Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Kulingana na uchunguzi mmoja, wanawake wanaojifungua kwa upasuaji, wana hatari mara tatu zaidi ya kufa kuliko wanawake wanaojifungua kwa njia ya kawaida.—OBSTETRICS AND GYNECOLOGY, MAREKANI.
▪ Mwanasayansi anayeitwa Stephen Hawking aliuliza swali hili kwenye Intaneti: “Katika ulimwengu uliojaa vurugu za kisiasa, kijamii na kimazingira, wanadamu wanaweza kuendelea kuishi kwa miaka mingine 100?” Mwezi mmoja baadaye alikiri: “Sina jibu. Ndiyo sababu niliuliza swali hilo ili watu walifikirie na kujua hatari tunazokabili.”—THE GUARDIAN, UINGEREZA.
▪ Kila mwaka kati ya watu milioni 14 na 19 wanaugua malaria katika nchi ya Tanzania yenye watu milioni 37. “Watu 100,000 hivi hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo nchini humo.”—THE GUARDIAN, TANZANIA.
Samaki Hutunza Maji
Majiji kadhaa ya Amerika Kaskazini yanatumia samaki aina ya bluegills, ambao hutambua kemikali katika mazingira yao ili kujua ubora wa maji ya kunywa. Ripoti moja ya Associated Press inasema kwamba “samaki hao huwekwa katika matanki ambayo mara kwa mara huongezwa maji kutoka kwenye mabomba ya baraza la jiji, na vifaa fulani hutumiwa usiku na mchana ili kutambua mabadiliko katika kupumua, katika mapigo ya moyo, na jinsi samaki hao wanavyoogelea maji yanapokuwa na sumu.” Ripoti hiyo inasema kwamba katika kisa kimoja huko New York City, “samaki hao waligundua petroli iliyokuwa inavuja saa mbili kabla ya vifaa vingine . . . vya kitaalamu,” na hivyo kuzuia sumu isiingie katika mfumo wa maji ya umma.
Viwango vya Nikotini Vyaongezwa
Ingawa kampeni za afya zimewahimiza watu kuacha kuvuta sigara, makampuni ya sigara “yamekuwa yakitumia ujanja ili kufanya iwe vigumu kwa watu kuacha kuvuta sigara” kwa kuongeza viwango vya nikotini kwa “asilimia 10 katika miaka sita iliyopita,” laripoti gazeti The New York Times. Uchunguzi mpya unaosemekana kuwa unaonyesha tabia halisi za wavutaji, umefunua kwamba makampuni ya sigara yanajaribu “kuwashawishi vijana walioanza kuvuta sigara karibuni na wavutaji wa muda mrefu waendelee kuvuta sigara.” Katika uchunguzi mbalimbali “iligunduliwa kwamba karibu aina zote [za sigara] zina kiwango kikubwa cha nikotini kinachoweza kumfanya mtu awe mraibu.”
Mkono Bandia Unaoongozwa na Ubongo
Mwanamume mmoja huko Marekani ambaye alikatwa mikono yote miwili kuanzia mabegani baada ya kuhusika katika aksidenti fulani, sasa anatumia mkono bandia unaoongozwa na ubongo. Anaweza kupanda ngazi, kupaka rangi akitumia brashi, na hata kuwakumbatia wajukuu wake. Kulingana na ripoti ya Cable News Network, “Mkono wake wa kushoto ni bandia na unaongozwa na ubongo. Anapotaka kukunja mkono, yeye hufikiria tu, kisha ujumbe unatumwa kupitia chembe za neva zilizoelekezwa kwenye mkono huo kupitia upasuaji.” Mikazo kutoka kwenye misuli ya mikono hutambua ujumbe unaotoka kwenye ubongo na kuupeleka kwenye kompyuta ndogo iliyo mkononi. Kompyuta hiyo hutendesha mashine zilizo kwenye mkono bandia na kufanya sehemu za mkono huo kuiga matendo fulani ya kiwiko na ya mkono wa kawaida.
Maelfu ya Viumbe Vyagunduliwa!
Kulingana na gazeti la Fenua Info la Tahiti, karibu viumbe 17,000 vinagunduliwa kila mwaka. Asilimia 75 hivi ya viumbe vilivyogunduliwa ni wadudu, pia waligundua wanyama 450 wenye uti wa mgongo, kutia ndani aina 250 za samaki na aina 20 hadi 30 za wanyama wanaonyonyesha. Asilimia 66 hivi ya wanyama wanaonyonyesha wanaogunduliwa ni wanyama wagugunaji na popo, na “kwa wastani” lasema gazeti hilo, “mnyama mmoja wa jamii ya sokwe anagunduliwa kila mwaka,” jambo ambalo linawashangaza wanasayansi. Orodha ya viumbe vinavyogunduliwa inatia ndani pia miti na mimea.