1. Ni Sahihi Kihistoria
Sababu za Kuitegemea Biblia
1. Ni Sahihi Kihistoria
Ni vigumu kukiamini kitabu ambacho kina mambo yasiyo sahihi. Wazia ukisoma kitabu cha kisasa cha historia ambacho kinaonyesha kwamba Vita vya Pili vya Ulimwengu vilipiganwa katika miaka ya 1800 au kinachosema rais wa Marekani ni mfalme. Je, kasoro hizo hazingefanya ukitilie shaka kitabu hicho?
HAKUNA mtu ambaye amefaulu kupinga usahihi wa historia ya Biblia. Biblia hutaja watu na matukio halisi.
Watu. Kuhusu Pontio Pilato, yule gavana Mroma wa Yudea ambaye alimtoa Yesu ili atundikwe, wachambuzi wa Biblia walitia shaka ikiwa aliwahi kuishi. (Mathayo 27:1-26) Uthibitisho wa kwamba wakati fulani Pilato aliwahi kuwa mtawala wa Yudea ulipatikana katika jiwe [1] lililogunduliwa kwenye jiji la bandarini la Kaisaria katika Bahari ya Mediterania mnamo 1961.
Kabla ya mwaka wa 1993, hakukuwa na ushuhuda nje ya Biblia uliounga mkono maisha ya Daudi, yule mchungaji kijana mwenye ujasiri aliyekuja kuwa mfalme wa Israeli. Lakini mwaka huo, wachimbaji wa vitu vya kale walipata jiwe la volkano [2], katika eneo fulani upande wa kaskazini mwa Israeli linalofikiriwa kuwa la karne ya tisa K.W.K., na wataalamu wanasema lina maneno “Nyumba ya Daudi” na “mfalme wa Israeli.”
Matukio. Kwa muda mrefu hadi nyakati za hivi karibuni, wasomi wengi walishuku usahihi wa simulizi la Biblia la taifa la Edomu kupigana na Waisraeli nyakati za Daudi. (2 Samweli 8:13, 14) Walisema kwamba Edomu ilikuwa jamii ya wafugaji wakati huo na haikuwa na mpangilio wala nguvu za kutosha kuweza kuwatisha Waisraeli mpaka muda mrefu baadaye. Hata hivyo, uchimbuzi uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kwamba “Edomu ilikuwa jamii iliyo na nguvu na yenye mpangilio karne kadhaa mapema [tofauti na ilivyodhaniwa mapema], kama ilivyoonyeshwa katika Biblia,” inaeleza makala moja katika jarida Biblical Archaeology Review.
Vyeo vinavyofaa. Kulikuwa na watawala mbalimbali katika karne 16 ambazo Biblia iliandikwa. Nyakati zote Biblia hutumia cheo kinachofaa inapomtaja mtawala fulani. Kwa mfano, Biblia hutaja kwa usahihi inapomrejezea Herode Antipa kuwa “mtawala wa wilaya” na Galio kuwa “liwali.” (Luka 3:1; Matendo 18:12) Ezra 5:6 inamtaja Tatenai, gavana wa mkoa wa Uajemi “ng’ambo ya Mto,” yaani, Mto Efrati. Sarafu iliyotengenezwa katika karne ya nne K.W.K. ina maelezo kama hayo, ikimtambulisha gavana Mwajemi Mazeasi kuwa mtawala wa mkoa “Ng’ambo ya Mto.”
Usahihi hata katika mambo madogo haupaswi kupuuzwa. Ikiwa tunaweza kuwaamini waandikaji wa Biblia hata katika mambo madogo, je, hilo halipaswi kuongeza uhakika wetu katika mambo mengine ambayo waliandika?
[Picha katika ukurasa wa 5]
1: Photograph © Israel Museum, Jerusalem; courtesy of Israel Antiquities Authority; 2: HUC, Tel Dan Excavations; photo: Zeev Radovan