Maajabu ya Hekima ya Kisilika
Maajabu ya Hekima ya Kisilika
“Kuhama [kwa ndege] ni kati ya mambo ya asili yenye kustaajabisha zaidi.”—COLLINS ATLAS OF BIRD MIGRATION.
DESEMBA 9, 1967 (9/12/1967) rubani mmoja aliona ndege 30 aina ya bata-maji wakiruka mita 8,200 juu ya usawa wa bahari kuelekea Ireland. Kwa nini walikuwa wakiruka juu hivyo ambako hali ya joto ni Selsiasi 40 chini ya sufuri? Zaidi ya kuepuka dhoruba za barafu zilizokuwa katika maeneo ya chini, ndege hao walikuwa wakibebwa kwa upepo uliowasaidia waruke kwa mwendo wa kilomita 200 kwa saa. Inakadiriwa kwamba ndege hao walisafiri umbali wa kilomita 1,300 kutoka Iceland hadi Ireland kwa muda wa saa saba tu.
Ndege ambaye huhamia maeneo ya mbali zaidi ni membe wa aktiki ambaye hutaga kwenye Mzingo wa Aktiki na wakati wa majira ya baridi kali, yeye huhamia maeneo ya Antaktiki. Kwa mwaka mmoja, ndege huyo mdogo husafiri kati ya kilomita 40,000 na 50,000, umbali unaolingana na kuizunguka dunia!
Korongo weupe huzaliana Ulaya Kaskazini na kusafiri kuelekea Afrika Kusini wakati wa majira ya baridi kali, hiyo ikiwa safari ya kilomita 24,000. Maelfu ya ndege hao hupitia Israel wakati wa majira ya kupukutika kwa majani na majira ya kuchipua, wakati uliojulikana katika nyakati za Biblia.—Yeremia 8:7.
Ni nani aliyewapa uwezo huo wa kisilika? Miaka 3,500 hivi iliyopita, Mungu alimwuliza hivi mwanamume mwadilifu Ayubu: “Je, ni kwa sababu ya uelewaji wako kwamba kipanga hupaa juu, kwamba yeye hunyoosha mabawa yake kuuelekea upepo wa kusini? Au, je, ni kwa agizo lako kwamba tai huruka kuelekea juu na kwamba hujenga kiota chake huko juu?” Alipojibu, Ayubu alimsifu Mungu kwa uwezo wa ajabu wa ndege na wanyama wengine.—Ayubu 39:26, 27; 42:2.
Uwezo Unaozidi Silika
Wanadamu, ambao waliumbwa kwa njia ya kustaajabisha na Mungu, hawaongozwi hasa na silika. Badala yake, sisi ni viumbe wenye uwezo wa kujiamulia mambo kwani tuna dhamiri na uwezo wa kuwapenda watu. (Mwanzo 1:27; 1 Yohana 4:8) Kwa sababu ya kuwa na zawadi hizo zote, tunaweza kufanya maamuzi ya haki na yanayotegemea maadili ambayo nyakati nyingine huonyesha upendo mwingi na kujidhabihu.
Bila shaka, mtazamo na tabia ya mtu hutegemea hasa kanuni za maadili na za kiroho ambazo alifundishwa au hakufundishwa alipokuwa mchanga. Kwa sababu hiyo, watu wanaweza kuwa na maoni yanayotofautiana kuhusu lililo sawa na lililo kosa, kuhusu linalofaa na lisilofaa. Tofauti hizo zinaweza kutokeza kutoelewana, kutovumiliana na hata kuchukiana, hasa ikiwa mambo kama utamaduni, uzalendo, na dini yanahusika.
Ulimwengu ungekuwa bora zaidi ikiwa familia yote ya wanadamu ingefuata viwango vilevile ambavyo vinapatana na maadili na kanuni za Biblia, kama tu sote tunavyofuata sheria zilezile za kiasili zinazoongoza ulimwengu wote! Lakini je, kuna mtu yeyote aliye na uwezo na ujuzi wa kuweka viwango vya kufuatwa ulimwenguni pote? Ikiwa yupo, je, atafanya hivyo? Je, tayari amefanya hivyo? Maswali hayo yatajibiwa katika makala inayofuata.