Wadudu Maridadi Kama Vito
Wadudu Maridadi Kama Vito
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA
MITI mirefu ya msitu wa mvua wa kitropiki huficha maelfu ya viumbe walio kama vito. Wengine wanametameta kama dhahabu na fedha, wengine kama zumaridi, zabarijadi, na yakuti. Viumbe hao walio kama vito, ambao mara nyingi hawaonekani na wanadamu, ni mbawakawa.
Wewe hufikiria nini unaposikia kuhusu mbawakawa? Je, wewe huwazia wadudu weusi wenye sura ya ajabu, wanaotambaa ardhini? Kwa kweli, mbawakawa ni miongoni mwa viumbe wengi zaidi na maridadi zaidi duniani. Kulingana na kitabu The Guinness Book of Animal Records, aina 400,000 hivi zinazojulikana za Coleoptera, ambacho ni kikundi cha wadudu kinachotia ndani mbawakawa, hufanyiza thuluthi moja hivi ya aina zote za wanyama wanaojulikana duniani. Na ikiwa unataka kuvumbua aina mpya, basi jaribu kuwachunguza mbawakawa. Dakt. Terry Erwin, ambaye ni mtaalamu wa wadudu, anasema kwamba huenda sayansi bado haijavumbua mamilioni ya aina za mbawakawa. Inapendeza kwamba Erwin alipata aina 1,200 za mbawakawa katika miti 19 mikubwa ya kitropiki.
Unamna-namna Wenye Kustaajabisha
Kwa kuwa kuna aina nyingi sana za mbawakawa, si ajabu kwamba kuna mbawakawa wenye maumbo na ukubwa mbalimbali. Gazeti National Geographic linasema kwamba mbawakawa fulani “ni wakubwa sana hivi kwamba watu waliokuwa wakiwakusanya zamani waliwaangusha chini kwa kuwafyatua kwa bunduki zenye
mchanga.” Pia gazeti hilo linasema kwamba wengine ni “wadogo sana hivi kwamba wao husafiri kwa kujishikilia kwenye midomo ya nyuki. Hata kuna mbawakawa wanaoshambulia majumba ya kuhifadhi vitu vya kale ili kula mbawakawa wenzao wanaohifadhiwa humo.”Unaweza kupata pesa nyingi kwa kukusanya mbawakawa. Bei ya mbawakawa hutegemea rangi yake na kupatikana kwake. Mbawakawa wa aina ya scarab wana rangi mbalimbali za kijani na nyekundu na vilevile za fedha na dhahabu. Kwa mfano, mbawakawa wa scarab mwenye rangi nyekundu nyangavu anaweza kuuzwa kwa dola 200, hali mwenye rangi ya dhahabu anaweza kuuzwa kwa zaidi ya dola 400.
Mbawakawa fulani wenye vipapasio virefu sana huwa na mapambo yenye rangi za kupendeza. Pia mbawakawa wengine humetameta sana. Rangi zao nyangavu za kijani na bluu ni kama zile za ndege wa humming. Si rangi zao tu zinazowafanya mbawakawa wawe wenye thamani. Kwa kuwa mbawakawa hula mimea inayooza na samadi, wao huchangia kusafisha mazingira.
Vito Vinavyotokana na Wadudu
Si wakusanyaji wa mbawakawa tu wanaovutiwa nao. Huko Amerika, wanawake wengine hutengeneza mikufu kwa kuunganisha mabawa maridadi ya mbawakawa kwa kamba. Katika maeneo fulani ya Mexico, mbawakawa wengine hupachikwa glasi zenye rangi na shanga kisha wanatumiwa kama vito kwa kuunganishwa kwenye nguo za watu kwa mnyororo mfupi.
Iwe unapendelea kuwatazama mbawakawa kutoka mbali au karibu, viumbe hao walio kama vito huonyesha waziwazi jinsi viumbe wanaopatikana duniani walivyo maridadi na tata.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]
Mbawakawa Wanaokula Majani
Hata hivyo, ingawa mbawakawa fulani ni maridadi, wanaweza kuharibu mimea. Kwa mfano, aina fulani hula majani, mashina, na mizizi ya mimea mingi.
Ingawa kuna aina 25,000 hivi za mbawakawa wanaokula majani, wakulima wengi wanajua aina moja tu, yaani, mbawakawa wa Colorado, ambao hula viazi. Wakazi wa Amerika Kaskazini waligundua kwa mara ya kwanza kwamba mbawakawa hao ni wavamizi wa mimea ya viazi katika mwaka wa 1859. Kufikia mwanzoni mwa karne ya 20, mbawakawa hao walikuwa wamevamia Ulaya, na sasa wameenea katika bara hilo na hata katika bara la Asia.
Kwa kuwa mbawakawa hao wamesitawisha uwezo wa kukinza dawa za kuwaua, wao ni maadui wakubwa. Leo, mbinu za kilimo, za kibiolojia, na za kikemikali zinatumiwa kudhibiti mbawakawa hao hatari wanaokula majani.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mbawakawa wa Colorado anayekula viazi, Marekani
[Hisani]
Scott Bauer/Agricultural Research Service, USDA
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
Mbawakawa wa Pekee
▪ Mbawakawa huishi kwa muda mrefu kuliko wadudu wengine. Ingawa wadudu wengi huishi kwa muda usiozidi mwaka mmoja, mbawakawa fulani wanaotumiwa kutengeneza vito huishi kwa zaidi ya miaka 30, na inasemekana mmoja aliishi kwa miaka 47. Mbawakawa hao “hutaga mayai ndani ya gamba la mti,” chasema kitabu The Guinness Book of Animal Records. “Mti huo unapokatwa, nyakati nyingine baadhi ya mabuu hubaki na husafirishwa hadi sehemu mbalimbali za ulimwengu yakiwa ndani ya mbao; kwa kuwa aina fulani hukomaa baada ya miaka mingi, si ajabu kuona mbawakawa waliokomaa wakitoka nje ya vyombo vilivyotengenezwa kwa mbao hizo.”
▪ Mbawakawa wa Goliathi wa maeneo ya kitropiki ya Afrika ndio wadudu wazito zaidi. Mbawakawa fulani wa kiume wanaweza kuwa na uzito wa gramu 100 hivi, yaani, mara tatu ya uzito wa panya wa kawaida.
▪ Mbawakawa wanaoweza kubeba vitu vizito zaidi (kulingana na uzito wao) ni wale wa rhinoceros wa jamii ya Dynastinae. Viumbe hao wenye nguvu wanaweza kubeba vitu vinavyozidi uzito wao mara 850.
[Picha]
Mbawakawa wa Goliathi, Jam. ya Kidemo. ya Kongo
[Hisani]
Faunia, Madrid
[Picha]
Mbawakawa wa rhinoceros, Equatorial Guinea
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mbawakawa anayetumiwa kutengeneza vito, Mexico
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mbawakawa anayetumiwa kutengeneza vito, Honduras
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mbawakawa anayetumiwa kutengeneza vito, Kosta Rika
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mbawakawa mwenye vipapasio virefu, Indonesia
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mbawakawa wa “scarab,” Thailand
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mbawakawa anayetoboa mbao, Thailand
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mbawakawa anayetoboa mbao, Hungaria
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mbawakawa anayetumiwa kutengeneza vito, Honduras
[Hisani]
Top left and middle: © David Hawks; right: © Barbara Strnadova/Photo Researchers, Inc.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Top left to right: First three: Faunia, Madrid; fourth: Gyorgy Csoka, Hungary Forest Research Institute, www.insectimages.org; fifth: © Barbara Strnadova/Photo Researchers, Inc.