Kumweleza Binti Yako Kuhusu Hedhi
Kumweleza Binti Yako Kuhusu Hedhi
Wakati wa kubalehe huwa na mabadiliko mengi. Kwa wasichana wachanga, badiliko kubwa wakati huo huwa kuanza kupata hedhi.
KUPATA hedhi kunaweza kuwa wakati mgumu kwa wasichana wachanga, na mara nyingi wakati huo msichana huwa na hisia mbalimbali. Kama tu mabadiliko mengine wakati wa kubalehe, jambo hilo linaweza kutatanisha. Wasichana wengi huwa na woga na wasiwasi wanapopata hedhi kwa mara ya kwanza, hasa kwa sababu walipewa habari zisizo za kweli au hawakuelezwa chochote.
Wasichana ambao wameelezwa kimbele kuhusu hedhi huwa hawachanganyikiwi wanapopata hedhi kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kwamba wasichana wengi hawaelezwi kimbele. Uchunguzi mmoja uliohusisha wasichana kutoka nchi 23 ulionyesha kwamba karibu thuluthi moja ya wasichana hao walisema kuwa hawakuelezwa kimbele kuhusu hedhi. Wasichana hao hawakujua la kufanya walipoanza kupata hedhi.
Baadhi ya wale ambao walikabili hali ngumu zaidi ni wanawake ambao hawakuwa wameelimishwa kuhusu hedhi. Katika uchunguzi mmoja, wanawake walitumia maneno kama “woga,” “kushtuka,” “aibu,” na “wasiwasi,” kusimulia jinsi walivyohisi walipopata hedhi kwa mara ya kwanza.
Kwa kawaida, watu hushtuka wanapoona damu kwa kuwa mara nyingi kutokwa na damu huhusianishwa na uchungu au kuumia. Kwa hiyo, haishangazi kwamba wasichana wasipoelezwa vizuri au kutayarishwa kimbele kuhusu hedhi, maoni ya kitamaduni yasiyobadilika, hekaya, au kutojua kunaweza kuwafanya wahusianishe kimakosa hedhi na ugonjwa au jeraha au waone hedhi kuwa kitu cha kuaibikia.
Binti yako anahitaji kujua kwamba kupata hedhi ni jambo la kawaida linalowapata wasichana wote wenye afya nzuri. Ukiwa mzazi, unaweza kumsaidia binti yako asiwe na woga au wasiwasi. Utafanyaje hivyo?
Wazazi Wana Daraka Muhimu
Kuna vyanzo vingi vya habari kuhusu hedhi kama vile walimu, watu wanaotoa huduma za afya, vichapo, na hata filamu zenye kuelimisha. Wazazi wengi huona kwamba vyanzo hivyo vina habari muhimu kuhusu utendaji wa mwili wakati wa hedhi na jinsi ambavyo msichana anaweza kujitunza wakati huo. Hata hivyo, huenda wasichana wakawa na maswali na mahitaji ambayo vyanzo hivyo havizungumzii. Hata kama wanajua jambo la kufanya wanapopata hedhi, mara nyingi wasichana hawajui jinsi ya kukabiliana na hisia mbalimbali ambazo mtu huwa nazo wakati huo.
Nyanya, dada wakubwa, na hasa akina mama wanaweza kutoa habari za ziada na kuwategemeza wasichana wachanga kihisia. Mara nyingi, wasichana huona kwamba mama zao ndio wanaoweza kuwaeleza vizuri zaidi kuhusu hedhi.
Namna gani akina baba? Wasichana wengi huona aibu kuzungumza na baba zao kuhusu hedhi. Wengine hutaka baba awasaidie kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kuwategemeza na kuwaelewa, hali wengine hawataki ajihusishe hata kidogo.
Katika nchi nyingi, familia zenye baba wasio na wake zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni. * Kwa hiyo, akina baba wengi watahitaji kujifunza jinsi ya kuwaelimisha binti zao kuhusu hedhi. Akina baba hao watajitahidi kufahamu mambo ya msingi kuhusu hedhi na pia kuhusu mabadiliko mengine ya mwili na kihisia ambayo binti zao hupata. Huenda baba hao wakawaomba msaada na mashauri mama au dada zao.
Utaanza Mazungumzo Lini?
Katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani, Korea Kusini, na sehemu fulani za Ulaya Magharibi, wasichana huanza kupata hedhi wakiwa na wastani wa umri wa miaka 12 na 13, ingawa wanaweza kuanza kuipata mapema wakiwa na miaka 8 au wakiwa wamechelewa wakiwa na umri wa miaka 16 au 17. Katika sehemu fulani za Afrika na Asia, huenda wasichana wakaanza kupata hedhi wakiwa na umri mkubwa zaidi. Kwa mfano, huko Nigeria, kwa kawaida wasichana huanza kupata hedhi wakiwa na wastani wa umri wa miaka 15. Mambo kama vile, chembe za urithi, hali za kiuchumi, vyakula, mazoezi, na mwinuko juu ya usawa wa bahari, yanaweza kuathiri umri ambao msichana ataanza kupata hedhi.
Ni vizuri kumweleza binti yako kuhusu hedhi kabla hajaanza kupata hedhi. Kwa hiyo, mazungumzo kuhusu mabadiliko ya mwili na hedhi yanapaswa kuanza mapema, pengine binti yako akiwa na umri wa miaka minane hivi. Huenda ukahisi kwamba ni mapema mno, lakini ikiwa binti yako ana umri wa kati ya miaka
minane na miaka kumi, yaelekea kwamba tayari mwili wake umeanza kukomaa kwa ndani kwa sababu ya kuongezeka kwa homoni. Utaona mabadiliko mengine ya mwili yanayohusianishwa na kubalehe kama vile kuanza kukua kwa matiti na kuongezeka kwa nywele mwilini. Wasichana wengi hukua haraka kabla tu ya kuanza kupata hedhi.Jinsi ya Kuanzisha Mazungumzo
Mara nyingi wasichana ambao wanakaribia kupata hedhi hutaka sana kujua mambo yatakayowapata. Huenda ikawa wamesikia wasichana wengine wakizungumzia jambo hilo shuleni. Wana maswali, lakini wengi wao hawajui jinsi ya kuyauliza. Huenda wakaona aibu kuzungumzia jambo hilo.
Huenda wazazi wakahisi hivyo pia. Ingawa akina mama ndio hasa huwaeleza binti zao kuhusu hedhi, mara nyingi wao huhisi kuwa hawana habari za kutosha au hawajisikii huru kuzungumzia habari hiyo. Huenda ikawa unahisi hivyo. Kwa hiyo utaanzishaje mazungumzo kuhusu hedhi na binti yako?
Yaelekea wasichana ambao hawajafikia umri wa utineja wanaokaribia kupata hedhi wataelewa mambo rahisi na hususa kuhusu hedhi. Mambo hayo yanaweza kutia ndani mara ambazo atapata hedhi, muda ambao itachukua, au kiasi cha damu atakachopoteza. Hivyo, mwanzoni mwa mazungumzo yenu, ingefaa kuzungumzia mambo ambayo msichana atafanya mara aanzapo kupata hedhi. Pia, huenda ikakubidi kujibu maswali kama: Nitahisije? au Nitazamie nini?
Baadaye, huenda ukataka kuzungumzia zaidi utendaji wa mwili wakati wa hedhi. Mara nyingi, unaweza kupata vichapo vinavyozungumzia habari hiyo kutoka kwa wale wanaotoa huduma za afya au kutoka kwenye maktaba, au kwenye duka la vitabu. Vichapo hivyo vitakusaidia kueleza mambo kwa undani. Huenda wasichana fulani wakapendelea kujisomea vichapo hivyo na wengine wakataka msome pamoja.
Tafuta mahali patulivu. Anza mazungumzo kwa kumweleza kuhusu mabadiliko ambayo hutukia wakati wa kubalehe hadi anapokomaa kabisa. Huenda ukasema hivi: “Hivi karibuni utapatwa na jambo fulani la kawaida ambalo huwapata wasichana wote. Unajua ni nini?” Au mama anaweza kuanza mazungumzo kwa kutaja jambo lililompata. Anaweza kusema: “Nilipokuwa msichana kama wewe, nilianza kujiuliza mambo ambayo hutukia mtu anapopata hedhi. Mimi na rafiki zangu tulizungumzia
jambo hilo shuleni. Je, rafiki zako wameanza kuzungumzia jambo hilo?” Mwulize yale ambayo anajua kuhusu hedhi na rekebisha maoni yoyote yasiyofaa. Uwe tayari kuzungumza sana mwanzoni, kwa kuwa huenda binti yako asizungumze sana au hata anyamaze kabisa.Kwa kuwa wewe ni mwanamke, bila shaka ulikuwa na wasiwasi na woga kuhusu hedhi. Unaweza kutumia yale yaliyokupata unapozungumzia jambo hilo. Ulihitaji kujua nini? Ulitaka kujua nini? Ni habari gani zilizokusaidia? Jaribu kuwa na usawaziko unapoeleza mambo yanayofaa na yasiyopendeza kuhusu hedhi. Uwe tayari kuulizwa na kujibu maswali.
Elimu Inayoendelea
Kuwaelimisha wasichana kuhusu hedhi si jambo linalopaswa kufanywa mara moja tu, bali mafundisho hayo yanapaswa kuendelea. Si lazima ueleze kila kitu mara ya kwanza. Msichana anaweza kutatanika ukimweleza habari nyingi mara moja. Watoto hujifunza mambo hatua kwa hatua. Pia huenda ikafaa kurudia habari hiyo pindi mbalimbali. Wasichana wachanga huelewa habari zaidi kadiri wanavyokua.
Jambo lingine ni kwamba maoni ya msichana kuhusu hedhi hubadilika-badilika kadiri anavyobalehe. Mara binti yako anapozoea kupata hedhi, huenda akawa na mahangaiko na maswali mengine. Kwa hiyo, unahitaji kuendelea kumpa binti yako habari zaidi na kujibu maswali yake. Zingatia habari iliyo muhimu na inayomfaa zaidi binti yako ikitegemea umri na uwezo wake wa kufahamu mambo.
Kuchukua Hatua ya Kwanza
Lakini utafanya nini ikiwa binti yako anaonekana kwamba hapendezwi na habari hiyo? Huenda ikawa hataki kuzungumzia mambo ya kibinafsi. Au labda anahitaji muda ili ajihisi huru kuzungumzia habari hizo na kuuliza maswali. Pengine hata atasema kwamba tayari anajua kila kitu kuhusu habari hiyo.
Uchunguzi mmoja uliofanyiwa wasichana wenye umri wa miaka 11 hivi huko Marekani ulifunua kwamba wengi wa wasichana hao walidai kuwa wanajua mambo mengi kuhusu hedhi. Hata hivyo, walipohojiwa zaidi, iligunduliwa kwamba hawakuwa na habari kamili na tayari walikuwa wameamini hekaya na maoni ya kitamaduni yasiyobadilika kuhusu hedhi. Hivyo, hata binti yako akisema kwamba anajua kila kitu kuhusu hedhi, bado utahitaji kuzungumza naye kuhusu habari hiyo.
Huenda ikakubidi wewe ukiwa mzazi, kuanzisha mazungumzo mafupi kuhusu hedhi na kuyaendeleza. Kwa kweli, hilo ni daraka lako ukiwa mzazi. Iwe atakubali kwamba anahitaji msaada wako au la, binti yako anahitaji msaada wako. Huenda ukavunjika moyo na kuhisi kuwa hustahili, lakini usikate tamaa. Uwe na subira. Bila shaka baada ya muda, binti yako atathamini jitihada zako.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 12 Huko Japani, idadi ya familia zenye baba wasio na wake ilifikia kiwango cha juu kabisa mwaka wa 2003. Nchini Marekani, karibu familia 1 kati ya 6 zenye mzazi moja ni zile za baba wasio na wake.
[Blabu katika ukurasa wa 11]
Ni vizuri kumweleza binti yako kuhusu hedhi kabla hajapata hedhi kwa mara ya kwanza
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
JINSI YA KUZUNGUMZA NA BINTI YAKO KUHUSU HEDHI
❖ Mwulize habari ambazo tayari anajua. Rekebisha maoni mabaya. Hakikisha kwamba nyote wawili mna habari sahihi kuhusu hedhi.
❖ Simulia mambo yaliyokupata. Kwa kutafakari na kusimulia mambo yaliyokupata ulipoanza kupata hedhi, unaweza kumtegemeza binti yako kihisia.
❖ Mweleze jambo la kufanya. Kwa kawaida wasichana wachanga huuliza maswali kama: “Nitafanya nini nikipata hedhi nikiwa shuleni?” “Nitatumia vifaa gani?” “Nitavitumiaje?”
❖ Eleza habari sahihi kwa njia rahisi. Rahisisha habari ikitegemea umri na uwezo wa binti yako wa kufahamu mambo.
❖ Endeleza mazungumzo hayo. Anza kumwelimisha binti yako kabla hajaanza kupata hedhi, na endeleza mazungumzo hayo kukiwa na uhitaji hata baada ya yeye kupata hedhi.
[Picha katika ukurasa wa 12, 13]
Elewa hali. Huenda ikawa binti yako hataki kuzungumzia mambo ya kibinafsi