya na Mashahidi wengine sita walitiwa nguvuni kwa sababu ya kazi yao ya kuhubiri, naye akahukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani. Baada ya kuachiliwa, alitumikia kwa uaminifu katika kutaniko la Usol’ye-Sibirskoye, katika eneo la Irkutsk, hadi alipokufa mnamo 2005. Sasa kuna makutaniko 30 hivi ya Mashahidi wa Yehova katika eneo la Baikal na katika jiji la Irkutsk lililo karibu.

[Picha katika ukurasa wa 15]

 

URUSI

Ziwa Baikal

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Ziwa Baikal na milima ya Sayan

[Hisani]

© Eric Baccega/age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 17]

Bata-mdogo wa Baikal

[Hisani]

Dr. Erhard Nerger/ Naturfoto-Online

[Picha katika ukurasa wa 15 zimeandaliwa na]

Dr. Konstantin Mikhailov/Naturfoto-Online

[Picha katika ukurasa wa 18 zimeandaliwa na]

© Eric Baccega/age fotostock; Boyd Norton/Evergreen Photo Alliance