Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Maoni Yasiyo Sahihi Kuhusu Kukua kwa Nywele
Makala moja ya afya na mazoezi katika gazeti The New York Times, inasema kwamba “kupunguza au kunyoa nywele hakuathiri ukuzi, aina, au wingi wa nywele.” Kwa muda mrefu, watu wamekuwa na maoni yasiyo sahihi kwamba nywele hukua haraka na kwa wingi inapopunguzwa au kunyolewa. Hata hivyo, uchunguzi ambao umefanywa tangu miaka ya 1920 umeonyesha kwamba “urefu, aina, na ugumu wa nywele yako hautegemei mara ambazo unanyoa bali unategemea chembe za urithi na kiasi cha homoni,” inasema makala hiyo. Kwa nini bado watu wanashikilia maoni hayo? Labda ni kwa sababu watu wengi huanza kunyoa wakiwa wachanga, kabla nywele hazijafikia urefu wake kamili na zina rangi hafifu. Mara nyingi, “nywele huwa nyeusi zaidi na ngumu kwenye shina, kwa hiyo, kukata ncha hufanya nywele zionekane kuwa ngumu,” linasema gazeti Times. “Huenda pia nywele zinazokua baada ya kunyolewa zikaonekana kwa urahisi kuliko nywele ambazo tayari ni ndefu.”
Jihadhari na Vitu vya Kuchezea Vyenye Kelele
“Vitu vya kuchezea vyenye kelele hudhuru masikio ya watoto,” linasema gazeti Toronto Star. Baada ya kuchunguza “vitu 40 vya kuchezea ambavyo vimetengenezewa watoto wenye umri unaopungua miaka mitatu,” kikundi cha wataalamu wa sauti wa Kanada waligundua kwamba “angalau vitu 25 vya kuchezea vilikuwa na kelele ya kutosha kuharibu masikio ya watoto,” linasema gazeti hilo. Simu ya mkononi ya kuchezea ndiyo iliyokuwa na kiasi kikubwa zaidi cha kelele cha desibeli 115. Kulingana na mtaalamu wa sauti, Richard Larocque, kiasi hicho cha kelele ni “cha chini kuliko kelele ya ndege ya jeti lakini ni cha juu sana kuliko disko nyingi.” Kiwango cha sasa kinachoruhusiwa na shirika la Afya la Kanada ni desibeli 100. Uchunguzi huo unadokeza kwamba “kukaa mahali penye kelele ya kiwango cha desibeli 87 kwa dakika 30 hukinga masikio,” inasema makala hiyo.
Kukabiliana na Magumu ya Mikutano
Gazeti The New York Times linaripoti kwamba kampuni nyingi zinaona uhitaji wa kufanya mikutano ya kampuni iwe mifupi na kuzungumzia mambo makuu tu na hata kufutilia mbali mikutano isiyo ya lazima. Kwa hiyo, ili kupunguza kupoteza wakati katika mikutano, wakurugenzi fulani wameamua kutumia mbinu kabambe kama vile saa ya kupima wakati, filimbi, na viti visivyostarehesha, na vilevile kuwafanya wahudhuriaji wasimame badala ya kuketi. Inaonekana si wakurugenzi hao tu walio na maoni hayo. Katika uchunguzi uliofanyiwa wafanyakazi zaidi ya 600, “mikutano inayochukua muda mrefu sana” ilitajwa kuwa mojawapo ya mambo makuu ambayo hupoteza wakati. Patti Hathaway, mwandishi wa kitabu ambacho hutoa mashauri ya kushughulikia hali mbalimbali kazini, anapendekeza kwamba wakurugenzi kwanza waangalie ajenda ili waamue kama kweli mkutano huo ni muhimu. Ikiwa kusudi la mkutano ni kusambaza tu habari, basi chunguza ikiwa habari hiyo inaweza kusambazwa kupitia barua-pepe.
Mimea Inayokuzwa Chini ya Ardhi
“Mgodi wenye unyevu ni mahali panapofaa sana kukuza miti. Hii ni kwa sababu kwanza, mgodi huwa na unyevu kila mara na kiwango cha joto kisichobadilika cha nyuzi 25 Selsiasi mwaka mzima,” linasema gazeti, Toronto Star. Tangu mwaka wa 1986, kampuni ya madini na vyuma ya Inco Limited, imekuwa ikikuza mimea chini ya ardhi kisiri. Kwenye mgodi wao wa Creighton karibu na Sudbury, Kanada, ambao una kina cha meta 1,400, kampuni hiyo imekuwa ikikuza miche 50,000 kila msimu. Matangi ya kuhifadhi maji yenye vidhibiti-wakati hunyunyizia miche lita 2,000 za maji na mbolea kila siku. Gazeti hilo linasema kwamba ili kuwe na nuru kama ya jua, balbu 30 zenye wati 1,000 “huwashwa saa 24 kwa siku katika juma la kwanza, kisha saa 18 na kuzimwa kwa saa 6 kwa majuma matatu, halafu huwashwa kwa saa 12 na kuzimwa kwa saa 12 kwa wakati uliobaki.” Msimu wa kupanda huanza mwishoni mwa Januari, na kufikia mwisho wa Mei, miche ya misonobari myekundu na ile inayoitwa jack pine huwa tayari kupandwa kwenye eneo lililo katika mgodi ulio karibu na hapo. Pia baadhi ya mti hiyo midogo hupewa wakazi wa huko.
Kutunza Bustani Hupunguza Athari za Kiharusi
Gazeti la Ujerumani Gießener Allgemeine, linaripoti kwamba “kutunza bustani huwapa watu uradhi mwingi sana maishani baada ya kupatwa na kiharusi.” Miezi sita baada ya wagonjwa 70 wa kiharusi kumaliza mazoezi, waliulizwa ni kazi zipi zilizowaletea uradhi. Walitaja kazi za nyumbani, kununua vitu, kupika, kusoma, kwenda matembezi, kuendesha gari, kufanya kazi zao, na tafrija mbalimbali. Lakini kazi ya kutunza bustani ndiyo iliyotajwa kuwa inaleta uradhi maishani. Brigitte Oberauer, daktari anayewasaidia wagonjwa kupata nafuu kwa kufanya kazi fulani anasema kwamba kutunza bustani “hufanya iwe rahisi kwa wagonjwa wa kiharusi kukazia fikira mambo fulani na kuendelea kufanya hivyo. Hufanya akili zao zitende na kuwaonyesha kwamba kuna mimea mipya inayokua na kwamba maisha yanaendelea. Jambo hilo ni muhimu baada ya kupatwa na ugonjwa mbaya.” Kufanya kazi nje pia kunaweza kuondoa uchovu wa kukaa ndani ya nyumba, kuwasaidia waweze kutembea, na kuwafanya wawe na usawaziko wanapotembea.
Kutakuwa na Tatizo Kubwa la Kuwatunza Wazee
Richard Jackson, mkurugenzi wa Global Aging Initiative huko Washington, D.C. anaonya hivi: “Msipoinua kiwango cha maisha sasa na kuanzisha mpango fulani wa kuwasaidia wazee, kufikia mwaka wa 2030 au 2040 kutatokea matatizo makubwa yanayotisha hali njema ya wanadamu.” Kulingana na toleo la kimataifa la gazeti The Miami Herald, kuna wazee wengi sana ulimwenguni kwa sababu ya watu kuishi muda mrefu na kutozaa sana. Kwa mfano, idadi ya wazee nchini Mexico inatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 5 hadi asilimia 20 kufikia mwaka wa 2050. Kuna ongezeko kubwa kama hilo la wazee katika mataifa mengi yanayoendelea kama vile China, ambako inatarajiwa kwamba kufikia katikati mwa karne hii, kutakuwa na wazee milioni 332. Makala hiyo ilisema kwamba sasa “muda uliobaki [wa kuandaa] huduma nyingi za kijamii” kwa ajili ya wazee ni mfupi.
Kutibu Watoto Nyumbani
Gazeti Folha Online linaripoti kwamba watu huko Brazili na nchi nyingine wamekuwa na zoea la kutumia dawa za watoto vibaya. Familia nyingi huweka dawa nyingi nyumbani mwao. Lakini “tofauti na maoni ya watu wengi, hata dawa zinazoweza kununuliwa bila idhini ya daktari zinaweza kudhuru afya ya mtoto kwa njia isiyoweza kurekebika zikitumiwa vibaya au isivyo lazima.” Na magonjwa mengi ya watoto kama vile kikohozi hupona bila dawa. Lúcia Ferro Bricks, daktari wa watoto kwenye Hospitali ya Taasisi ya Kliniki za Watoto huko São Paulo anasema hivi: “Tumezoea kutatua tatizo lolote kwa kutumia dawa.” Vitamini pia zinatumiwa vibaya, lakini mara nyingi kutumia tu chakula kinachofaa kungetosheleza mahitaji ya mtoto. Bricks anasema: “Wazazi wanaponiomba niwaandikie vitamini, mimi huwaambia wanunue matunda kadhaa na kumtengenezea mtoto maji ya matunda.”