Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Majiji Nina umri wa miaka 13, na nilifurahia kusoma makala “Madrid—Jiji Kuu Lililojengwa kwa Ajili ya Mfalme” (Juni 22, 2003), “Barcelona—Jiji Lenye Sanaa na Mitindo ya Kuvutia” (Julai 8, 2003), na “Seville—Lango la Kuelekea Amerika” (Julai 22, 2003). Kwa kuwa mimi ni Mhispania anayeishi Ujerumani, nilifurahi kusoma kuhusu nchi yangu. Tafadhali endeleeni kuandika makala kama hizo.
C.G.R., Ujerumani
Kwa kawaida mimi hufurahia kusoma Amkeni! lakini ninapenda hasa makala zinazozungumzia nchi na majiji mbalimbali. Nilisisimuka kusoma makala kuhusu majiji ya Hispania. Kisha nilifurahia kusoma makala yenye kichwa “St. Petersburg Ni Njia ya Urusi ya Kuelekea Ulaya.” (Agosti 22, 2003) Ningependa sana kuona mandhari yake yenye kupendeza na wakati ambapo mchana ni mrefu. Makala hiyo ilinisaidia kuelewa hali za huko.
O.A.V., Urusi
Wadudu Asanteni sana kwa mfululizo wa makala “Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu,” ambao ulikuwa na sanduku lenye kichwa “Je, Wadudu Hueneza Virusi vya UKIMWI?” (Mei 22, 2003) Kwa miaka kadhaa sasa, nimeishi katika jiji lenye mbu wengi wakati wa kiangazi. Nimekuwa nikiogopa kwamba nitaambukizwa virusi vya UKIMWI. Kutokana na makala yenu sitakuwa na wasiwasi katika majira ya kiangazi!
J. L., Albania
Kutoka kwa Wasomaji Wetu Ninapenda kusoma makala ya “Kutoka kwa Wasomaji Wetu.” Wakati mwingine mimi hutumia maelezo ya wasomaji kuwatia moyo wale ninaojifunza nao Biblia kukazia fikira makala fulani. Makala hiyo inaonyesha kwamba jitihada zenu za kufikia mioyo ya watu si za bure.
S. A., Urusi
Kulala Nilisoma mfululizo wa makala “Je, Unalala vya Kutosha?” (Machi 22, 2003) kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kwa kawaida nimekuwa nikilala kwa saa mbili au tatu tu kila siku tangu nilipokuwa kijana. Gazeti hili limenisaidia kuona umuhimu wa kumwona daktari.
W. A., Taiwan
Maji Mimi ni mtaalamu wa mambo ya lishe na ya kudhibiti uzito wa mwili, na makala “Maji Ni Muhimu kwa Uhai” ilinifaa sana. (Juni 8, 2003) Mlieleza vizuri sana katika makala moja tu kila kitu nilichojifunza katika mafunzo ya saa 30 kuhusu lishe. Nakusudia kutumia habari hii kuwasaidia wateja wangu.
J.F.S.F., Brazili
Mshuko wa Moyo Baada ya Kujifungua Katika mwezi wa Aprili mimi na mume wangu tulipata mtoto. Baada ya mwana wetu kuzaliwa, nilianza kuhisi kama ilivyosimuliwa katika makala “Kuelewa Mshuko wa Moyo Baada ya Kujifungua.” (Juni 8, 2003) Kila mtu aliniambia kwamba mtoto wetu alikuwa mrembo sana, lakini sikutaka hata kumwona. Nilikaa nyumbani na kulia. Baada ya kusoma makala hiyo, nilimkumbatia mume wangu na kumweleza yaliyo moyoni. Alifurahi kuelewa mambo yaliyonifanya nibadilike. Nawashukuru kwa kuandika habari hii kwa busara. Mligusa moyo wangu.
S. V., Italia
Tour de France Niliamua kuandika insha kuhusu baiskeli. Makala “Tour de France—Miaka 100 ya Mashindano Makali ya Baiskeli” (Julai 8, 2003) ilikuja kwa wakati unaofaa! Hata niliwasomea wanafunzi wenzangu insha yangu. Nimetumia makala nyingi kutoka katika gazeti la Amkeni! kwa ajili ya kazi zangu za shule. Asanteni.
N. K., Ujerumani