Kuhifadhi Maji ya Mvua Mbinu za Kale na za Sasa
Kuhifadhi Maji ya Mvua Mbinu za Kale na za Sasa
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA
KWA maelfu ya miaka, maji yaleyale yametumiwa tena na tena kupitia kuvukizwa kwa maji yaliyo ardhini na baharini, kufanyizwa kwa mawingu, na kunyesha. Mfumo huo huandaa maji ya kumtosha kila mtu duniani. Basi kwa nini wanadamu wanapatwa na matatizo makubwa ya maji? Matatizo hayo yanaweza kusuluhishwaje? Ili kupata jibu, acheni tuchunguze hali ya maji nchini India.
Kwa kuwa nchi ya India ina idadi ya watu zaidi ya bilioni moja, vyanzo vyake vya maji vinatumiwa kupita kiasi. Maji yanayotumiwa India hutoka wapi? Huko kaskazini ya mbali, maji ya mito hutoka katika theluji na mabamba ya barafu yanayoyeyuka katika Milima ya Himalaya. Lakini sehemu kubwa ya India hutegemea mvua za msimu ili kulowesha ardhi iliyokauka, kujaza visima, maziwa, na mito mikubwa inayopita katika nchi hiyo. Mvua za msimu za India zimefafanuliwa kuwa “mojawapo ya mambo magumu zaidi kutabiriwa,” ambayo “licha ya kuwa na maendeleo makubwa ya kiteknolojia, yaani, kuwepo kwa setilaiti na kompyuta zenye nguvu sana . . . , bado ni vigumu kuzitabiri.”
Mvua za kawaida za msimu hudumu kwa miezi mitatu au minne, lakini badala ya kunyesha kwa kipindi hicho chote, mvua nyingi hunyesha kwa vipindi vifupi. Kwa hiyo, mabwawa hujaa maji na hivyo lazima yafunguliwe. Mito hufurika na kujaza maji kwenye mashamba na nyumba. Kwa sababu ya kuongezeka kwa viwanda vya kisasa na watu kuhamia mijini, misitu mingi imeharibiwa, na hivyo hakuna miti ya kutosha kuzuia maji katika mizizi na kuifanya iloweshe ardhi polepole. Kwa hiyo, maji hayo huondoa tabaka la juu la udongo na kumomonyoa ardhi. Mchanga-tope hujaa katika maziwa na mabwawa na kupunguza kina chake hivi kwamba haziwezi kuhifadhi maji mengi. Kwa hiyo maji mengi ya mvua hayatumiwi inavyofaa.
Kisha kipindi cha mvua za msimu huisha. Katika sehemu inayobaki ya mwaka, kutia ndani miezi yenye joto kali, jua huwaka kila siku! Ardhi hukauka haraka na mashamba huunguzwa na kufanyiza nyufa. Mito mikubwa hukauka na kuwa vijito vidogo. Maporomoko ya maji hutoweka. Visima huchimbwa chini zaidi ili kupata maji yaliyo chini ya ardhi, nalo tabaka la maji hushuka. Mvua inapopungua, ukame hutokea, mazao huwa machache, mifugo hufa, nao watu wanaoishi vijijini huhamia mijini na hivyo kuongeza tatizo la maji.
Lakini hali haikuwa hivyo nyakati zote. Katika nyakati za kale watu kotekote India walijifunza kwamba si vizuri kutegemea tu mito na maziwa ambayo yangekauka baada ya mvua za msimu kupita. Walibuni njia ya kuhifadhi maji ya mvua, na kuyatumia kwa ajili ya mahitaji yao ya wakati huo na pia kuyahifadhi kwa ajili ya kipindi kisicho na mvua. Hiyo ilikuwa mbinu ya kuhifadhi maji ya mvua.
Umuhimu wa Kuhifadhi Maji ya Mvua Leo
Mtu anaweza kufikiri kwamba hakuna haja kuchunguza mbinu za kale za kuhifadhi maji kwa kuwa kuna teknolojia ya kisasa na mabwawa makubwa, madimbwi, na mifereji ya kumwagilia mashamba maji, ambayo tayari yalipatikana nchini India kwa wingi. Isitoshe, mbinu hizo zilipotelea mbali wakati watu walipopata maji ya mabomba katika nyumba au vijiji vyao. Lakini kuna sababu ya kuhangaika. Kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, miradi mikubwa ya maji haijafaulu kutatua tatizo la ongezeko la idadi kubwa ya watu na mabadiliko makubwa ambayo yamefanywa kutoka kuwa jamii ya wakulima mpaka kuwa jamii iliyoendelea kiviwanda. Maji ya kutosha ili kutosheleza mahitaji ya taifa zima hayajahifadhiwa bado.
Sasa wanamazingira na wasimamizi wa maji wanahisi kwamba kuna uhitaji wa kuwachochea watu binafsi wahifadhi maji. Watu wanatiwa moyo wahifadhi maji nyumbani, viwandani, shuleni, na mahali popote pale ambapo inawezekana kuhifadhi maji kwa kiwango kidogo. Hata majiji na majimbo mengi yameweka sheria kwamba kila nyumba mpya inayojengwa iwe na vifaa vya kuhifadhi maji ya mvua!
Mamilioni ya lita za maji ya mvua hunyesha katika maeneo ambapo hayaelekezwi katika vyombo vya kuhifadhia lakini yanavukizwa au kupotelea baharini. Hata hivyo, mbinu za kuhifadhi maji ya mvua zinategemea dhana ya kuhifadhi maji mahali yanapomwagika. Maji ya mvua huhifadhiwa na mtu mmojammoja. Tofauti na maji ya mabwawa na mifereji ambayo lazima watu maskini wayalipie, maji ya mvua ni ya bure.
Kuchukua Hatua ya Kwanza
Kwa hiyo, watu wengi wanaohangaika nchini India wanajihusisha na miradi ya kuhifadhi maji. Wengine wao wametambuliwa kimataifa kwa kupewa tuzo, kama vile Rajendra Singh aliyepokea tuzo maarufu ya Magsaysay katika mwaka wa 2001 kwa kuhusika katika miradi ya maendeleo ya jamii. Akifanya kazi na shirika lisilo la kiserikali aliloanzisha, Singh alifufua mradi uliokuwa karibu kukwama wa Mto Aravari katika jimbo la Rajasthan, jambo lililonufaisha asilimia 8 ya wakaaji wa nchi hiyo kwa kutumia asilimia 1 tu ya maji yaliyopatikana huko. Kwa zaidi ya miaka 15, kikundi cha Singh kilipanda miti na kutengeneza matangi 3,500 ya kienyeji yanayoitwa johads kwa ajili ya kuhifadhia maji na hivyo kuleta ufanisi kwa wanakijiji hao. Wengine walifanya kazi ya kuhifadhi maji ambayo haikutambuliwa na wengi, lakini waliridhika kwa sababu ya msaada waliotoa.
Wenye viwanda wanaona manufaa ya kutumia maji ya mvua waliyohifadhi badala ya kutegemea tu maji yanayotolewa na jiji. Kwenye kiwanda fulani katika vitongoji vya Bangalore, kusini mwa India, njia rahisi, isiyo ghali ya kuhifadhi maji kutoka kwenye paa ilianzishwa. Maji ya mvua ambayo hapo awali yalipotea tu barabarani, sasa yanaelekezwa kwenye tangi linaloweza kuhifadhi lita 42,000 za maji. Wakati wa mvua za msimu, lita 6,000 za maji yaliyohifadhiwa hutumiwa kila siku kusafisha vyombo vya chakula na mkahawa wa kiwanda hicho. Maji yanayotolewa na jiji hayatumiwi kwa kazi hizo.
Huenda ukasema, ‘hilo ni tone tu katika ndoo.’ Lakini wazia kwamba una akaunti ya benki ambayo huongezwa pesa mara moja kwa mwaka. Ili kutosheleza mahitaji yako ya kila siku, inakubidi kutoa kiasi fulani kutoka kwenye akaunti hiyo, lakini pole kwa pole unachukua pesa nyingi kuliko zile ulizo nazo. Siku moja utakuwa na deni. Hata hivyo, ikiwa katika miezi michache utapata kazi inayokupa mshahara unaozidi ule unaohitaji kugharimia mahitaji yako ya kila siku, huenda ukaongeza pesa kwenye akaunti yako. Sasa jaribu kulinganisha kanuni hiyo na kuhifadhi maji. Ukizidisha akiba yako kwa milioni utapata nini? Vyanzo vya maji vitarudishwa, tabaka la maji litainuka, visima vitajaa, nawe utakuwa na maji ya kutumia wakati mvua zitakapokwisha. Kumbuka kwamba maji ni machache, hivyo hakuna kukopa.
Suluhisho la Kudumu
Sayari yetu ina maji ya kuwatosha wakaaji wake. Hata hivyo, kwa karne nyingi pupa na kutofikiri kwa wanadamu kumefanya mamilioni ya wakaaji wa dunia waishi katika hali ngumu. Licha ya jitihada za wanadamu wanyoofu, ni wazi kwamba wanadamu hawana uwezo wa kuondoa kabisa matatizo ya kimazingira yanayoikumba dunia. Jambo la kufurahisha ni kwamba Muumba wa dunia ameahidi kuwa ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia’ na kurudisha usawaziko wa mzunguko wa maji ili ‘maji yabubujike katika nyika, na mito katika nchi tambarare ya jangwani.’ Kwa kweli, “nchi iliyokaushwa na joto itakuwa kama dimbwi lenye matete, na nchi yenye kiu kama mabubujiko ya maji.” Bila shaka, wakati huo maji ya mvua yatahifadhiwa katika njia yenye kuburudisha sana.—Ufunuo 11:18; Isaya 35:6, 7.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]
Kutumia Tena Mbinu za Kale za Kuhifadhi Maji ya Mvua
MAJI KUTOKA KWENYE PAA: Ni rahisi na hayana gharama. Paa zilizoinamishwa kidogo huruhusu maji yateremke kupitia michirizi, mabomba, na kuingia katika matangi ya pekee. Vichujio vya waya, mchanga, kokoto, na makaa husafisha maji hayo. Huingizwa katika vifaa vya kuhifadhia maji chini ya ardhi au matangi yaliyo juu ya ardhi. Matangi hayo huzibwa ili hewa, nuru ya jua, na uchafu usiingie; huwekwa dawa ya alum ambayo hupunguza matope; na dawa ya klorini inayoua bakteria. Maji hayo yanaweza kutumiwa kumwagilia bustani, kusafisha choo, kufulia nguo. Yakiwekwa dawa zaidi yanaweza kunywewa. Maji ya ziada yanaweza kuhifadhiwa katika visima au yanaweza kuhifadhiwa katika tabaka la maji lililo chini ya ardhi. Hutumiwa sana mijini.
NAULAS: Kuta za mawe zilizojengwa kwenye kijito ili kuhifadhi maji hayo katika bwawa. Miti yenye kivuli iliyopandwa kandokando hupunguza kiasi cha maji yanayovukizwa, nayo mimea yenye dawa ambayo hutupwa ndani ya hifadhi hizo ndogo husafisha maji hayo.
MATANGI YA KUCHUJIA, RAPATS: Matangi madogo yaliyojengwa juu ya mchanga au udongo wenye mawemawe ili kuhifadhi maji ya mvua. Kiasi fulani cha maji hayo hutumiwa, lakini kile kinachosalia hujichuja na kuingia kwenye visima vya chini na kuvijaza tena.
BHANDARAS: Matangi yaliyo chini ya ardhi ambayo yamejengwa ili kutega maji yanayotoka kwenye chemchemi, na kuyaelekeza kwenye matangi ya kuhifadhia maji ya kutumiwa jijini.
QANATS: Mabomba yaliyo wima kwenye maeneo ya mlima ili kutega maji ya mvua. Maji hayo hukusanywa katika mifereji ya chini ya ardhi ambayo huyaelekeza kwenye matangi ya kuhifadhia maji yaliyo mbali.
MATANGI YALIYOUNGANISHWA: Matangi ya kukusanya maji ya mvua kwenye michirizi. Tangi la juu likijaa, maji hayo huingia kwenye matangi mengine yaliyo chini.
[Hisani]
Courtesy: S. Vishwanath, Rainwater Club, Bangalore, India
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]
◀ UN/DPI Photo by Evan Schneider
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]
UN/DPI Photo by Evan Schneider ▶