Kinyonga Mjanja wa Baharini
Kinyonga Mjanja wa Baharini
“Pweza ni hatari kwa usalama! Anaweza kummeza mtu. Humvuta mtu, humtia mdomoni; na kwa kuwa amemfunga na kumlemaza, kiumbe huyo wa ajabu hummeza polepole.”—TOILERS OF THE SEA, CHA VICTOR HUGO.
MAMBO mengi mabaya yamesemwa kuhusu pweza. Hekaya na hadithi za ajabu, kama hadithi ambayo imenukuliwa hapo juu, zimemharibia sifa kiumbe huyo.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba pweza mkubwa sana wa Pasifiki anayeweza kufikia urefu wa meta 6 hivi na uzito wa karibu kilogramu 50, kwa kawaida si hatari kwa wanadamu. Katika miaka ya karibuni, hekaya za kustaajabisha kuhusu kiumbe huyo mwenye minyiri minane zimethibitishwa kuwa za uwongo. Wapiga-mbizi na wanabiolojia wa baharini wamejifunza mengi kuhusu aina mbalimbali za pweza.
Jinsi Anavyowinda na Kuwahepa Adui
Badala ya kula wanadamu, pweza hutumia minyiri yake minane na sehemu 1,600 hivi za kujishikilia ili kukamata hasa viumbe wadogo wenye magamba. Akitumia sehemu hizo za kujishikilia, pweza mdogo anaweza kuvuta kitu chenye uzito mara 20 kuliko uzito wake mwenyewe! Pweza wengine pia hunyunyizia mawindo yao sumu na kuyalemaza mara moja. * Kisha wao huvuta mawindo hayo na kuyaingiza mdomoni wakitumia taya zao zilizo kama mdomo wa ndege.
Vipi pweza akijipata anawindwa na mnyama mwingine? Maumbile yake humtia taabani. Damu yake ya bluu ambayo hutegemea kemikali ya hemocyanin badala ya himoglobini hubeba oksijeni kidogo. Kwa hiyo, yeye huchoka haraka. Hata hivyo ana ustadi wa pekee wa kujihami anaposhambuliwa na sili, nyangumi, na wawindaji wengine.
Kwa mfano, pweza anaweza kuruka kwa ustadi. Anapotishwa, yeye hujisukuma kinyumenyume kwa kutoa maji kupitia gamba lake zito. Kiumbe huyo mjanja ana mbinu nyingine ya kuhepa. Anaweza kutoa umajimaji wenye rangi ambao hauyeyuki kwenye maji. Anapofichwa na rangi hiyo, yeye humpiga chenga mwindaji wake kabla ya rangi hiyo kupungua.
Stadi wa Kujibadili
Bila shaka, pweza hapendi kujihatarisha. Yeye hujifichaje asipatikane na wawindaji? Mchunguzi mashuhuri wa bahari Jacques-Yves Cousteau, aliandika: “Huko
Marseilles mahali ambapo tulianza kuwapiga pweza picha, wapiga-mbizi wengi walisema kwamba hakukuwa na pweza wowote katika eneo hilo; au, kama walikuwapo mapema, walikuwa wameondoka. Hata hivyo, wapiga-mbizi hao walikuwa wakiogelea kando tu ya pweza hao, waliokuwa wamejificha wasiweze kuonekana hata kidogo.” Pweza hao walifanyaje hivyo?Pweza aliyekomaa ana chembe za rangi zipatazo milioni mbili kwenye ngozi yake, au chembe 200 kwa kila milimeta ya mraba. Kila chembe ina rangi nyekundu, ya manjano, au nyeusi. Kwa sekunde chache tu, pweza anaweza kutoa rangi nzito au mchanganyiko wa rangi anapokaza au kulegeza misuli iliyo karibu na chembe hizo.
Kwa kushangaza, inaonekana kwamba pweza hana uwezo wa kuona rangi mbalimbali. Hata hivyo, anaweza kutoa rangi nyingi kuliko zile tatu. Chembe fulani zinazong’aa hurudisha nuru ili kumfanya afanane na mazingira. Na mambo bado. Iwapo anajificha kwenye tumbawe, pweza anaweza kubadili ngozi yake na kufanyiza makunyanzi ili afanane na tumbawe hilo.
Fundi na Mtunzaji Stadi
Haishangazi kwamba ni vigumu kupata nyumba ya pweza. Pweza hupenda kujenga makao yao katika nyufa na chini ya miamba mikubwa wakitumia vifaa vinavyopatikana. Huenda paa na kuta za nyumba ya pweza zikawa na mawe, vipande vya vyuma, makoa, na hata mabaki ya meli zilizovunjika na takataka za baharini.
Baada ya kujenga makao yake, pweza huyatunza kwa ustadi. Yeye hunyunyiza maji ili kulainisha sakafu ya mchanga ya makao yake. Baada ya kula, yeye hutupa takataka nje. Kikundi cha wapiga-mbizi wa Cousteau kilitoa mawe machache kwenye ukuta wa makao ya pweza ili kuchunguza jinsi anavyotunza makao yake. Pweza huyo alifanya nini? Alirudisha jiwe moja baada ya lingine na kuujenga ukuta huo! Cousteau aliandika: “Pweza huyo aliendelea na kazi yake mpaka ukuta wote ulipokamilika, nao ulifanana kabisa na ule uliobomolewa na wapiga-mbizi.” Pweza anajulikana sana kwa kudumisha usafi na utaratibu katika makao yake. Wapiga-mbizi wanapoona mchanga au takataka ndani ya makao ya pweza, wanajua ni mahame.
Nyumba Yake ya Mwisho
Kwa kawaida, makao muhimu zaidi na ya mwisho ya pweza-jike ni mahali pake pa kutagia. Baada ya kupokea shahawa kutoka kwa dume na kuzihifadhi mpaka atakapotaga, yeye hutumia majuma kadhaa akitafuta makao yanayofaa. Halafu, yeye huimarisha makao hayo, kisha hubandika maelfu ya mayai kwenye paa katika mafungu-mafungu. Hata hivyo, yule pweza kutoka Australia, hajengi makao kama hayo. Kwa kuwa rangi zake nyangavu huwaonya wawindaji wasimkaribie,
anapendelea kuwatunza watoto wake baharini, ambapo anaweza kuwatahadharisha adui zake.Pweza-jike ni mama mwenye bidii. Baada ya kutaga mayai yake, huenda akakataa kula. Yeye huyalinda, huyasafisha, na kuyaruhusu yapate hewa, huimarisha makao yake, na kukaa chonjo akiyalinda dhidi ya wawindaji. Ingawa pweza-jike hufa baada ya kuangua mayai yake, yeye huyatunza hadi kifo chake. Cousteau alisema hivi: “Hakuna pweza-jike aliyeripotiwa kwamba aliyaacha mayai yake.”
Katika jamii nyingi za pweza, watoto huelea juu ya maji. Wengi wao huliwa na viumbe wengine wa baharini. Hata hivyo, baada ya majuma kadhaa, wale waliookoka hurudi chini ya bahari na kukomaa, nao huishi kwa miaka mitatu.
Wana Akili Kadiri Gani?
Watu fulani wanadokeza kwamba neno “akili” linapotumiwa kuhusu wanyama, linahusisha uwezo wa kujifunza kutokana na mambo yaliyowapata na kutatua matatizo. Kuhusiana na hilo, hebu fikiria maelezo haya ya Cousteau: “Woga wa pweza ni tendo la akili na tahadhari. . . . Mpiga-mbizi akionyesha kwamba hana nia ya kumdhuru, pweza huacha kuogopa haraka sana kuliko mnyama ‘mwitu’ yeyote.”
Pweza wana ubongo na macho ya hali ya juu zaidi kuliko wanyama wote wasio na uti wa mgongo. Kama macho ya wanadamu, macho yao yanaweza kukazwa na kubadilika kulingana na mwangaza. Sehemu ya ubongo inayohusiana na jicho hutafsiri habari zinazopokewa na jicho. Uwezo huo pamoja na hisi ya kugusa, humwezesha pweza kufanya maamuzi ya ajabu yanayoonyesha kwamba ana akili sana.
Wanasayansi kadhaa wamesema kwamba walimwona pweza akijifunza kufunua chupa ili afikie mnyama mdogo aliye ndani. Wengine kati yao wamesema kwamba pweza anaweza kugundua jinsi ya kutoa kifuniko cha chupa ili apate chakula kilichomo. Katika hifadhi ya viumbe wa baharini huko Vancouver, Kanada, pweza mmoja alikuwa akitoroka kila usiku kupitia bomba la kutoa maji na kwenda kula samaki katika chombo kilichokuwa karibu.
Kitabu Exploring the Secrets of Nature, kinasema hivi kuhusu akili ya pweza: “Kwa kawaida sisi husema kwamba mamalia ndio viumbe wenye akili nyingi zaidi, lakini kuna uthibitisho kwamba pweza ni kati ya wanyama wenye akili nyingi zaidi.”
Akili ya pweza inaweza kutukumbusha viumbe ambavyo Biblia inavitaja kuwa vina “hekima ya kisilika.” (Methali 30:24) Kwa kweli pweza ni viumbe wa ajabu. Tofauti na maoni ya Victor Hugo, wanasayansi na wapiga-mbizi hawamwogopi pweza. Wale wanaomchunguza pweza hustaajabishwa sana na kinyonga huyo mjanja wa baharini.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 6 Pweza fulani kutoka Australia ndiye tu anayeonwa kuwa hatari kwa wanadamu. Sumu yake inaweza kumfanya mtu ashindwe kupumua.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Aina ya pweza
[Hisani]
© Jeffrey Rosenfeld
[Picha katika ukurasa wa 16]
Pweza aliyejificha kabisa kwenye tumbawe huko Pasifiki, akiwa chini ya mdomo wa samaki mwindaji. Je, unaweza kumwona pweza huyo?
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Kuna aina mbalimbali za pweza wa rangi tofauti-tofauti
[Picha katika ukurasa wa 17]
Watoto wa pweza wanaelea juu ya maji
[Hisani]
© Fred Bavendam
[Picha katika ukurasa wa 16 zimeandaliwa na]
Top left: © Roger T. Hanlon; above: © Jeffrey Rosenfeld