Wakati Ujao wa Utalii
Wakati Ujao wa Utalii
“Kuna mifano kutoka karibu kila nchi ulimwenguni ambako miradi ya utalii imetajwa kuwa kisababishi kikuu cha kuharibiwa kwa mazingira.”—An Introduction to Tourism, cha Leonard J. Lickorish na Carson L. Jenkins.
MBALI na kuhatarisha mazingira, utalii unaweza kusababisha matatizo mengine pia. Na tuchunguze baadhi ya matatizo hayo. Baadaye, tutazungumzia jinsi tutakavyoweza kutalii dunia yetu maridadi na kujifunza kuhusu maajabu yake, hasa wakazi wake wazuri.
Matatizo ya Kimazingira
Idadi kubwa ya watalii leo imetokeza matatizo. Watafiti Lickorish na Jenkins, wanaandika hivi: “Huko India, kaburi la Taj Mahal linachakaa kwa sababu ya kutembelewa na wageni.” Kwa kuongezea, wanasema: “Pia huko Misri, piramidi zinaendelea kuharibika kwa sababu ya kutembelewa na wageni wengi sana.”
Isitoshe, waandishi hao wanaonya kwamba utalii usiodhibitiwa unaweza kuharibu au kuzuia ukuzi wa mimea wakati wageni wengi wanapokanyaga-kanyaga maeneo yaliyotengwa ili kuhifadhi maliasili. Kwa kuongezea, jamii za viumbe wanaweza kuhatarishwa watalii wanapokusanya vitu visivyopatikana kwa urahisi kama vile makombe ya baharini na marijani au wakati wenyeji wanapokusanya vitu hivyo ili kuwauzia watalii.
Watalii husababisha uchafuzi. Kulingana na makadirio ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, kila mtalii hutokeza wastani wa kilo moja ya takataka kila siku. Inaonekana kwamba hata maeneo ya mbali zaidi yanaathiriwa. Ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Mvua linasema: ‘Katika vijia vya Himalaya vinavyotumiwa sana na watalii, takataka zimetupwa kotekote na msitu huo wa milimani umeharibiwa na wageni ambao hutafuta kuni za kupasha moto chakula na maji ya kuoga.’
Isitoshe, mara nyingi watalii hutumia kiasi kikubwa cha mali ambacho kingetumiwa na wenyeji. Kwa mfano, James Mak anaandika hivi katika kitabu chake Tourism and the Economy: “Huko Grenada watalii hutumia mara saba kiasi cha maji ambacho wakazi wa huko hutumia.” Anaongeza hivi: “Asilimia 40 ya nishati inayotumiwa huko Hawaii hutumiwa katika utalii kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, ingawa kwa wastani ni mtu mmoja tu kati ya wanane ambaye ni mtalii.”
Ingawa watalii hutumia pesa nyingi kutembelea nchi zinazositawi, kiasi kikubwa cha pesa hizo hakiwafaidi wenyeji. Benki ya Dunia inakadiria kwamba asilimia 45 tu ya pesa zinazokusanywa kutokana na utalii ndizo zinazotumiwa na nchi iliyotembelewa, kiasi kikubwa cha pesa hurudia mataifa yaliyositawi kupitia kampuni za kigeni za kupanga safari za watalii na hoteli zinazomilikiwa na wageni.
Athari za Kijamii
Watalii walio na utajiri wa kiasi kutoka nchi za Magharibi ambao hutembelea nchi zinazositawi wanaweza kutokeza athari zilizojificha na nyakati nyingine zinazoonekana waziwazi kwa utamaduni wa wenyeji. Kwa mfano, mara nyingi watalii huja na vitu vya anasa. Huenda wenyeji wasiwazie kamwe kuwa na vitu kama hivyo. Wenyeji wengi hutamani vitu hivyo ghali lakini hawawezi kuvigharimia bila kufanya mabadiliko makubwa maishani, mabadiliko ambayo huenda yakaathiri tabia za wenyeji.
Mak alitaja matatizo yanayoweza kutokea akisema kwamba kuongezeka kwa biashara ya utalii kunaweza “kufanya utamaduni na tabia za pekee za wenyeji zitoweke, kutokeza mizozo katika jamii za kitamaduni kuhusu jinsi mashamba ya jamii na maliasili inavyopaswa kutumiwa, na kueneza tabia zisizokubaliwa na jamii kama vile uhalifu na ukahaba.”
Mara nyingi leo watalii huhisi kwamba wako huru kufanya watakavyo, kwa hiyo wao hujihusisha na mambo ambayo hawangefanya ikiwa wangekuwa nyumbani pamoja na familia na marafiki wao. Hivyo, ukosefu wa maadili wa watalii umekuwa tatizo kubwa. Akitaja mfano unaojulikana sana, Mak alisema: “Ulimwenguni pote kuna wasiwasi kuhusu jinsi utalii unavyochangia kuongezeka kwa ukahaba wa watoto.” Mnamo 2004, shirika la habari la CNN liliripoti hivi: “‘Makadirio yanayotegemeka yanaonyesha kwamba watoto 16,000 hadi 20,000’ hutendewa vibaya kingono huko Mexico, ‘hasa mipakani, mijini, na katika maeneo ya watalii.’”
Manufaa ya Kusafiri
Dunia yetu ni makao yenye mambo mengi ya kupendeza kama vile machweo yenye rangi nyingi, nyota nyingi zenye kumeta-meta, na mimea na wanyama wa aina mbalimbali. Haidhuru mahali tunapoishi, sisi hufurahia mambo hayo kutia ndani maajabu mengine ya dunia yetu. Hata hivyo, ni jambo la kupendeza kama nini tunapopata nafasi ya kusafiri na kuona maajabu mengine ya dunia!
Hata hivyo, ingawa watalii wengi huvutiwa na mandhari za asili za dunia, wengi wao husema
kwamba jambo kuu katika safari zao huwa kufahamiana na watu walio na utamaduni tofauti. Mara nyingi, wasafiri hutambua kwamba maoni yasiyofaa kuhusu watu wa nchi nyingine si ya kweli. Kusafiri huwasaidia wawaelewe watu wa rangi na utamaduni mwingine na kusitawisha urafiki wenye kudumu.Watalii wengi hujifunza kwamba si vitu vya kimwili hasa huwafanya watu wawe na furaha. Jambo muhimu ni kuwa na uhusiano mzuri na wengine, yaani, kudumisha urafiki wa muda mrefu na kuanzisha urafiki na wengine. Simulizi fulani la Biblia linaeleza jinsi wasafiri wa karne ya kwanza waliovunjikiwa na meli huko Malta walivyonufaika na “fadhili za kibinadamu” zilizoonyeshwa na wenyeji wa huko “wenye kusema lugha ya kigeni.” (Matendo 28:1, 2) Kutembelea nchi na watu wengine leo kumewasaidia wengi kutambua kwamba kwa kweli sisi sote ni familia moja na tunaweza kuishi pamoja duniani kwa amani.
Sasa ni watu wachache tu wanaoweza kutembelea sehemu mbalimbali ulimwenguni. Lakini mambo yatakuwaje wakati ujao? Je, itawezekana kwa watu wengi, au hata wote kufanya hivyo?
Matarajio ya Wakati Ujao
Ukweli ni kwamba sisi sote tuna ukoo, sisi ni washiriki wa familia ya kibinadamu. Ni kweli kwamba wanadamu wa kwanza wawili walikufa sawa na vile Mungu alivyokuwa amewaonya ingetukia ikiwa wangekosa kumtii. (Mwanzo 1:28; 2:17; 3:19) Kwa hiyo, wazao wao wote, kutia ndani sisi sote leo huzeeka na kufa. (Waroma 5:12) Lakini Mungu anaahidi kuwa kusudi lake la awali kwamba dunia ikaliwe na watu wanaompenda litatimizwa. Neno lake linasema: “Mimi nimesema hilo . . . pia nitalitenda.”—Isaya 45:18; 46:11; 55:11.
Hebu wazia hilo! Biblia inaahidi kwamba chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu: “Waadilifu wenyewe wataimiliki dunia, nao watakaa milele juu yake.” (Zaburi 37:29; Mathayo 6:9, 10) Ikifafanua hali ya wakati ujao ya watu duniani, Biblia inasema hivi: “Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena.”—Ufunuo 21:3, 4.
Fikiri kuhusu jinsi itakavyowezekana kutembelea sehemu mbalimbali duniani na kufahamu maajabu yake, hasa watu wake wazuri. Wakati huo hakutakuwa na wasiwasi kuhusu usalama! Watu wote duniani watakuwa marafiki wetu, kwa kweli, watakuwa kama Biblia inavyowaita ‘ushirika mzima wa ndugu ulimwenguni.’—1 Petro 5:9.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Jambo kuu la kusafiri linaweza kuwa kuanzisha urafiki na watu walio na utamaduni tofauti
Wakati ujao kutakuwa na matarajio mengi ya kutembelea watu na maeneo mbalimbali