Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Mahubiri Yauzwa
“Sala za makasisi wenye shughuli nyingi ambao huona ugumu kutayarisha mahubiri yao zimejibiwa: kituo kipya kwenye Intaneti chenye mahubiri kwa ajili ya pindi zote kimeanzishwa na mhudumu wa Kanisa la Anglikana,” laripoti gazeti The Daily Telegraph la London. Mwanzilishi wa kituo hicho, Bob Austin, anasema: “Wahubiri wana shughuli nyingi siku hizi na mahubiri hayatiliwi maanani sana.” Anadai kwamba katika kituo chake kuna mahubiri “yenye busara na yaliyo tayari,” ambayo “yanasisimua, yanachochea, na kuelimisha.” Kulingana na gazeti hilo, kufikia sasa kituo hicho “kina zaidi ya mahubiri 50 ‘yaliyojaribiwa kanisani’ kuhusu maandiko na vichwa mbalimbali vya Biblia,” lakini hayahusishi maoni ya kupita kiasi au mafundisho yanayoweza kuzua ubishi. Mahubiri hayo yanayofafanuliwa kuwa “mahubiri ya dakika 10 hadi 12 yanayoeleweka kwa urahisi na waumini,” yanagharimu dola 13.
“Mfalme na Bwana wa Jiji”
“Magari yamekuwa mfalme na bwana wa jiji,” laripoti gazeti Reforma la Mexico City. Katika mwaka wa 1970, kulikuwa na gari moja kwa kila watu 12,423 katika maeneo ya mjini. Kufikia mwaka wa 2003, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka na kufikia gari moja hivi kwa kila watu 6. Magari mengi yanaongezeka katika barabara za Mexico City hivi kwamba katika mwaka wa 2002, magari mapya yaliyoandikishwa katika jiji hilo lenye wakazi milioni 18 yalikuwa mengi zaidi ya idadi ya watoto waliozaliwa na kuandikishwa. Ubaya ni kwamba asilimia 80 ya uchafuzi wa hewa katika jiji hilo umesababishwa na magari. Isitoshe, wale wanaoenda kazini kwa magari wanaweza kutumia saa tatu hivi kwa sababu ya msongamano wa magari katika barabara za jiji. Inakadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2010, kutakuwa na magari milioni moja zaidi katika Mexico City.
Madeni Yanazidi Nchini Uingereza
Kulingana na gazeti The Daily Telegraph la London, “huenda madeni nchini Uingereza yakadhoofisha uchumi na kufanya robo ya watu wawe na matatizo makubwa ya kiuchumi. Raia wa nchi hiyo wamezoea kununua vitu kwa mkopo na wana madeni yapatayo dola trilioni 1.49.” Bila kutia ndani malipo ya mikopo iliyowekewa rehani, kwa wastani kila Mwingereza ana deni la dola 5,737 kutokana na kadi za mikopo, mikopo ya kibinafsi, na madeni katika akiba ya benki. Hivyo, “watu wengi sana wanapambana na madeni ambayo wanahofia kwamba hawataweza kuyalipa” hasa ikiwa viwango vya riba na vya ukosefu wa kazi vitaongezeka. Frances Walker wa Shirika la Kutoa Mashauri Kuhusu Mikopo anashauri hivi: “Ikiwa unatumia zaidi ya asilimia 20 ya mshahara wako wa kila mwezi kulipia madeni, bila kutia ndani malipo ya mikopo iliyowekewa rehani, basi unatumia pesa nyingi kuliko uwezo wako.” Licha ya maonyo hayo, Waingereza walitarajiwa kukopa dola bilioni 5 zaidi kwa ajili ya likizo katika mwaka wa 2003.
Je, Ng’ombe Ana Thamani Kuliko Mwanadamu?
Tofauti iliyopo kati ya matajiri na maskini inazidi kuongezeka. Kwa muda wa miaka 20 iliyopita, kiwango cha biashara inayofanywa na nchi maskini zaidi ulimwenguni (zenye wakazi milioni 700) kimepungua kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.6 ya jumla ya biashara zote zinazofanywa ulimwenguni. “Idadi kubwa ya Waafrika weusi ni maskini zaidi leo kuliko walivyokuwa kizazi kimoja kilichopita,” anaandika Philippe Jurgensen, mtaalamu wa uchumi wa Ufaransa katika gazeti Challenges. Kwa mfano, nchini Ethiopia watu milioni 67 huishi kwa thuluthi moja ya jumla ya mali zote za wakazi 400,000 wa Luxembourg. Jurgensen anasema kwamba wakulima wa Ulaya wanapaswa kupokea dola 3 kwa kila ng’ombe wanayefuga, hali kiasi ambacho watu bilioni 2.5 hivi wanatumia kila siku kinapungua dola hizo. Kwa hiyo, kulingana na Jurgensen, katika sehemu nyingi ulimwenguni, “ng’ombe ana thamani kubwa kuliko mtu maskini.”
Muziki na Jeuri
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Iowa na Wizara ya Huduma za Jamii huko Texas (Marekani) walifanya majaribio matano yaliyohusisha zaidi ya wanafunzi 500 wa vyuo ili kuchunguza athari za nyimbo zenye jeuri. Baada ya kusikiliza nyimbo kadhaa zenye jeuri na zisizo na jeuri ambazo ziliimbwa na mwanamuziki mmoja, wanafunzi walichunguzwa kwa njia mbalimbali ili kutambua viwango vyao vya jeuri. Uchunguzi huo uliochapishwa katika gazeti Journal of Personality and Social Psychology ulionyesha kwamba huenda nyimbo zenye jeuri zikachangia sana hisia na maoni ya jeuri hata bila kuchokozwa. Kiongozi wa utafiti huo Craig Anderson alisema kwamba “jambo moja kuu linalobainishwa na uchunguzi huu na mwingine kuhusu burudani yenye jeuri ni kwamba maneno ya muziki yana athari.” Anderson aliongezea hivi: “Wanunuzi wote wanapaswa kuzingatia jambo hilo, hasa wazazi walio na watoto na vijana waliobalehe.”
Watoto Walevi
Huko Uingereza, uchunguzi uliofanywa katika idara za misiba na hali za dharura katika hospitali 50 umefunua kwamba “hata watoto wenye umri wa miaka sita wanalazwa hospitalini baada ya kunywa kupindukia,” linaripoti gazeti The Daily Telegraph la London. Katika hospitali moja, madaktari na wauguzi walisema kwamba waliwatibu watoto walevi wapatao 100 kwa juma wakati wa likizo ya kiangazi. Kulingana na gazeti hilo, “zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi waliamini kwamba watoto wachanga zaidi na zaidi walikuwa wakilazwa hospitalini kwa sababu ya kulewa.” Pia, ripoti ya karibuni ya serikali inaonyesha kwamba vifo vinavyosababishwa na pombe huko Uingereza vimeongezeka mara tatu kwa muda wa miaka 20.
Dawa za Kulevya na Vijana wa Italia
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya San Raffaele ya Milan, asilimia 42 ya vijana wa Italia waliochunguzwa, wenye umri wa miaka 14 hadi 19, walikubali kwamba wanatumia dawa za kulevya. Hata hivyo, Mariolina Moioli, mkurugenzi-mkuu katika Wizara ya Elimu ya Italia anasema kwamba vijana wengi zaidi wanatumia dawa za kulevya. Dawa ya kulevya inayotumiwa sana ni bangi. Kati ya wanafunzi hao wanaotumia dawa za kulevya, asilimia 34 walisema wanazitumia shuleni, asilimia 27 kwenye disko, na asilimia 17 nyumbani. Uchunguzi huo pia ulifunua kwamba asilimia 82 ya wanafunzi hao hunywa pombe.
Ngisi Mkubwa Ajabu
Kulingana na gazeti The Daily Telegraph la Australia, “ngisi mmoja hatari wa ajabu mwenye macho makubwa kama sahani na minyiri mikali kama wembe, anayoitumia kukamata windo lake, amekamatwa na wavuvi karibu na ufuo wa Antaktika.” Mwanabiolojia wa mambo ya baharini huko New Zealand, Steve O’Shea alisema hivi: “Nimeona ngisi wakubwa, lakini huyo ni wa ajabu.” Inaonekana ngisi huyo mkubwa ajabu (Mesonychoteuthis hamiltoni), mwenye uzito wa kilo 150 ni mtoto. Mwanabiolojia wa mambo ya baharini Mmarekani, Kat Bolstad, alisema hivi: “Huyo ni mnyama mkali sana. Ukianguka kando yake majini, utakuwa taabani.” Kulingana na shirika la habari la Reuters, “ngisi huyo mkubwa hutafuta chakula kwa kung’aa ndani sana majini ili aweze kuona kwa macho yake makubwa, ambayo ni makubwa kuliko ya mnyama mwingine yeyote. . . . Mikono yake minane na minyiri yake miwili ina sehemu 25 zenye ncha kali kama meno ambazo zimeshikamana sana na misuli na zinaweza kuzunguka. Pia mikono yake ina viungo vya kujishikilia vinavyozuia samaki kutoroka.”