Vipepeo Maridadi wa Tropiki
Vipepeo Maridadi wa Tropiki
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hispania
WATU wanapotembelea msitu wa mvua wa tropiki kwa mara ya kwanza wanaweza kukatishwa tamaa. Wao hutazamia kuona wanyama na ndege wa aina ya pekee, lakini wanyama wengi hutembea usiku, na ndege wengi hawawezi kuonekana katika msitu huo wenye matawi yaliyoshikana sana.
Kitabu The Mighty Rain Forest kinasema: “Kuna dalili nyingi kwamba kuna viumbe wengi humo kwani kuna kelele nyingi kila mahali.” Kitabu hicho kinaongezea kusema kwamba “ikiwa mtu hayuko tayari kutumia wakati mwingi akisubiri na kutafuta-tafuta, hataona mnyama yeyote isipokuwa vipepeo.” Jambo la kupendeza ni kwamba, vipepeo hao wa tropiki huwa na rangi nyangavu na maridadi ambayo hufanya mtu afurahie kutembelea msitu huo wa mvua.
Vipepeo wa eneo la tropiki ni wa kipekee kwa sababu ni wakubwa na wana rangi tofauti-tofauti. Rangi ya kijani ya msituni hufanya rangi ya buluu, nyekundu, na manjano ya vipepeo hao wanaorukaruka ionekane waziwazi. Katika maeneo ya Amerika Kusini unaweza kuona pia vipepeo wenye mabawa yanayopenyeza nuru, mbali na wale wenye rangi za kawaida. Vipepeo wa jamii nyingine wana rangi yenye kuvutia sana chini ya mabawa yao kuliko sehemu ya juu. Vipepeo wasio na rangi nyangavu wanaoitwa nondobundi wana madoadoa yanayofanana na macho ya bundi ambayo hufanya miili yao ing’ae. Lakini vipepeo fulani hawaonekani kwa urahisi na mtu anahitaji kuwa makini sana ili aweze kutambua kwamba kitu kinachoonekana kuwa jani lililokauka kwa kweli ni kipepeo.
Mara nyingi watu huvutiwa na ukubwa wa kipepeo wa tropiki. Vipepeo wengine ni wakubwa kuliko ndege wadogo nao hunyiririka tu kama ndege. Kuna jamii nyingi sana za vipepeo katika msitu huo. Eneo la tropiki la Malaysia lina jamii elfu moja hivi, na Peru ina jamii elfu nne hivi, hiyo ikiwa asilimia 20 ya vipepeo wote ulimwenguni.
Ingawa bawa la kipepeo huonekana kuwa na rangi za aina mbalimbali, kwa kweli kipepeo hana rangi hizo zote. Bawa hilo huwa na utando unaopenyeza nuru ambao una maelfu ya magamba madogo na kila gamba huwa na rangi moja tu. Hata hivyo, magamba ya rangi tofauti-tofauti huungana na kumfanya mtazamaji afikiri kwamba kuna rangi nyingine tofauti.
Unaweza kufikiri kwamba inafaa kuwatazama vipepeo hawa maridadi wakati wanaporuka juu ya maua, lakini huwezi kufanya hivyo katika msitu wa mvua. Maua mengi huchanua kwenye matawi yaliyo juu kabisa na yaliyoshikana na ingawa maua hayo huandaa chakula kwa ajili
ya vipepeo, mtu hawezi kuwaona vipepeo hao akiwa chini. Jambo la kufurahisha ni kwamba vipepeo wa kiume hushuka chini ili kutafuta chumvi. Inadhaniwa kwamba tendo la kujamiiana hupunguza madini muhimu mwilini nao hurudisha madini hayo kwa kufyonza unyevunyevu kutoka ardhini. Kwa hiyo, kijia chenye unyevunyevu au ukingo wa kijito kidogo kinaweza kuwa mahali panapofaa pa kuwatazama vipepeo wa msitu wa mvua.Huenda pia ukaona kikundi cha vipepeo wakiwa wametua mahali fulani pamoja. Vipepeo wa nchi zenye joto wana zoea la kutua mahali pamoja. Vipepeo fulani wanaweza kukuruhusu uwakaribie wanapoota jua la asubuhi juu ya jani fulani. Ingawa aina fulani ya vipepeo hawatui mahali popote, kuwatazama tu wanaporuka kunaweza kufanya ufurahie kutembelea msitu wa mvua.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
Vipepeo na Nondo Wengi Maridadi
Ingawa ni vigumu kusema ni kipepeo au ni nondo yupi aliye maridadi zaidi, jamii fulani huwa maridadi zaidi kuliko zote. *
Vipepeo wa jamii ya Swallowtail (Papilionidae)
Ni jamii kubwa ya vipepeo maridadi, wengi wao wana “mkia” mdogo katika mabawa yao ya nyuma. Wao huruka kwa kasi, na mara nyingi hula maua yaliyo kwenye misitu yenye matawi yaliyo juu kabisa na yaliyoshikana.
Vipepeo wa jamii ya Morpho (Morphidae)
Vipepeo hawa wanaopatikana tu Amerika Kusini na Kati, wana mabawa yenye rangi ya buluu inayometameta. Rangi yao hubadilika-badilika ikitegemea kupindika kwa mwangaza. Wanapopiga-piga mabawa yao polepole, rangi hiyo ya buluu hubadilika ikitegemea upande ambao nuru inatokea.
Vipepeo wa jamii ya bird-wing (Ornithoptera)
Vipepeo hao hutoka Kusini-Mashariki mwa Asia na Australia. Kama jina lao linavyodokeza, vipepeo hao wakubwa wana mabawa makubwa sana kuliko ndege wengi. Kwa sababu hawapatikani kwa urahisi nao ni maridadi sana, wao ni wenye thamani kwelikweli.
Nondo wa jamii ya Uraniid (Uraniidae)
Kwa kuwa wanasemwa kuwa wa jamii ya nondo wala si ya vipepeo, wadudu hao wenye kuvutia huruka mchana. Chrysiridia madagascariensis anayepatikana Madagaska, ambaye mabawa yake huonyesha rangi zote za upinde wa mvua anatajwa kuwa “mdudu maridadi zaidi ulimwenguni.”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 12 Vipepeo na nondo hufanyiza jamii ya Lepidoptera.
[Hisani]
Morpho: Zoo, Santillana del Mar, Cantabria, España; all others in box: Faunia, Madrid
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mabawa yanayopenyeza nuru ya kipepeo aina ya “Hypoleria oto”
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kipepeo anayeitwa “Hewitson’s” mwenye mlia wa buluu. Upande wa chini wa mabawa yake (kushoto) unavutia kama upande wa juu (juu)
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Kipepeo anayeitwa “goliath birdwing” (ukubwa halisi)
[Picha katika ukurasa wa 17]
Upande wa chini wa bawa la kipepeo anayeitwa nondobundi
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kipepeo anayeitwa “dry-leaf”
[Picha katika ukurasa wa 18]
Vipepeo wa tropiki wakifyonza unyevunyevu wenye chumvi kutoka ardhini
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Hypoleria oto: Zoo, Santillana del Mar, Cantabria, España; all other photos: Faunia, Madrid
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Dry-leaf and yellow butterflies: Zoo, Santillana del Mar, Cantabria, España; all other photos: Faunia, Madrid