Huonekana Kama Chakula Halisi!
Huonekana Kama Chakula Halisi!
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Japani
UNATAZAMA kitu kinachoonekana kama mlo mtamu. Hamu yako inachochewa na mdomo unajaa mate. Hata hivyo, kwa kushangaza “chakula” hiki hakinukii, hakina ladha, wala lishe. Hakiwezi kuoza wala hakihitaji kuwekwa ndani ya friji. Ni chakula gani hicho? Kwa Wajapani, hicho ni chakula cha plastiki. Chakula hicho hutengenezwa kwa plastiki ngumu na ni mfano wa chakula halisi kinachopatikana mikahawani. Kina ukubwa uleule, umbo, na rangi ya chakula halisi.
Vyakula mbalimbali hutengenezwa kwa plastiki. Hivi vinatia ndani vyakula vya asili vya Japani kama vile sushi, na vyakula vinavyopendwa katika nchi za Magharibi kama vile piza na spageti. Pia kuna mifano ya vinywaji, viamsha-hamu ya kula, na vyakula vitamu vinavyoandaliwa baada ya mlo mkuu. Kuna mifano chungu nzima. Kwa kweli, mtengenezaji mmoja wa vyakula hivyo, hutengeneza aina zaidi ya 10,000 za vyakula vya plastiki!
Chakula cha plastiki huonekana kuwa halisi. Chakula hicho hutengenezwa kwa ustadi sana
hivi kwamba mambo madogo-madogo kama vile miinuko midogo-midogo katika ngozi ya kuku aliyeokwa, mpangilio wa mbegu za tikitimaji, na jinsi jani la letusi linavyojipinda, huonekana wazi. Lakini vyakula vya plastiki vilikuwaje maarufu sana katika mikahawa ya Japani?Karibu mwisho wa karne ya 19, mikahawa fulani iliweka vyakula vya kigeni vya sampuli mbalimbali mahali ambapo Wajapani wangeweza kuviona. Wapita-njia wangeweza kuona vyakula hivyo bila kuingia ndani. Bila shaka, vyakula hivyo havikuwavutia tu watu, bali viliwavutia pia wanyama na nzi. Vyakula hivyo viliharibika kwa sababu ya joto na unyevunyevu, na iligharimu pesa nyingi kuvitengeneza kila siku.
Baadaye, nta iliyopakwa rangi ilichukua mahali pa chakula halisi. Lakini nta haikufaa kwa sababu iliharibika kulipokuwa na joto. Mwishowe, plastiki ngumu ikaanza kutumiwa badala ya nta. Sasa kulikuwa na kifaa cha kudumu ambacho kingeweza kustahimili joto na wakati huohuo kuwavutia wateja wanaofaa, yaani, watu! Lakini vyakula vya plastiki hutengenezwaje?
Kwanza, umbo la chakula hutengenezwa. Kwa mfano, kipande cha nyama hutiwa ndani ya chombo cha mraba, kisha silikoni humwagwa kwenye chombo hicho hadi ifunike nyama hiyo kabisa. Silikoni hiyo inapokauka, chombo hicho huinamishwa. Nyama hutolewa, na umbo la nyama linabaki. Plastiki yenye rangi humwagwa ndani ya umbo hilo na kuokwa katika joto la Selsiasi 82. Plastiki hiyo inapopoa, nyama hiyo ya plastiki hutolewa. Sasa inaweza kupakwa rangi.
Ili kutengeneza sandiwichi, sehemu zake zote, yaani, mkate, nyama, jibini, na letusi zinahitaji kutengenezwa zikiwa peke yake. Baada ya hapo, kama sandiwichi ya kawaida, vipande hivyo vitawekwa katikati ya vipande vya mkate kisha viunganishwe kwa gundi.
Kutengeneza chakula cha plastiki ni aina fulani ya sanaa. Katsuji Kaneyama ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka 23 hivi, anasema kwamba “jambo muhimu katika kutengeneza chakula cha plastiki ni kuchunguza chakula halisi. Watu huona chakula kuwa kitu cha kuliwa. Sisi huona chakula kuwa kitu cha kutengenezwa.”
Unapoangalia kwa makini bakuli la wali wa Japani ambao umetoka tu kupikwa, utaona ni kama kila punje husimama na ni tofauti na nyingine. Bakuli lote la wali “huumuka kutoka chini na kuinuka katikati,” aeleza Kaneyama. Ili kutokeza umbo hilo, lazima kila punje itengenezwe ikiwa peke yake. Kukusanya tu punje hakutoshi kwa sababu haziwezi kusimama wima. Badala yake, lazima punje ziunganishwe kwa gundi kwa makini ili zionekane kama wali halisi ulioumuka. Kuongeza madoido halisi hufanya chakula kiwavutie wale wanaokitazama kwa makini.
Mtu anahitaji kuwa na uzoefu wa miaka mingi ili atengeneze vyakula vya plastiki kwa ustadi. Huenda mwanafunzi akatumia miaka michache ya kwanza kujifunza mambo ya msingi, akianza na vyakula rahisi kama vile uyoga. Mtu anahitaji kujifunza kwa miaka kumi hivi ili aweze kutengeneza samaki wa plastiki akiwa na umbile na rangi ya samaki halisi aliyetoka tu kuvuliwa. Huenda ikachukua miaka 15 kabla ya mtu kuonwa kuwa stadi wa sanaa hiyo.
Ikiwa utapita karibu na mkahawa fulani nchini Japani na uone sampuli za vyakula vyenye kuvutia, fikiria kazi ngumu iliyofanywa ili kuvitengeneza. Huenda ukajiuliza ni chakula kipi kinachohitaji ustadi zaidi ili kukitengeneza—chakula halisi au cha plastiki!
[Sanduku katika ukurasa wa 27]
Chakula Kinachotumiwa Katika Sinema
Ukiona chakula katika sinema, kipindi cha televisheni, au katika matangazo ya biashara, kichunguze kwa makini. Huenda kisiwe halisi. Chris Oliver, wa Los Angeles, ambaye ni mtaalamu wa kupamba vyakula, anasema kwamba inafaa kutumia vyakula vya plastiki katika sinema kwani kupiga picha huchukua muda mrefu sana. Anasema hivi: “Inafaa zaidi kutumia vyakula hivyo, ingawa ni vya bei ghali kuliko vyakula halisi.” Kwa kuwa kamera zinazotumiwa hutoa mwangaza wenye joto jingi, vyakula vya plastiki vinafaa zaidi kuliko vyakula halisi.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Unaweza kutofautisha ni chakula kipi ambacho ni halisi?
Jibu: Chakula halisi ni kile ambacho mwanamke huyo ameshika kwa mkono wa kuume.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Bottom photos: Hachiman Town, Gujyo City, Gifu Prefecture, Japan