Vitu vya Kuchezea vya Zamani na vya Sasa
Vitu vya Kuchezea vya Zamani na vya Sasa
PHILIP * na watoto wenzake wanatazama kwa furaha jinsi mpira waliotengeneza kwa vipande vya kamba unavyodunda. Wanaanza kuupiga na kucheza kandanda. Mike anashangaa kuona jinsi gari lake dogo linavyojiendesha anapofinya kibonyezo alichoshika. Anaweza kuliendesha mbele na nyuma kwa urahisi. Nyumbani, Andrea na rafiki zake wadogo wanawavisha nguo na viatu wanasesere wao, huku wakizungumza jinsi watakavyovalia watakapokua.
Watoto hao wana jambo gani linalofanana? Wote wana vitu wanavyoweza kuchezea kwa saa nyingi. Nyakati nyingine kitu cha kuchezea kama vile dubu aliyetengenezwa kwa vitambaa, huwa kipenzi cha mtoto tangu utotoni. Huenda hata akapigwa picha na kuwekwa katika albamu ya familia. Vitu vya kuchezea vilianzaje? Kwa nini watoto huviona kuwa muhimu sana?
Historia ya Vitu vya Kuchezea
Ensaiklopedia moja inasema: “Vitu vya kuchezea na michezo kutoka utamaduni mbalimbali imekuwapo kwa muda mrefu. Vingine, kwa mfano kijiti ambacho mtoto huchezea kama farasi, ni vya kawaida tu, navyo vingine vimebuniwa kwa teknolojia ya hali ya juu.” Kwa hiyo kitu cha kuchezea ni kidude chochote kinachoweza kutumiwa
kwa ajili ya kujifurahisha na kucheza. Na kwa kuwa ni kawaida kwa wanadamu kutafuta jambo tofauti la kufanya, kuna uwezekano mkubwa kwamba vitu vya kuchezea vimekuwepo tangu mwanadamu alipoumbwa.Kwa mfano, wanasesere, au sehemu zao, zimepatikana katika nchi kama vile Babilonia na Misri za kale. Huenda wanasesere ndio vitu vya kuchezea vya kale zaidi. Mpira ni kitu kingine cha kuchezea cha zamani. Ingawa hakuna njia ya kujua mpira wa kwanza ulitumiwa lini, vidude vya mawe ambavyo hugongwa kwa kutumia mpira wa mawe katika mchezo wa kuviringisha tufe, vimepatikana katika kaburi la kale la mtoto fulani huko Misri.
Vitu vya kuchezea vinavyoitwa yo-yo vilivyotengenezwa kwa mawe vilitumiwa miaka zaidi ya 3,000 iliyopita huko Ugiriki na kuna uthibitisho kwamba vilitumiwa katika China ya kale. Karagosi na maumbo mbalimbali yaliyofanyizwa kutokana na pembe za tembo, ni baadhi ya vitu ambavyo watoto Waroma walitumia kuchezea. Pia wavulana Wagiriki na Waroma walikuwa na mikokoteni midogo ya kuchezea, jambo linaloonyesha kwamba magari ya kuchezea yamekuwako kwa miaka mingi. Jumba moja la makumbusho lina sanamu ya mnyama iliyotengenezwa kwa udongo ambayo ina magurudumu, na huenda ikawa ilitumiwa kuchezea katika utamaduni wa kale wa Mexico. Hakuna magurudumu mengine ambayo yamepatikana kuhusiana na utamaduni huo. Katika zama za kati, mipira ya mviringo au yenye umbo la yai ilitengenezwa kwa kutumia vibofu vya wanyama. Sawa na mipira ya leo, mipira hiyo ilipigwa au kubebwa hadi kwenye goli.
Baadaye huko Uingereza katika karne ya 18, mafumbo ya kuunganisha vipande vya kufanyiza picha yalibuniwa kwa makusudi ya elimu, nayo yalipendwa sana mwanzoni mwa karne ya 20. Pia penseli za rangi zilianza kuwa maarufu. Nchini Marekani pekee, kampuni moja imetengeneza penseli za rangi zaidi ya bilioni 100. Kama unavyoona, baadhi ya vitu vya kuchezea sasa vilikuwepo tangu zamani navyo vimechangia sehemu muhimu katika maisha ya watu.
Kwa Nini Ucheze na Uwe na Vitu vya Kuchezea?
“Ni jambo la kawaida kwa kila mtoto kucheza. Kucheza humpa mtoto nafasi nyingi za kujifunza na kukua kimwili, kiakili, na kijamii. Ikiwa kazi ya mtoto ni kucheza basi vifaa vya kazi yake ni vitu vya kuchezea, na vitu vya kuchezea vinavyofaa vinaweza kumsaidia afanye kazi yake vizuri.” Hivyo ndivyo mwongozo fulani wa serikali wa kuchagua vitu vya kuchezea vinavyofaa ulivyoeleza umuhimu wa vitu hivyo.
Bila shaka, sababu kuu inayofanya vitu vya kuchezea vipendwe ni kwamba inafurahisha kucheza navyo. Hata hivyo, vinatimiza sehemu muhimu katika ukuzi wa mtoto. Fikiria mifano ifuatayo: Mtoto anaposukuma mkokoteni mdogo, anaimarisha utendaji wa misuli yake. Anaporuka kamba, anaboresha ustadi wake wa kujisawazisha. Anaposimama kwa mguu mmoja ili kupiga mpira au anapoendesha baiskeli, anajifunza kujisawazisha. Na anapojenga kwa
kutumia vipande vya mbao au kuchora picha, anajifunza kusogeza viungo vyake kwa njia bora.Vipi akili ya mtoto? Uwezo wa lugha husitawishwa mtoto anapocheza akiimba, labda anaporuka kamba au anapocheza mchezo wa watoto wa kukimbizana na kugusana. Mtoto anapotumia matofali kujenga, anapofuata maagizo ya mchezo fulani, anapounganisha vipande vya fumbo vinavyofanyiza picha, anapoigiza hadithi, au anapocheza kwa kuvalia mavazi maalumu ya kuigiza, uwezo wake wa kufikiri na kubuni vitu huchochewa pia. Na ndivyo inavyokuwa anapocheza ala za muziki au anapofanya kazi za mikono.
Jambo jingine muhimu ni kwamba kucheza huwasaidia watoto wasitawishe stadi za kushughulika na wengine kama wanapounda kikundi cha kucheza mpira. Dakt. Bruce Duncan Perry anasema: “Mtoto huwaelewa watu wanaomzunguka na huenda akawa mwenye huruma na asijifikirie sana. Wanapocheza na wenzao, watoto hujifunza sheria zinazoongoza watu, kutia ndani njia za kujizuia na kuvumilia wanapotamauka wakiwa katika kikundi.”
Pia watoto hutumia vitu vya kuchezea ili kuiga yale wanayoona watu wazima wakifanya. Mwanafalsafa Mgiriki Aristotle alisema: “Ni jambo la asili kwa mwanadamu kuiga vitu tangu utotoni.” Naam, watoto wanapocheza wao huiga na kujifunza utendaji mwingi wa kila siku. Tunaweza kuwazia msichana mdogo akimbembeleza mwanasesere wake alale, kama tu atakavyofanya baadaye atakapokuwa na mtoto halisi. Au anaweza kutayarisha vyakula bandia kwa ajili ya rafiki zake wadogo. Vivyo hivyo, wavulana huendesha “magari” yao, huku wakinguruma kama gari, wakijitayarisha kuendesha gari halisi. Hata hivyo, kuna mambo unayopaswa kufikiria unapowachagulia
watoto wako vitu vya kuchezea. Kwa nini?Kuchagua Vitu vya Kuchezea
Gazeti The Daily Telegraph la London linasema: “Sasa vitu vya kuchezea huonyesha wazi kuwa jamii yetu ni yenye jeuri na isiyotii sheria.” Ingawa maneno hayo hayahusu vitu vyote vya kuchezea, makala moja katika gazeti la Mexico La Jornada inaonyesha kwamba ni jambo la kawaida kuona vitu vichache vya kuchezea ambavyo vimetumiwa kwa muda mrefu, na vitu vingi “vyenye maumbo ya kutisha . . . yanayoonekana kuwa ya kikatili.” Makala hiyo inamnukuu Patricia Ehrlich, ambaye ni mwalimu na mtafiti kwenye Chuo Kikuu cha Xochimilco Autonomous cha Mexico, akisema kwamba vitu vingi vya kuchezea vinavyouzwa hukazia maoni ya watu wengi ya kumiliki kwa kutumia jeuri, ukatili, mamlaka, ujitiisho, na woga.
Shirika la Kitaifa la Wanasaikolojia wa Shule huko Marekani linaunga mkono wazo la kwamba kutumia sana vitu vya kuchezea vinavyokazia sana jeuri “kunaweza kuathiri vibaya uwezo wa mtoto wa kujifunza na kukua na kusababisha madhara.” Uchunguzi unaonyesha kwamba michezo yenye jeuri ya video na kompyuta inaweza kumfanya mtoto awe mkatili na mhalifu. Kwa hiyo, kila mtu ambaye humtunza mtoto anapaswa kufikiria kwa makini anapochagua vitu vya kuchezea vinavyofaa.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 26.
Kwa sababu ya maendeleo ya teknolojia ya kisasa, kuna vitu vya kuchezea vya namna nyingi na vya hali ya juu. Lakini huenda wazazi wasiwe na pesa za kuvinunua, huenda watoto wakachoshwa navyo haraka, au huenda tu visiwafae watoto. Leanne, mama mwenye watoto watano asiye na mwenzi huko Australia anasema: “Wavulana wangu wakubwa huathiriwa na matangazo ya kibiashara na mara nyingi wao huniomba niwanunulie michezo ya kompyuta iliyo ghali. Hata hivyo, wao huonekana kuwa wenye furaha zaidi wanapocheza nyuma ya nyumba kwa kutumia gongo la bei rahisi na mpira. Nimeona kwamba vitu vya kawaida vya kuchezea ndivyo hudumu zaidi na huwafanya watoto wangu watumie uwezo wao wa kufikiri katika njia nyingi.”
Kwa Nini Usijitengenezee Vitu vya Kuchezea?
Ikiwa wewe ni mtoto na huwezi kununua kitu cha kuchezea cha kisasa bado unaweza kuwa mwenye furaha kwa kutumia ubunifu na uwezo wako wa kufikiri. Katika sehemu nyingi za ulimwengu, watoto wenzako hujitengenezea vitu vya kuchezea.
Ona picha zilizo kwenye makala hii. Je, watoto hao hawaonekani kuwa wenye furaha? Si rahisi sana kutengeneza baadhi ya “magari” hayo. Lazima uokote nyaya za zamani na uzikunje ifaavyo. Ili kutengeneza magurudumu, unahitaji kukata mpira au plastiki katika umbo la mviringo. Unaonaje gari-moshi hilo lililotengenezwa kwa chupa za soda na za maziwa? Au unalionaje lori lililotengenezwa kwa mbao? Hata unaweza kubebwa na magari hayo, kama vile skuta hiyo ya Afrika iliyotengenezewa nyumbani. Watoto hao wameona kwamba si lazima vitu vya kuchezea viwe ghali ili wajifurahishe. Na inafurahisha kuvitengeneza. Kwa nini usijaribu?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Majina yamebadilishwa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
Kitu kizuri cha kuchezea . . .
● Ni salama na kinafaa umri na uwezo wa mtoto
● Kimetengenezwa vizuri na kinadumu (watoto hupenda kubomoa vitu)
● Kinavutia na kumpendeza mtoto vya kutosha kunasa fikira zake
● Kinachochea uwezo wa mtoto wa kubuni na kufikiri
● Si ghali
● Hakina sumu
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]
Ili Kuepuka Madhara Yanayoletwa na Vitu vya Kuchezea . . .
● Weka vitu vya kuchezea vya watoto wakubwa mahali ambapo wale wadogo hawawezi kuvipata
● Soma vibandiko na maagizo yote ya usalama kwa uangalifu, ikiwezekana pamoja na mtoto wako
● Mfundishe mtoto na rafiki zake jinsi ya kutumia na kuweka vitu vya kuchezea
● Epuka vitu vya kuchezea vyenye kelele zinazoweza kudhuru
● Kagua vitu vya kuchezea mara kwa mara. Kitu cha kuchezea kilichoharibika kinapaswa kurekebishwa au kutupwa mara moja
● Vitu vya kuchezea vinavyoweza kuwa hatari kama vile vya kulenga shabaha, vyenye ncha kali, na vya stima vinapaswa kutumiwa tu na watoto wakubwa chini ya usimamizi wa watu wazima
● Vitu vya kuchezea vyenye sehemu ndogo zinazoweza kumezwa vinapaswa kuwekwa mbali na watoto wadogo
[Picha katika ukurasa wa 24]
Simba na nungunungu juu ya jukwaa la kukunjwa, milenia ya pili, K.W.K., Iran
[Hisani]
Lion and hedgehog: Erich Lessing/Art Resource, NY
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mwanasesere wa udongo, karibu 600 K.W.K., Italia
[Picha katika ukurasa wa 25]
Sehemu ya juu inayozunguka, karibu 480 K.W.K., Ugiriki ya kale
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mwanasesere wa gunzi la hindi, Amerika wakati wa Ukoloni
[Picha katika ukurasa wa 25]
Penseli za rangi, mapema miaka ya 1900, Marekani
[Picha katika ukurasa wa 26]
Watoto wenye vitu vya kuchezea vilivyotengenezewa nyumbani
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Clay doll: Erich Lessing/Art Resource, NY; top: Réunion des Musées Nationaux/ Art Resource, NY; corn husk doll: Art Resource, NY