Jinsi Viumbe Hushirikiana
Jinsi Viumbe Hushirikiana
Ili viumbe “waendelee kuwa hai ni muhimu washirikiane kwa ukaribu na jirani zao sawa na ilivyo muhimu kukua na kuzaana.”—“Liaisons of Life.”
BAHARI ilikuwa imetulia tuli. Kulikuwa tu na kelele za ndege wengi wa baharini. Msisimko wao ulionyesha kwamba jambo fulani lilikuwa likiendelea chini ya bahari. Kwa ghafula, povu likatokea na kufanyiza mviringo mweupe. Muda mfupi baadaye, viumbe wawili wakubwa weusi wakatokea katika maji safi katikati ya mviringo huo. Viumbe hao walikuwa nyangumi wawili wenye nundu ambao waliibuka kutoka kwenye sehemu za chini za bahari wakiwa wamefungua midomo yao yenye kitu kama kichungi kilichofanyizwa kwa mifupa. Wakiwa juu ya bahari walifunga taya zao kubwa, wakarusha maji kupitia pua zao, na kuzama tena ili warudie tendo hilo.
Nyangumi hao wawili walikuwa wakishirikiana kukusanya na kula viumbe wengi wanaofanana na uduvi. Kana kwamba walikuwa wakicheza dansi chini ya maji, viumbe hao wenye uzito wa tani 40 walizama chini ya uduvi hao na kuogelea kwa mviringo huku wakirusha maji kwa pua zao. Mbinu hiyo ya ajabu ilifanyiza “wavu” wa povu kuwazunguka uduvi. Kisha nyangumi hao wakaingia katikati ya “wavu” huo kutokea chini na kuwala uduvi walionaswa.
Kwenye nyanda za Afrika, mara nyingi nyani na swalapala hushirikiana. Jarida Scientific American linasema “wanyama hao wawili hupiga
kelele za kuonyana kunapokuwa na hatari.” Uwezo mzuri wa swalapala wa kunusa na uwezo wa nyani wa kuona mbali, hufanya iwe vigumu kwa wanyama hao kushambuliwa ghafula. Pia mbuni wenye uwezo wa kuona mbali hushirikiana katika njia kama hiyo na pundamilia walio na uwezo mzuri sana wa kusikia.Hiyo ni baadhi tu ya mifano mingi ya ushirikiano kati ya viumbe wanaotuzunguka. Kwa kweli, ushirikiano unaonekana kati ya viumbe wa aina zote, iwe ni kati ya viumbe wadogo na wanadamu au kati ya viumbe wanaofanana na wasiofanana. Maelfu ya miaka iliyopita, Mfalme Sulemani, aliyekuwa akijifunza kuhusu mambo ya asili, aliwachunguza chungu. Aliandika hivi: “Mwendee chungu, ewe mvivu; zitazame njia zake upate kuwa na hekima. Ijapokuwa hana kiongozi, ofisa wala mtawala, yeye hutayarisha chakula chake wakati wa kiangazi; amekusanya akiba ya chakula chake wakati wa mavuno.”—Methali 6:6-8.
Chungu ni mfano mzuri wa viumbe wanaoshirikiana, wenye bidii, na wenye utaratibu, ambao mara nyingi hushirikiana kukokota vitu vikubwa zaidi kuliko wao. Chungu wengine hata huwasaidia wenzao walioumia au kuchoka kwa kuwabeba hadi kwenye makao yao. Kwa kufikiria tabia hizo, haishangazi kwamba Sulemani alitumia chungu kuwa mfano tunaopaswa kuiga.
Katika makala zinazofuata tutaona jinsi ushirikiano ulivyo muhimu katika ‘kitabu cha asili,’ na jinsi unavyoendeleza uhai, kutia ndani uhai wa wanadamu. Pia tutajifunza jinsi wanadamu wanavyoharibu dunia, kuichafua, na kuangamiza viumbe wake. Je, Muumba ataruhusu jambo hilo liendelee milele?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Juu: Nyani na swalapala hushirikiana kuonyana hatari inapotokea
[Picha katika ukurasa wa 4]
Chungu ni mfano mzuri wa ushirikiano
[Picha katika ukurasa wa 4]
Kuna ushirikiano kati ya mbuni walio na uwezo mzuri wa kuona na pundamilia walio na uwezo mzuri wa kusikia