Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Donge la Chumvi

Donge la Chumvi

Donge la Chumvi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ZAMBIA

Wewe huwazia nini unapofikiri kuhusu chumvi? Labda wewe huwazia mwamba wa chumvi, chumvi ya baharini, au chumvi ya kawaida. Lakini je, umewahi kusikia kuhusu chumvi ya Cibwa kutoka wilaya ya Mpika katika Mkoa wa Kaskazini wa Zambia? Chumvi ya Cibwa ni ya pekee kwa kuwa inatokana na nyasi!

Wanakijiji wanaoishi karibu na kinamasi cha Cibwa hutoa chumvi kwa njia ya pekee kutokana na nyasi ndefu zinazokua karibu na Mto Lwitikila. Wao huvuna nyasi hizo kuanzia Agosti hadi Oktoba kabla ya msimu wa mvua kuanza. Mvua inapoanza, nyasi hizo hazitoi chumvi yoyote.

Nyasi hizo zinapokatwa na kukaushwa, huchomwa ili kuondoa takataka. Hata hivyo, chumvi hiyo haiteketei. Inabaki kwenye majivu. Majivu hayo hutiwa katika chombo fulani kama vile kibuyu, kisha hutiwa maji na kuchujwa polepole. Maji hayo huyeyusha chumvi hiyo na kuipitisha katika matundu madogo yaliyo chini ya kibuyu. Maji ya chumvi yaliyokusanywa huvukizwa.

Maji hayo huvukizwa kwa kuchemshwa katika chungu kwa muda wa saa sita kwa moto wa kuni. Maji mengine ya chumvi huongezwa yale ya kwanza yanapovukizwa. Mwishowe, chungu hicho hujaa umajimaji mzito wa chumvi. Chungu hicho hutumika kama chuma cha kukalibu. Chungu hicho kinapotolewa kwenye moto na kuvunjwa, donge la chumvi hubaki.

Wanakijiji wamekuwa wakitengeneza chumvi ya Cibwa kwa miaka mingi. Hakuna mtu anayejua mbinu hiyo ilianzishwa na nani. Hata hivyo, inashangaza kwamba ingawa watu hao wako mbali na maeneo yaliyoendelea, mbinu ileile ya kisasa inayotumiwa kutokeza chumvi ndiyo hutumiwa katika eneo hilo la mashambani la Zambia.

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kibuyu kikichuja maji

[Picha katika ukurasa wa 19]

Chumvi iliyosafishwa

[Picha katika ukurasa wa 19]

Chungu