Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wenzi Wasio wa Kawaida

Wenzi Wasio wa Kawaida

Wenzi Wasio wa Kawaida

Hivi majuzi wanasayansi wanaochunguza viumbe walio majini katika eneo lililo karibu na Tumbawe Kubwa la Australia, walimwona pweza wa kiume aliye hai wa aina ya blanket kwa mara ya kwanza kabisa walipokuwa wakipiga mbizi usiku. Kwa nini hilo lilikuwa jambo lisilo la kawaida?

Kwa kufaa pweza wa jamii hiyo hufafanuliwa kuwa “kiumbe wa kiume anayetofautiana sana kwa ukubwa na yule wa kike miongoni mwa viumbe wakubwa.” Pweza wa kike hukua kufikia urefu wa meta mbili na uzito wa kilo kumi. Lakini pweza wa kiume huwa na urefu wa sentimeta tatu tu na uzito wa gramu 0.3! Kwa kweli, ukubwa wa pweza wa kiume unakaribia kutoshana na mboni ya jicho la pweza wa kike. Hiyo inamaanisha kwamba uzito wa pweza wa kike unaweza kuzidi ule wa pweza wa kiume mara 40,000 hivi. Inaonekana kwamba tofauti hiyo ya ukubwa ndiyo kubwa zaidi katika jamii za wanyama wakubwa. Pweza huyo huishi baharini, na kufikia sasa pweza waliovuliwa na kuchunguzwa ni wale wa kiume waliokufa na wa kike.

Kwa kuwa wanatofautiana sana kwa ukubwa, wao hujamiiana jinsi gani? Sehemu ya ndani ya mojawapo ya miguu minane ya pweza wa kiume haina kitu. Baada ya kumpata pweza wa kike, mguu huo hujaa mbegu za uzazi za kiume. Kisha mguu huo huvunjika na kuingia katika mwili wa pweza wa kike. Mguu huo hukaa ndani yake hadi anapoyatungisha mayai yake kwa kuufinya mguu huo na kumwaga mbegu hizo juu ya mayai hayo.

Kwa kuwa pweza wa kiume ni mdogo, yeye hujikinga kwa kutumia minyiri ambayo yeye humnyang’anya yavuyavu na kuzishika katika sehemu ya juu ya mikono yake. Hata hivyo, minyiri hiyo haiwezi kumwokoa, kwa kuwa anapomaliza kujamiiana, yeye hufa. Basi si ajabu kwamba wanasayansi walishangaa kumwona pweza wa kiume aliye hai!

Ijapokuwa hatujui sababu inayofanya pweza wa kiume wa aina ya blanket awe mdogo sana kuliko pweza wa kike, maneno haya ya Biblia ni ya kweli: “Na kwa habari ya bahari hii iliyo kubwa na pana, humo mna vitu vyenye kutambaa visivyo na hesabu, viumbe hai, vidogo kwa vikubwa.”—Zaburi 104:25.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Pweza wa kike: ana urefu wa karibu meta mbili na uzito wa kilo kumi

Pweza wa kiume: ana urefu wa sentimeta tatu na uzito wa gramu 0.3

Ukubwa kamili wa pweza wa kiume akilinganishwa na wa kike

[Hisani]

Female: Photo P. Wirtz; male: Photo: D. Paul