Mbwa Mdogo Zaidi Duniani
Mbwa Mdogo Zaidi Duniani
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO
JE, UNATAFUTA mwandamani ambaye ni mchangamfu na mwenye urafiki, anayependa kulala kwa utulivu pajani mwako au kando yako unaposoma? Mwandamani anayekula chakula kidogo, asiyehitaji nafasi kubwa, na asiyehitaji mazoezi ya kila siku? Ikiwa ndivyo, yaelekea utafurahi kuwa na Chihuahua, anayeonwa kuwa mbwa mdogo zaidi duniani. *
Chihuahua ni walinzi wazuri kwani wanaweza kutoa onyo kwa kubweka. Kwa hakika, wao ni jasiri na hawatishwi hata kidogo na mbwa wakubwa.
Chihuahua ana kichwa chenye umbo zuri, nafasi kubwa katikati ya macho yake mawili, macho yanayong’aa, sura yenye kupendeza, na masikio yaliyosimama ambayo huinama anapopumzika. Chihuahua huwa na manyoya mafupi laini au manyoya marefu yanayofanana na hariri, nao wanaweza kuwa wa rangi mbalimbali kama vile nyekundu, manjano, bluu, au kahawia na pia wanaweza kuwa na mabaka au madoadoa. Jambo la pekee kuhusu Chihuahua wachanga ni kwamba wana sehemu laini kwenye utosi wa kichwa chao sawa na ile ya mtoto mchanga.
Walitoka Wapi?
Ingawa kuna dhana mbalimbali kuhusu chanzo cha Chihuahua, inaelekea kwamba walitokana na mbwa wadogo wanaoitwa Techichi. Mbwa hao walifugwa na Watolteki huko Mexico katika karne ya 9 W.K. Uthibitisho wa jambo hilo unapatikana katika makao ya watawa, yaliyojengwa huko Huejotzingo na watawa wa kiume wa Mtakatifu Francis, kwa mawe yaliyotolewa kwenye piramidi ya Cholula. Mawe hayo yana michoro ya kale inayofanana sana na mbwa wa Chihuahua wa leo.
Baadaye, Waazteki walipowashinda Watolteki, watawala wa Waazteki waliwachukua mbwa hao hasa wale wa bluu ili kuwatumia katika ibada. Iliaminika kwamba mbwa hao wangeweza kuongoza roho za wafu katika safari yao baada ya kifo. Montezuma wa Pili, aliyekuwa maliki wa mwisho wa Waazteki aliwapenda sana mbwa hao wa Chihuahua. Inasemekana kwamba alikuwa na mamia ya mbwa hao, kila mmoja akiwa na mtunzaji wake. Mifupa ya Chihuahua imepatikana ndani ya makaburi ya watu katika mpaka wa Mexico na Marekani.
Uchunguzi uliofanywa na mwanahistoria na mtaalamu wa mbwa wa Chihuahua, Thelma Gray, ulimfanya aamini kwamba mbwa hao walitokana na mbwa wa Waazteki na mbwa mwingine aliyeletwa na washindi wa vita Wahispania. Hivyo ikawezekana kutokeza Chihuahua wadogo zaidi wa leo. Mbwa hao huitwa Chihuahua kwa sababu katika miaka ya katikati ya 1800, wasafiri wa Marekani waliipata jamii hiyo ya mbwa katika jimbo la Chihuahua huko Mexico, nao wakarudi na baadhi ya mbwa hao Marekani. Karibu wakati huohuo, Carlotta, mke wa Maliki Maximilian wa Mexico, aliwapeleka mbwa hao Ulaya na hivyo akafanya wajulikane sana ulimwenguni.
Kumfuga Chihuahua
Chihuahua hufaa sana kufugwa ndani ya nyumba, hasa katika nyumba za orofa nao huwafaa sana wazee-wazee, walemavu, au watu wanaoshinda
nyumbani. Wao husitawi sana wanapotunzwa na kupapaswa-papaswa na watu. Hata hivyo, uangalifu unahitajiwa kwa sababu wao ni wadogo sana. Wanaweza kujeruhiwa vibaya au kuuawa wakikanyagwa, kukaliwa, au kufinywa sana. Hawapaswi kuachwa peke yao mahali palipoinuka, kama vile vitandani na kwenye viti kwani hawawezi kutambua urefu na hivyo wanaweza kuruka na kuvunjika. Basi, haipendekezwi mbwa hao watunzwe na watoto wadogo.Ingawa hivyo, Chihuahua ni mbwa sugu. Kwa hakika, yeye ni kati ya mbwa wanaoishi muda mrefu zaidi kwani wao huishi kwa karibu miaka 19. Mbwa huyo ni mwenye nguvu na hupenda kucheza sana, na hivyo hahitaji mazoezi mengine. Hata hivyo, kwa kuwa anatumia kalori haraka kuliko jamii kubwa ya mbwa na ana mfumo mdogo wa kusaga chakula, yeye hupatwa kwa urahisi na ugonjwa wa sukari. Hivyo, mara kwa mara anahitaji kupewa kiasi kidogo tu cha chakula na kupumzika sana. Kwa kawaida Chihuahua hutetemeka. Mbwa huyu hatetemeki tu wakati wa baridi, bali pia anaposisimuka au kuogopa.
Chihuahua ni mwaminifu, hufurahisha, na hufundishika kwa urahisi. Kitabu A New Owner’s Guide to Chihuahuas chasema: “Ikiwa uko tayari kumfuga Chihuahua, utatambua kwamba ndiye mbwa mwenye urafiki na mwenye kubadilikana sana kulingana na hali.” Watu wengi wametambua kwamba Chihuahua ni mwandamani bora.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Chihuahua ndio jamii ya mbwa-vipenzi wadogo zaidi “kiasili,” yaani, mbwa pekee walio wadogo wasiozalishwa kutokana na mbwa wengine wakubwa wa jamii yao.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mtoto wa paka na mtoto wa “Chihuahua”
[Hisani]
© Tim Davis/CORBIS
[Picha katika ukurasa wa 15]
“Chihuahua” mkubwa